Tafuta

Tafakari ya Njia ya Msalaba kwa Ajili ya Ijumaa Kuu kwa mwaka 2020 imeandaliwa na wafungwa wanaotumikia adhabu zao megerezani. Tafakari ya Njia ya Msalaba kwa Ajili ya Ijumaa Kuu kwa mwaka 2020 imeandaliwa na wafungwa wanaotumikia adhabu zao megerezani. 

Papa Francisko: Tafakari ya Njia ya Msalaba: Ijumaa Kuu 2020!

Tafakari ya Njia ya Msalaba, Ijumaa Kuu 2020 ni kielelezo cha sauti ya watu wasiokuwa na sauti, kielezo cha mapambano kati ya kifo na uhai. Katika hali na mazingira haya, Njia ya Msalaba, Via Crucis, inageuka kuwa ni Njia ya Mwanga, Via Lucis. Kwa mara ya kwanza katika historia, sauti ya wafungwa wasiokuwa na majina inasikika na kuingia katika maskani ya watu sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso, mahangaiko na matumaini ya wafungwa sehemu mbali mbali za dunia, ameamua kwa dhati kwamba, tafakari ya Ijumaa Kuu, Njia ya Msalaba kwa Mwaka 2020, iandaliwe na wafungwa wanaotumikia adhabu yao kutoka katika magereza mawili yaliyoko mjini Padua, Kaskazini mwa Italia. Baba Mtakatifu ameyasema haya katika barua aliyomwandikia Bwana Paolo Possamai, Mkurugenzi mkuu wa Gazeti la “Mattino di Padova”. Baba Mtakatifu anasema, lengo la Kanisa ni kutoa sauti kwa watu wasiokuwa na sauti, ili hata wao waweze kusikika. Tafakari hii imehaririwa na Padre Marco Pozza na inawashirikisha kwanza kabisa: wafungwa wenyewe; askari magereza, watu wa kujitolea, familia za wafungwa, mahakimu, wanasaikolojia wanaotoa ushauri kwa wafungwa, Kanisa, pamoja na raia wasiokuwa na hatia ambao wakati mwingine “wanabambikiziwa kesi” na matokeo yake ni kuishia magerezani.

Gereza ni mahali ambapo mtu anaonja unyonge na udhaifu wake wa kibinadamu kwa kunyimwa uhuru. Lakini, hii pia ni fursa ya kuweza kutubu na kumwongokea Mungu, ili baada ya Ijumaa kuu, aweze kufufuka tena. Baba Mtakatifu anasema, wokovu wa binadamu ni kazi ya umoja na mshikamano inayotekelezwa na Jumuiya ya waamini, kielelezo cha mshikamano wa upendo unaomwilishwa katika haki na huruma. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa tafakari ya Ijumaa kuu imetungwa na wafungwa gerezani. Kutokana na kipeo cha maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 maadhimisho ya Njia ya Msalaba Ijumaa kuu, yatafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican badala ya kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma kama ilivyokuwa kawaida. Ibada ya Njia ya Msalaba itaanza 3:00 Usiku kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 4:00 kwa Saa za Afrika Mashariki.

Tafakari hii ina Vituo 14 vya Njia ya Msalaba kadiri ya Mapokeo ya Kanisa. Hii ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti, kielezo cha mapambano kati ya kifo na uhai. Ni wakati wa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake kwani hakuna linaloweza kushindikana mbele ya Mungu, kwani wokovu ni zawadi inayotolewa bure na Mwenyezi Mungu. Katika hali na mazingira haya, Njia ya Msalaba, Via Crucis, inageuka kuwa ni Njia ya Mwanga, Via Lucis. Kwa mara ya kwanza katika historia, sauti ya wafungwa wasiokuwa na majina inasikika na kuingia katika maskani ya watu sehemu mbali mbali za dunia!

