Vatican News
Jumapili ya Mchungaji Mwema ni Siku ya Kuombea Miito Duniani: Ujumbe wa Papa Francisko: Jipeni Moyo ni Mimi! Msiogope: Maneno ya Miito: Mateso, Shukrani, Ujasiri na Sifa. Jumapili ya Mchungaji Mwema ni Siku ya Kuombea Miito Duniani: Ujumbe wa Papa Francisko: Jipeni Moyo ni Mimi! Msiogope: Maneno ya Miito: Mateso, Shukrani, Ujasiri na Sifa. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya 57 ya Kuombea Miito: 2020

Baba Mtakatifu Francisko anaweka mbele ya macho ya watu wa Mungu: “Maneno ya Miito”: Mateso, Shukrani, Ujasiri na Sifa. Ujumbe huu unaongozwa na sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo: 14: 22-33: Yesu anatembea juu ya maji, kielelezo cha taswira ya safari ya maisha ya waamini, mtumbwi wa safari ya maisha unatembea taratibu, ili kutafuta bandari salama! Msiogope!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema, ni Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani, ambayo inaadhimishwa tarehe 3 Mei 2020. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho haya unaongozwa na kauli mbiu: “Jipeni Moyo Ni Mimi Msiogope: Maneno ya Miito: Mateso, Shukrani, Ujasiri na Sifa. (Rej. Mt.14:22-33). Baba Mtakatifu katika barua aliyowaandikia Mapadre Wote Duniani kama kumbu kumbu ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Msimamizi wa Maparoko wote, aliwataka kukumbuka kwamba, wao ni marafiki wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwatia moyo Mapadre wote wakitambua kwamba, wao ni marafiki wa Kristo Yesu. Ameyaona mateso na mahangaiko ya watu wake, anasema, haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Mapadre, akiwakumbuka katika sala zake; anataka kuwafariji ili hatimaye, waweze kuimba ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha na utume wao!

Kwa ufupi Baba Mtakatifu anasema, katika mateso na mahangaiko katika historia na hasa pale watu wanapokaribia kuzama kutokana na dhoruba kali, Kristo Yesu anawanyooshea mkono wake na kuwakirimia ari na mwamko mpya wa kuishi wito wao kwa furaha na moyo mkuu. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anaweka mbele ya macho ya watu wa Mungu maneno makuu manne kuhusu miito: “Maneno ya Miito”: Mateso, Shukrani, Ujasiri na Sifa. Ujumbe huu unaongozwa na sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo Sura ya 14: 22-33: Yesu anatembea juu ya maji, kielelezo cha taswira ya safari ya maisha ya waamini, mtumbwi wa safari ya maisha unatembea taratibu, ili kutafuta bandari salama, tayari kukabiliana na changamoto pamoja na fursa zinazoweza kujitokeza baharini sanjari na kuwa na dira na mwelekeo sahihi wa maisha. Katika safari hii, waamini watambue kwamba, Kristo Yesu yuko tayari kupanda chomboni na kwa hakika upepo na dhoruba kali vitakoma!

Huu ndio uzoefu na mang’amuzi waliyokutana nayo Kristo Yesu na Petro Mtume. Baada ya Kristo Yesu kuwalisha watu zaidi ya elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, Yesu akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga makutano. Safari hii ya kuvuka kwenda ng’ambo ya pili inaweza kulinganishwa na safari ya maisha ya mwamini hapa duniani. Mtumbwi wa safari ya maisha unatembea taratibu, ili kutafuta bandari salama, tayari kukabiliana na changamoto pamoja na fursa zinazoweza kujitokeza baharini sanjari na kuwa na dira na mwelekeo sahihi wa maisha. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, wakati mwingine inaweza kutokea watu kupoteza dira na mwelekeo sahihi wa maisha na hivyo kujikuta wakizama katika ombwe badala ya kufuata mwanga angavu unaowaelekeza katika bandari salama! Wakati mwingine, wanatikiswa na mawimbi ya matatizo mazito, wasi wasi na woga.

