Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. 

Baba Mtakatifu Francisko: Mahubiri ya Sherehe ya Pentekoste 2020

Baba Mtakatifu Francisko, ameadhimisha Sherehe ya Pentekoste, Jumapili tarehe 31 Mei 2020, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika mahubiri yake amekazia kuhusu: Karama za Roho Mtakatifu; Historia ya Pentekoste; Umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo; Roho Mtakatifu ndiye siri ya umoja na sadaka ya maisha kwa ajili ya jirani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Pentekoste inahitimisha kipindi cha Pasaka ya Kristo Yesu, kwa kumminina Roho Mtakatifu ambaye amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama Nafsi ya Mungu. Roho Mtakatifu ni Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya Manabii.Hii ni siku ambayo Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume; mwanzo wa maisha na utume wa Kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Hii ni Siku kuu ya waamini walei wanaohimizwa kutoka kifua mbele, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa karama na matunda ya Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko, ameadhimisha Sherehe ya Pentekoste, Jumapili tarehe 31 Mei 2020, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika mahubiri yake amekazia kuhusu: Karama za Roho Mtakatifu; Historia ya Pentekoste; Umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo; Roho Mtakatifu ndiye siri ya umoja na sadaka ya maisha kwa ajili ya jirani! Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho: 12:24 anaelezea kuhusu Karama za Roho Mtakatifu kwamba, kuna tofauti za karama, huduma na kutenda kazi, bali Roho ni yeye yule. Hapa kuna umoja na utofauti, kielelezo kwamba, Roho Mtakatifu ndiye anayeunganisha mambo kwa pamoja. Na kwa njia hii, Kanisa liliweza kuzaliwa. Kuna tofauti kubwa kati ya watu, lakini wote wanaunganishwa chini ya kifungo cha Roho Mtakatifu.

Mwanzo wa Pentekoste: Mitume wa Yesu walikuwa ni watu wa kawaida kabisa katika jamii, wengi wao walikuwa ni wavuvi na wengine walijipatia riziki yao kutokana na kazi za mikono yao. Lakini kuna baadhi waliobahatika kupata kiwango cha juu cha elimu kama Mathayo, kiasi cha kupewa dhamana ya kuwa ni mtoza ushuru. Mitume ni watu walitoka katika matabaka mbali mbali ya kijamii, baadhi yao walikuwa ni Wayahudi na wengine walikuwa na majina ya Kigiriki. Ni watu waliokuwa na tabia na maoni na vionjo tofauti katika maisha. Kristo Yesu, aliheshimu na kuthamini tofauti hizi msingi na kuwaunganisha kwa pamoja kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kumbe, umoja ni matokeo ya kushukiwa na Roho Mtakatifu na hii ndiyo nguvu inayowaunganisha kama wafuasi wa Kristo Yesu. Mitume waliweza kushuhudia kwa macho yao kwani watu wa Mungu waliweza kusema kwa lugha nyingine kama Roho Mtakatifu alivyowajalia kutamka, kwa sababu Roho Mtakatifu ni chemchemi ya umoja.

Msingi wa Umoja katika Kanisa mamboleo ni Roho Mtakatifu kwani hata waamini wa Kanisa Katoliki leo hii, wana: mawazo, vipaumbele vyao na miguso mbali mbali ya maisha. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kishawishi kikubwa ni kwa baadhi ya watu kutaka kukomalia zaidi mawazo yao kwa kudhani kwamba ndiyo bora zaidi kuliko ya wengine. Lakini hii ni imani inayotengenezwa na binadamu mwenyewe na wala si kama Roho Mtakatifu anavyotaka. Watu wanaunganishwa na imani, kanuni maadili lakini zaidi wanapaswa kutambua kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Mungu. Roho Mtakatifu anawashukia katika tofauti zao msingi, matatizo na changamoto za maisha, lakini Roho Mtakatifu anawakumbusha wanaye Bwana mmoja, Kristo Yesu na wana wa Baba mmoja, Mungu mwenyezi na wote ni ndugu wamoja.