Kituo cha kwanza, Yesu anahukumiwa afe! Tafakari ya kituo hiki imeandikwa na mfungwa ambaye amehukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani pamoja na baba yake mzazi. Anakumbuka jinsi ambavyo ujinga tangu utotoni mwake ulivyomtumbukiza katika matendo ya kihuni na hatimaye, akaishia kuwa ni jambazi wa kutupwa. Akiwa gerezani kwa muda wa miaka 29 amebahatika kusoma tena historia ya maisha yake katika mwanga wa Injili, kiasi cha kujisikia kuwa kama Mtakatifu Petro aliyemkana Yesu mara tatu; Yuda Iskariote aliyemsaliti na Baraba aliyepaswa kuhukumiwa kifo, lakini akaachiwa huru na Yesu akateswa na kufa Msalabani. Anasikitika kusema kwamba, baba yake alifia kwenye gereza lenye ulinzi mkali katika hali ya mateso na mahangiko makubwa. Yote haya anayapokea kwa moyo wa toba kwa kutambua kwamba, gerezani amekutana na Kristo Yesu aliyempatia mwelekeo mpya wa maisha. Kumbe, kwa njia ya: huruma, upendo, msamaha na upatanisho wa kweli, Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake maisha mapya na hivyo wanageuka kuwa ni mahekalu ya Roho Mtakatifu.

Kituo cha Pili: Yesu anapokea Msalaba. Tafakari ya Kituo hiki imeandaliwa na wazazi wawili ambao walimuua mtoto wao mpendwa bila hata chembe ya huruma, mmoja kati ya watoto wao wawili akapona kwa muujiza, lakini hata yeye alikuwa afuate mkumbo wa ndugu yake. Maisha katika familia hii, yalikita mizizi yake katika tunu msingi za kifamilia, kazi pamoja na kuwafundisha watoto wao umuhimu wa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao. Tangu walipomuua mtoto wao, hawakuweza tena kupata amani na utulivu wa ndani na kwa sasa wamejiachilia mikononi mwa Serikali ili haki iweze kutendeka. Msalaba wa mauaji ya mtoto wao bado unawaelemea kwani kwa sasa ni wazee, hawana mtu wa kuliwalinda na wanasongwa sana na mateso. Lakini, hata katika mazingira haya ya kukatisha tamaa, Kristo Yesu, amekuwa daima ni faraja katika mateso na mahangaiko yao; amewasaidia kuwa ni chemchemi ya huruma na ukarimu na kwamba, hawataki tena kujisalimisha chini ya ubaya na mateso, kwani wameonja huruma na upendo wa Mungu ambayo umepyaisha tena maisha yao na wameendelea kupata faraja kutoka kwa Kristo Yesu. Kimsingi wanasema, Msalaba wa ukombozi uwe ni chemchemi ya maisha mapya!

Kituo cha Tatu: Yesu anaanguka mara ya kwanza: Tafakari hii imeandikwa na mfungwa mmoja ambaye alishiriki mauaji ya mtu asiyekuwa na hatia! Tangu wakati huo, anaendelea kusikia ndani mwake, ile sauti ya yule mnyang’anyi ikisema, “Ee Yesu nikumbuke utakapoingia katika Ufalme wako”. Tangu mwanzo wa utoto wake, anasema, amekulia katika mazingira hatarishi, akataka kuvuta hisia za watu kumtambua na kumheshimu na wale wote walioshindwa kufanya hivi, aliwaonjesha cha mtema kuni! Ubaya wa moyo ulizidi kuongezeka ndani mwake na siku moja akajikuta anatumbukia na kuzama katika giza nene na kusababisha mauaji. Familia yake ikajikuta ikiogelea katika matatizo mbali mbali kwa kukosa utambulisho halisi na heshima kiasi cha kugeuka kuwa ni familia ya muuaji! Anasikitika sana kwa yale yaliyotendeka, lakini gerezani amekutana na Wasamaria wema waliomsaidia tena kupata mwanga mpya wa matumaini ya maisha. Anamwomba Mwenyezi Mungu awakirimie waamini ujasiri wa kuona dhambi, udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani!

