Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema anawaalika waamini kusikiliza sauti ya Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao yaani dhamiri. Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema anawaalika waamini kusikiliza sauti ya Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao yaani dhamiri. 

Jumapili ya Mchungaji Mwema! Sikilizeni Sauti ya Mungu! Dhamiri!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Tafakari ya Sala ya Malkia wa Mbingu aliyoitoa kwenye Maktaba yake, Jumapili tarehe 3 Mei 2020 amefafanua zaidi umuhimu wa kusikiliza sauti ya Mchungaji mwema inayomsukuma kondoo kujikita katika kipaji cha ubunifu wa upendo kwa kumfungulia Mwenyezi Mungu malango ya moyo wake, ili aweze kumkirimia amani na utulivu wa ndani. Dhamiri!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka maarufu kama Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema, ni Siku pia ya Kuombea Miito ndani ya Kanisa. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani kwa mwaka 2020 unaongozwa na kauli mbiu: “Jipeni Moyo Ni Mimi Msiogope: Maneno ya Miito”: Baba Mtakatifu anafafanua kwa kina kuhusu Mateso, Shukrani, Ujasiri na Sifa katika miito mbali mbali ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake! Baba Mtakatifu wakati wa Tafakari ya Sala ya Malkia wa Mbingu aliyoitoa kwenye Maktaba yake, Jumapili tarehe 3 Mei 2020 amefafanua zaidi umuhimu wa kusikiliza sauti ya Mchungaji mwema inayomsukuma kondoo kujikita katika kipaji cha ubunifu wa upendo kwa kumfungulia Mwenyezi Mungu malango ya moyo wake, ili aweze kumkirimia amani na utulivu wa ndani.

Mwinjili Yohane anasema “kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao”. Yn. 10:3. Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu anawaita waja wake kwa majina yao kwa sababu anawapenda upeo! Lakini Injili inaonya kwamba kuna sauti nyingine za wageni, ambazo kamwe hawapaswi kuzisikiliza wala kuzifuata kwa sababu hizi ni sauti za wevi, wanyang’anyi wanaotaka kuiba na kuchinja. Sauti hizi zinasikika katika undani wa maisha ya kila mwamini. Kuna sauti ya Mungu inayozungumza kutoka katika undani wa mtu mwenyewe yaani dhamiri nyofu, lakini pia kuna sauti ya Shetani, Ibilisi anayetaka kuwatumbukiza watu kwenye dimbwi la dhambi. Baba Mtakatifu anasema inawezekana kabisa kutambua sauti hizi mbili kwa sababu kila sauti ina mfumo wake wa pekee inapobisha katika mlango wa moyo wa mwamini.

Sauti ya Mwenyezi Mungu inashauri na kamwe haimlazimishi mtu kuifuata. Lakini sauti ya Shetani, Ibilisi inashawishi, inalaghai na kulazimisha: inaamsha mambo ya kufikirika, hisia zenye kuvutia lakini ambazo hazina mashiko hata kidogo! Mwanzoni, ushawishi huu unaweza kumwaminisha mtu kuwa ni maarufu lakini ni hali inayomwachia mtu utupu katika undani wake kiasi hata cha kumsuta mtu kwamba, “wewe si mali kitu”! Sauti ya Mwenyezi Mungu inamkosoa mtu kwa uvumilivu mkuu, lakini daima inawatia moyo waja wake; ni sauti inayofariji na daima inakoleza matumaini! Baba Mtakatifu anasema, sauti ya adui, Shetani, Ibilisi inamwondolea mwamini uhalisia wa maisha yake na kumtumbukiza katika hofu kwa siku za mbeleni au hata wakati mwingine, inamwingiza mtu katika huzuni za mambo yaliyopita; kwa kupyaisha machungu moyoni; makosa yaliyotendeka na zaidi sana, anawakumbusha wale wote waliowatenda jeuri!

Lakini sauti ya Mwenyezi Mungu inazungumzia hali halisi kwa kumtaka mwamini kutenda mema, kwa kumwilisha ubunifu wa fadhila ya upendo, ili kuondokana na yale mambo ya kale yanayoendelea kumtumbukiza katika giza la moyo wake! Hizi ni sauti mbili zinazoibua maswali tofauti. Kwa Shetani, Ibilisi swali linajikita zaidi katika ubinafsi, Je, ni kitu gani kinachonipendeza kufanya? Lakini sauti ya Mungu ina inamuuliza mwamini, Je, ni jambo gani jema linalonifaa? Sauti ya Shetani, Ibilisi inafumbatwa katika ubinafsi, vionjo na mahitaji yake na ni mambo yanayohitajika kwa haraka iwezekanavyo! Sauti ya Mwenyezi Mungu kamwe haitoa ahadi za furaha kwa gharama hafifu, lakini inawaalika waamini kwenda mbali zaidi na ubinafsi wao ili kupata chema cha kweli, yaani amani! Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, ubaya kamwe hauwezi kumlipa mtu amani, kwani kwanza unamtia mtu wazimu na kumwachia machungu moyoni.

Sauti ya Mwenyezi Mungu na ile ya Shetani, Ibilisi anasema Baba Mtakatifu Francisko zinazungumza katika mazingira mawili tofauti kabisa. Ibilisi anapendelea giza, uwongo na udaku; lakini Mwenyezi Mungu anapenda mwanga angavu wa jua, ukweli, uwazi na unyofu. Ibilisi atamtaka mwamini kujifungia katika ubinafsi wake, kwa kumwaminisha kwamba, hakuna anayeweza kumwelewa, kumsikiliza wala kumtumainia. Lakini, Mwenyezi Mungu anawataka waamini kuwa wakweli na wenye imani kwa Mungu na jirani zao. Katika hali na mazingira ya wakati huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna mawazo na maneno yanayowatatiza watu wengi, kiasi cha kuwalazimisha kuingia katika undani wao. Kumbe, kuna haja ya kuwa makini na sauti zinazobisha hodi katika malango ya nyoyo zao, ili kutambua mahali zinakotoka. Waamini wanaalikwa kutambua na kufuata sauti ya Kristo Mchungaji Mwema, anayewawezesha kondoo wake kutoka katika zizi la ubinafsi na kuwaongoza kweli malisho ya uhuru wa kweli. Bikira Maria, Mama wa Shauri Jema, asaidie kuongoza na kusindikiza mang’amuzi ya watu wa Mungu!

Papa: Yesu Mchungaji Mwema

 

03 May 2020, 14:21