Hivi ndivyo inavyotokea hata katika mioyo ya wale wote ambao wameitwa na kuchaguliwa kumfuasa Kristo Yesu, wanapaswa kufanya maamuzi magumu ili kuweza kuvuka na kwenda ng’ambo ya pili. Huu ni uamuzi unaopaswa kufanywa kwa ujasiri, ili kuachana na usalama binafsi na kujikita katika ufuasi wa Kristo Yesu. Safari hii ni hatari sana kwani wakati usiku wakati mwingine kuna upepo wa mbisho na chombo kinataabika sana, woga na wasi wasi vinawashika, kiasi cha kudhani kwamba, hawataweza kuwa na sifa za wito na maisha yao. Lakini, waamini wanakumbushwa kwamba, hatika safari hii ya maisha, yupo Kristo Yesu. Katika mapambazuko ya usiku wa moyo, Kristo Yesu anatembea juu ya bahari yenye mawimbi mazito ili kuwaendea wanafunzi wake! Yesu akamwalika Petro, ili aweze kumwendea, lakini akaogopa na kuanza kuzama, mara Yesu akanyoosha mkono wake akamshika na kumwokoa; nao walipopanda chomboni, upepo ukakoma.

Baba Mtakatifu Francisko anasema Neno la Kwanza Kuhusu Wito ni Shukrani: Safari ya wito yenye mwelekeo sahihi si jitihada, nguvu wala uchaguzi wa mtu binafsi. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, wito ni jibu la mwaliko kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si mradi wa mtu binafsi. Mwenyezi Mungu anawaonesha waja wake njia wanayopaswa kuifuata, anawapatia ujasiri wa kuweza kupanda chomboni na hatimaye, kuwaongoza na kuwasindikiza, ili waweze kutembea katika bahari shwari na wala wasigonge miamba. Kila wito unapata chimbuko lake kwa kukutana na Uso wa Kristo Yesu mwingi wa huruma, anayekuja wakati ambapo pengine mtumbwi ulikua unaanza kuzama. Ili kuweza kuendelea na safari kuna haja kwanza kabisa kwa waamini kumfungulia nyoyo zao kwa ukarimu na shukrani; pamoja na kumpokea Mwenyezi Mungu anayepita katika maisha ya waja wake.

Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakadhani ni kivuli na wakaanza kupiga yote kwa hofu. Lakini, Kristo Yesu akawahakikishia kwamba, ni Yeye mwenyewe wajipe moyo na wala wasiogope. Baba Mtakatifu anasema, Neno la Pili Kuhusu Wito ni Msiogope! Kile ambacho ni kikwazo katika safari, ukuaji na uchaguzi wa kufuata njia ile ambayo Mwenyezi Mungu amewaandalia kinaweza kulinganishwa na “Kivuli”. Hii ni changamoto kwa waamini kuachana na yale mambo ambayo wanadhani kwamba yanawahakikishia usalama, ili kukumbatia na kuambata mfumo wa maisha na wito maalum, iwe ni katika maisha ya Ndoa, Daraja Takatifu ya Upadre au maisha ya Kitawa. Waamini wajichunguze kutoka katika undani wao, ikiwa kama kweli wameitwa katika wito huo na kwamba, njia wanayoitumia ni sahihi! Waamini wasikubali kupoteza dira na mwelekeo hata kabla ya kuanza safari ya wito kwa kudhani kwamba, wameona “Kivuli”.