Hii ni changamoto kwa waamini kuliangalia Kanisa kwa jicho la Roho Mtakatifu na wala si kama wanavyoliangalia walimwengu! Roho Mtakatifu anawaangalia kama watoto wa Baba mmoja na ndugu zake Kristo Yesu. Walimwengu wanaliona Kanisa kama taasisi iliyogawanyika katika makundi mawili; wafaidhina na watu wenye maendeleo, lakini Roho Mtakatifu anawaangalia wote kama watoto wa Mungu. Walimwengu wanaliangalia Kanisa kama miundo mbinu, bali kwa jicho la Roho Mtakatifu, wote ni ndugu wamoja wanaokimbilia huruma ya Mungu. Roho Mtakatifu anawapenda na kumkirimia kila mmoja wao nafasi yake inayothaminiwa sana! Kwa maadhimisho ya Pentekoste, Mitume wa Kristo Yesu walitambua kwamba, wanayo dhamana ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote bila ubaguzi. Roho Mtakatifu anawataka waamini wote kutangaza na kushudia imani na kumbu kumbu endelevu ya Kristo Yesu kati yao kwa njia ya umoja.

Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa umoja wa wale wanaotangaza na kushuhudia Injili. Mitume walikuwa na ari na mwamko wa kuwashirikisha watu wa Mungu kile ambacho walikuwa wamepokea! Roho Mtakatifu ni kiini cha siri ya umoja kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowashirikisha wengine, ili kuweza kumfahamu Mungu anayeleta mageuzi katika sakafu ya maisha ya mwamini. Waamini wakilitambua hili, wala hakuna sababu ya kuteseka kutafuta nafasi, kutambulikana au kuwa na uchu wa madaraka. Waamini wahakikishe kwamba, maisha yao yanakuwa pia ni zawadi. Kwa njia hii, wataweza: kupenda kwa unyenyekevu, kuhudumia kwa furaha na katika uhuru kamili, kama kielelezo cha sura ya kweli ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kuna maadui watatu wakuu wanaohatarisha zawadi hii ya Roho Mtakatifu: Ubabe! Waathirika! Walalamikaji wanaoona mabaya zaidi kuliko uzuri! Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, wababe ni wale wanaotaka kujinufaisha wao binafsi; kwa kudhani kwamba, wao ni tofauti sana na watu wengine, kiasi cha kushindwa kutambua na kukiri udhaifu na mapangufu yao ya kibinadamu.

Adui wa pili anasema Baba Mtakatifu ni wale watu wanaodhani kwamba, wao ni waathirika wa kwanza, wanaowalalamikia jirani zao kila kukicha, na kudhani kwamba, hakuna anayewapenda wala kuwajali. Hata katika hali ya sasa, ya janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kuna watu wanadhani kwamba wao ni waathirika wa kwanza! Baba Mtakatifu anakaza kusema, kundi la tatu ni watu wenye litania ya malalamiko kila kukicha, kiasi cha kushindwa kuona wema na uzuri unaobubujika kutoka katika jamii, masuala ya kisiasa na hata ndani ya Kanisa lenyewe. Hawa ni watu waliojikatia na kukata tamaa. Kwa hakika, walimwengu wanakabiliwa na ukame mkubwa wa fadhila ya matumaini, ili kuweza kufurahi zawadi ya maisha. Watu wa Mungu wanamhitaji Roho Mtakatifu, Zawadi ya Baba wa milele, ili aweze kuwaganga na kuwaponya kutoka katika magonjwa ya ubabe, kudhani kwamba wao ni waathirika wakuu pamoja na kuwaondoa kutoka katika “dimbwi” la litania ya walalamikaji.

Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu ambaye ni kumbu kumbu ya Baba wa milele, asaidie kupyaisha kumbu kumbu ya zawadi waliyokirimiwa. Awaokoe kutoka katika jangwa la ubinafsi na aweze kuamsha ndani mwao ari na moyo wa kuhudumia pamoja na kutenda mema. Janga hili kubwa la maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19, limewafanya watu wengi kuzama katika ubinafsi, kwa kujifungia katika undani wao. Roho Mtakatifu chemchemi ya amani na utulivu wa ndani, asaidie ujenzi wa umoja. Awawezeshe waamini kuwa na ujasiri wa kutoka katika ubinafsi wao, ili kupenda na kuwasaidia wengine, ili kujenga umoja na mshikamano wa familia moja ya binadamu!

Papa: Pentekoste

 

31 May 2020, 14:29