Kituo cha Nne: Yesu anakutana na Mama yake: Tafakari hii imeandaliwa na Mama ya mfungwa mmoja, ambaye hata baada ya mtoto wake kuhukumiwa na kufungwa gerezani, ameendelea kumwonesha huruma na upendo wake wa kimama! Tangu siku ile, ni kana kwamba, familia nzima imehukumiwa na kuingia gerezani, kiasi kwamba, bado anaendelea kuteseka kutokana na makosa yaliyotendwa na mtoto wake. Anasema, ni mwanamke ambaye amejifunza kusimama imara katika imani bila kukata tamaa. Amemweka mwanaye mpendwa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, aliyevumilia: mateso na hata kifo cha mwanae mpendwa Kristo Yesu. Hata katika Njia ya Msalaba, aliendelea kumsindikiza katika hali ya ukimya, lakini akafanikiwa kuonana mubashara na Uso wa huruma na upendo wa Mwanae mpendwa, ili kumhakikishia kwamba, hata katika mateso, bado anaendelea kumsindikiza! Mama huyu anasema, ataendelea kumsindikiza mtoto wake aliyefungwa gerezani, kwani uchungu wa mwana aujuaye ni mama! Mama huyu ameomba msamaha kwa ajili ya mtoto wake, ametambua pia udhaifu wake katika malezi na makuzi ya kijana wake. Kwa sasa anamwomba Mwenyezi Mungu amkirimie huruma mwanaye mpendwa, ili baada ya kumaliza adhabu yake kifungoni, aweze kuwa mtu mpya, anayeweza kupenda na kupendwa. Mama huyu anamwomba Bikira Maria, kusikiliza na kujibu kilio cha wale wote wanaoteseka, wakisubiri faraja na machozi yao kupanguswa!

Kituo cha Tano: Simoni wa Kirene anamsaidia Yesu kubeba Msalaba. Tafakari hii imeandaliwa na mfungwa mmoja aliyejivunia kazi yake, lakini akashtakiwa kwa makosa ya uwongo! Akatumbukizwa gerezani na gereza likaingia katika maisha yake. Giza kubwa likayafunika macho yake na hivyo kushindwa kuona maana ya huduma aliyokuwa anatoa kwa watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Akiwa gerezani amekutana na akina Simoni wa Kirene. Hawa ni watu wanaojitolea; watu wanaosikiliza mateso na mahangaiko ya jirani zao, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Akiwa gerezani alionja pia ukarimu kutoka kwa mfungwa mwenzake, ukarimu ambayo ulimfanya mke wake mpenzi kutokwa na machozi ya shukrani! Kwa bahati mbaya mfungwa huyu anasema, anaendelea kuzeekea gerezani, lakini anatamani kuona siku moja akiwa huru ili hata yeye pia aweze kuwa ni Simoni wa Kirene, kwa wale wanaoteseka na kusumbuka. Anamwomba Mwenyezi Mungu awajalie waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu na udugu wa kibinadamu.