Baba Mtakatifu Francisko anasema Neno la Tatu Kuhusu Wito ni Ujasiri: Mwenyezi Mungu amefanya uamuzi mzito katika maisha  kama wito wa Ndoa, Maisha ya Kitawa na Kipadre, kwa ajili ya huduma kwa Mungu na waja wake. Wito huu unahitaji ujasiri. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu anatambua: maswali, hofu na matatizo yanayousonga mtumbwi wa nyoyo zao, ndiyo maana anapenda kuwahakikishia kwamba, wasiogope, kwa sababu Kristo Yesu, yuko pamoja nao. Waamini wanapaswa kuwa na imani katika uwepo wake, kwa sababu anawajia na kuwasindikiza hata kama kuna machafuko na mawimbi makubwa ya bahari! Kristo Yesu atawaokoa na hali ya mtu kujikatia tamaa kutoka katika undani wake, hali inayomfanya mtu kushindwa kufurahia utakatifu na uzuri wa wito wake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kila wito una matatizo, changamoto na fursa zake. Mwenyezi Mungu anawaita waja wake kwani anataka kama ilivyokuwa kwa Petro Mtume, watembee juu ya maji, yaani wawe na ujasiri wa kuratibu maisha yao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Injili inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Yesu mwenyewe anawaonesha mifumo mbali mbali ya miito wanayoweza kutekeleza kama: waamini walei, wakleri na watawa. Kama ilivyokuwa kwa Mitume, hata waamini wanao ujasiri, lakini pia wanaelemewa na udhaifu wao wa kibinadamu pamoja na hofu! Hapa kuna haja ya kila mwamini kuwajibika barabara katika maisha na wito wake kwa kumwangalia Kristo Yesu. Licha ya udhaifu wa kibinadamu na umaskini, lakini imani inawawezesha waamini kutoka kifua mbele na kuanza kutembea ili kukutana na Kristo Mfufuka na hatimaye, kuweza kudhibiti mawimbi mazito ya bahari. Kristo Yesu, yuko tayari kuwanyooshea mkono wale wote ambao wako hatarini kuzama kutokana na kuchoka au hofu na hivyo kuwakirimia ari na mwamko mpya wa kuweza kuishi wito wao kwa furaha na bashasha!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma, kielelezo makini cha matendo makuu ya Mungu katika maisha ya waja wake. Anazuia dhoruba na mawimbi mazito, anakemea na kutuliza nguvu za bahari kiasi kwamba, hofu na hali ya kukata tamaa havina nguvu tena katika maisha ya waja wake. Dhoruba na mawimbi mazito ya bahari ni mambo yanayoweza kumwandama mtu katika maisha na wito wake. Baba Mtakatifu anawakumbuka watu wenye dhamana ya uongozi katika jamii, watu wanaoishi katika ndoa na familia; watu wenye ujasiri mkubwa, kwani kwa hakika anasema Baba Mtakatifu yataka moyo mkuu! Si haba kwa watawa na wakleri wanaojisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, anatambua fika mateso na mahangaiko yao; upweke hasi ambao wakati mwingine unaugumisha moyo, tatizo la kufanya kazi kwa mazoea ambalo taratibu linazima moto wa ari na mwamko wa wito na kuanza kutembea katika wasi wasi na mashaka; kwa kuogopa ya mbeleni. Hata leo hii, Kristo Yesu anasema, Msiogope, Jipeni Moyo! Yeye yuko tayari kuwanyooshea mkono na kuwakoa kwa haraka!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Neno la Nne Kuhusu Wito ni Sifa! Licha ya mawimbi mazito ya bahari, lakini maisha na wito vinasimikwa katika utenzi wa sifa kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Bikira Maria anamshukuru Mungu kwa kumwangalia katika unyonge wake, kiasi kwamba, akaweza kujizatiti zaidi katika imani na hivyo kushinda hofu na mateso, kwa kukumbatia wito wake kwa ujasiri na moyo mkuu. Maisha yote ya Bikira Maria yakawa ni wimbo wa sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini katika Maadhimisho ya Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani, kuhakikisha kwamba, huduma ya kitume kwa ajili ya Jumuiya ya waamini, inakuwa ni fursa kwa kila mwamini kutambua kwa moyo wa shukrani wito wa maisha yake, tayari kuitikia na kusema, “Ndiyo” ili kushinda: hali, matatizo na changamoto za maisha katika imani kwa Kristo Yesu, ili kweli maisha yao, yaweze kuwa ni wimbo wa sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu, jirani na ulimwengu katika ujumla wake!

Papa: Ujumbe wa Siku ya 57 ya Miito 2020

 

30 April 2020, 12:54