Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia watu wa Mungu Ujumbe wa: Imani, Matumaini na Mapendo wakati huu wa Maadhimisho ya Juma Kuu, 2020. Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia watu wa Mungu Ujumbe wa: Imani, Matumaini na Mapendo wakati huu wa Maadhimisho ya Juma Kuu, 2020. 

Ujumbe wa Papa Francisko Maadhimisho ya Juma Kuu 2020!

Maadhimisho ya Juma Kuu kwa Mwaka 2020 ni ya pekee sana, yanaonesha ufunuo na muhtasari wa Injili, yaani upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Katika hali ya ukimya, Injili ya Pasaka ya Bwana, itatangazwa kwa kishindo! Kristo Yesu alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumapili ya Matawi, tarehe 5 Aprili 2020 ni mwanzo wa maadhimisho ya Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Jumapili ya Matawi, Kanisa linaadhimisha Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwengu katika ngazi ya kijimbo. Alhamisi kuu, Kanisa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Ijumaa kuu, Mama Kanisa anakumbuka mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Jumamosi kuu, Kanisa katika majonzi makubwa, linasubiria ushindi wa Kristo Mfufuka!

Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa Juma kuu, Ijumaa tarehe 3 Aprili 2020 amewatumia watu wa Mungu ndani na nje ya Italia, ujumbe wa imani, matumaini na mapendo kwa watu wote wanaoteseka kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hiki ni kipindi cha mateso na mahangaiko makubwa kwa familia nyingi duniani zinazopaswa kujifungia ndani kama sehemu ya mchakato wa kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Watoto wengi hawawezi kutoka na kwenda kuhudhuria masomo shuleni au kuishi kadiri walivyozoea. Baba Mtakatifu anawakumbuka kwa namna ya pekee, wanafamilia ambao wana wagonjwa au wale ambao tayari wameguswa na kutikiswa na ugonjwa Virusi vya Corona au magonjwa mengine. Anayaelekeza mawazo yake kwa watu pweke ambao wanapambana na hali ngumu katika maisha yao, katika muktadha huu, waathirika wakubwa ni wazee. Kwa namna ya pekee kabisa anawakumbuka na kuwaombea wagonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 bila kuwasahau wale wote waliolazwa hospitalini.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza madaktari, wauguzi na kada ya watumishi wa sekta ya afya wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwatibu na kuwaganga wagonjwa pamoja na wale wote wanaoendelea kutoa huduma muhimu za kijamii. Hawa ndio mashujaa wa muda na nyakati zote. Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea wale wote ambao kwa sasa wanakabiliwa na ukata, hali ngumu ya maisha pamoja na hofu ya kukosa ajira kwa siku za usoni. Anawakumbuka wafungwa na mahabusu, ambao hata wao kwa sasa wanatishiwa na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa ajili yao binafsi au wapendwa katika familia zao. Anawakumbuka watu wasiokuwa na makazi ambamo wanaweza kujipatia ulinzi na hifadhi. Hiki ni kipindi kigumu sana katika maisha ya watu wote

Baba Mtakatifu anatambua ugumu na uchungu unaowaandama watu wa Mungu kwa wakati huu. Kwa maneno na ujumbe huu, anapenda kuwahakikishia watu wote upendo na uwepo wake wa karibu. Anawaalika watu kutumia vyema kipindi hiki kwa kujenga na kudumisha ukarimu; kwa kuwasaidia majirani kwa njia mbali mbali za mawasiliano na mitandao ya kijamii. Uwe ni muda wa sala kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale walioguswa na kutikiswa sana ndani na nje ya Italia. Hata kama ikiwa watu wanaendelea bado kuishi wakiwa wamewekwa chini ya karantini, lakini mawazo na roho ya upendo “inaweza kuchanja mbuga” na kuwafikia watu walioko mbali! Hiki ndicho kipaji cha ubunifu wa upendo kinachohitajika kwa wakati huu.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, Maadhimisho ya Juma Kuu kwa Mwaka 2020 ni ya pekee sana, yanaonesha ufunuo na muhtasari wa Injili, yaani upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Katika hali ya ukimya, Injili ya Pasaka ya Bwana, itatangazwa kwa kishindo. Mtakatifu Paulo, Mtume anasema kwamba, Kristo Yesu alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao. (Rej. 2 Kor. 5:15). Kwa njia ya Kristo Mfufuka, maisha yameyashinda mauti. Imani hii ya Kipasaka inarutubisha matumaini ya nyakati bora zaidi; kwa kukombolewa kutoka katika dhambi na janga hili la Virusi vya Corona. Haya ni matumaini ambayo kamwe hayawezi kudanganya.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga mtandao wa mshikamano unaokita mizizi yake katika upendo na uvumilivu ili kujiandaa vyema kwa ajili ya wakati mzuri zaidi ujao. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawashukuru wote waliomruhusu kuingia nyumbani mwao, ili kuwafariji wale wote wanaoteseka, watoto pamoja na wazee wenzake! Baba Mtakatifu anawaomba wote kufikisha ujumbe wake kwao kwamba, yuko karibu nao na anawaombea, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwaokoa watu wake, mapema iwezekanavyo!

Papa: Ujumbe wa Juma Kuu

 

04 April 2020, 14:18