Kituo cha Sita: Veronika anaupangusa Uso wa Yesu! Hii ni tafakari ya katekista kutoka Parokia moja anayesadaka maisha yake kwa ajili ya kutoa katekesi. Katika maisha yake, amekutana na watu ambao wamekata tamaa; watu wanaoelemewa na magumu ya maisha; waliotumbukia na kuzama katika upweke hasi kwa kutoeleweka vyema. Katekista huyu anatamani kuendelea kuwapangusa watu machozi, wale wote wanaoelemewa na matatizo bila ya kuogopa kuwaendea. Anatamani kuwasindikiza katika hali ya ukimya, kwa kuwasikiliza bila kuwa na maamuzi mbele wala kuwahukumu. Kwa sababu hata Kristo Yesu katika hali yake ya ukimya anawangalia waja wake kwa jicho la huruma na upendo. Anatambua udhaifu na mapungufu ya waja wake. Kuna haja hata kwa wafungwa kupewa fursa nyingine, ili waweze kuwa kweli ni watu wapya, kwa kuonja huruma na upendo kutoka kwa jirani zao. Watu wa Mungu wawe na ujasiri kama ule wa Veronika wa kuweza kuwapangusa machozi maskini na wale wanaoteseka kwa kutambua kwamba, wote hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kituo cha Saba: Yesu Anaanguka Mara ya Pili! Tafakari hii imeandikwa na mfungwa ambaye katika maisha yake, hakuwaza hata mara moja kwamba, iko siku hata yeye ataingia gerezani. Kwake gereza lilikuwa kama makaburi ya watu hai, lakini siku moja, yeye pamoja na ndugu yake, wakajikuta wanaingia “lupango”. Kufumba na kufumbua, baba na mama yake nao wakapigwa pingu na kutupwa gerezani! Tangu wakati huo, gereza likawa ni nyumbani kwao! Wazazi wake wanaendelea kuzeekea gerezani kutokana na makosa aliyotenda. Alikuwa ni mfanyabiashara wa dawa za kulevya, kazi ambayo alishirikiana kwa karibu sana na baba yake mzazi. Mara ya pili, alianguka alipogundua kwamba, ni kwa sababu ya makosa yake, Kristo Yesu amateseka na hata kufa Msalabani! Sasa anamwomba msamaha kwa sababu alitenda yote haya bila kujua, lakini sasa anatambua ubaya wa dhambi zake na anaomba huruma, msamaha na msaada wa Mungu, ili kuanza kujenga upya kuta za maisha yake. Anaona analo deni kubwa mbele ya wazazi wake lakini hata yeye mwenyewe maisha yake yamekuwa kama Njia ya Msalaba! Anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia waamini nguvu na uwezo wa kumkimbia Shetani, Ibilisi, ili asiwabwage na kuwagalagaza katika vishawishi na dhambi!

Kituo cha Nane: Akina Mama wa Yerusalemu Wanamlilia Yesu. Sehemu hii ya tafakari imeandaliwa na mtoto wa kike wa mfungwa anayetumikia kifungo cha maisha gerezani. Anatambua na kukiri kwamba, kwa hakika amekuwa ni sababu ya mateso na mahangaiko ya baba yake mzazi ambaye  kwa muda wa miaka 28 anaendelea kutumikia adhabu yake gerezani. Miaka yote hii imemjaza mwanamke huyu moyoni mwake: chuki, hasira na jazba. Amezunguka kutoka Kusini hadi Kaskazini mwa Italia ili aweze kuwa karibu zaidi na baba yake mzazi. Anatambua miji mbali mbali ya Italia si kwa uzuri wake, bali kwa magereza aliyoyatembelea, akimtafuta baba yake mzazi. Miaka kadhaa iliyopita, anasema, amepoteza fadhila ya upendo kwa sababu anajiona kuwa ni mtoto wa mfungwa gerezani na mama yake ametumbukia katika ugonjwa wa sonona na kwa hakika familia nzima imeanguka! Dada huyu anasema, amebaki peke yake na fedha kidogo kwa ajili ya kutegemeza uzito wa familia nzima! Amekuwa kwa haraka kutoka katika hali ya utoto na kujikuta amekomaa ili kuwajibika katika familia. Nyumba yao kwa sasa imekuwa ni Njia ya Msalaba na baba yake mzazi ni kati ya watu wale waliohukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha. Akafunga ndoa, bila ya uwepo wa baba yake mzazi. Kuna wazazi ambao wanawapatia watoto wao fursa ya kukua na kukomaa, lakini kwa upande wake, inampasa kumsubiri baba yake mzazi na kwamba, hii ndiyo chemchemi ya matumaini kwake! Dada huyu anawaalika waamini kutubu na kumwongokea Mungu. Anawakumbuka na kuwaombea wale wote wanaoteseka kutokana na  aibu na machungu ya moyo ili waweze kuwa na matumaini!

Kituo cha Tisa: Yesu Anaanguka Mara Tatu: Tafakari hii imetungwa na mfungwa mmoja wa kike anayekiri kwamba, kuteleza na kuanguka si jambo linalofurahisha sana, lakini kuanguka mara kadhaa, ni jambo linalofedhehesha sana. Katika maisha yake, ameteleza na kuanguka! Kuna wakati aliweza kusimama na kusonga mbele. Tangu akiwa mdogo ameonja maisha ya gereza kwa kujifungia ndani, kwa kuogopa hasira ya watu wazima walioshindwa kuwaheshimu na kuwathamini watoto. Mimba ya mtoto wake ilitoka na kwa sasa umri umekwenda na anaendelea kuzeeka. Akiwa gerezani ameonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake; upweke hasi ukageuka kuwa ni chemchemi ya maisha mapya. Kwa sasa anaweza kuandika ukurasa mpya wa maisha yake na kuyapatia maana halisi! Anawaombea wale wote walioteleza na kuanguka, kusimama tena kwa ujasiri na kusonga mbele, huku wakisaidiwa na jirani zao.

Kituo cha Kumi: Yesu Anavuliwa Nguo! Tafakari ya kituo hiki imeandaliwa na mwanamke anaye waelimisha wafungwa gerezani! Wafungwa ni watu ambao uhuru wao umebinywa sana kiasi cha kuvuliwa utu na heshima yao kama binadamu. Uhuru wa wafungwa unaendelea kupungua kila kukicha! Hawa ni watu dhaifu na wakati mwingine, hawana hata mambo msingi katika maisha kama sehemu ya adhabu ya makosa waliyotenda! Kuna baadhi ya watu ambao wana matumaini ya kupyaisha maisha yao, ikiwa kama watapewa nafasi. Shida na mahangaiko ya wafungwa hawa anasema, mwanamke huyu, wakati mwingine zinamzidia. Uamuzi wa kufanya kazi hii ni kutokana na uchungu aliokumbana nao katika maisha, baada ya mama yake kugongwa na kufariki dunia na gari iliyokuwa inaendeshwa na mfanyabiashara wa dawa za kulevya. Kwa ujasiri mkubwa akaamua kulipa ubaya kwa kutenda wema. Hata kama anaipenda kazi hii kwa moyo wake wote, lakini wakati mwingine anakosa nguvu na ari ya kusonga mbele. Katika hali na mazingira kama haya, kuna haja ya watu kama hawa kusindikizwa katika maisha na utume wao. Mwanamke huyu anamwomba Mwenyezi Mungu awakirimie waamini moyo wa huruma na uvumilivu; waweze kuishi katika ukweli na hivyo kuondokana na unafiki.

Kituo cha Kumi na Moja: Yesu Anasulubishwa Msalabani. Padre aliyeandaa tafakari hii anasema, mara nyingi ametafakari sana kuhusu sehemu hii ya Injili, lakini siku moja, Msalaba huu uliingia katika maisha yake, kwani alishutumiwa kwa maneno makali kama msumari wa moto uliokuwa unaingia mwilini wake na kuanza kuona giza nene mbele yake. Kama Padre akaona jina lake limetundikwa kwenye ubao wa matangazo ya Mahakama na kutambua kwamba, alipaswa sasa kusimama kidete ili kujitetea na hatimaye, kuonesha kwamba, hakua na hatia hata kidogo. Aliendelea kutundikwa Msalabani kwa muda wa miaka 10. Hii ikawa ni Njia yake ya Msalaba, kwa kushutumiwa, kuonewa mashaka na wakati mwingine kuonja hasira za watu. Akawaza moyoni mwake na kutaka “kupotezea hali hii” lakini akaamua kubaki amesimama kama Padre bila kupepesa pepesa macho! Akahukumiwa bila hatia. Daima katika Njia ya Msalaba alikutana na wanafunzi wake pamoja na familia zao. Hawa ni watu ambao wamepangusa uso wake, bila kuwasahau wale waliomsindikiza kwa sala na sadaka zao. Alipokata rufaa na kushinda, akatambua kwamba, kwa hakika alikuwa ni mtu mwenye furaha kubwa kuliko hata kipindi cha miaka 10 iliyopita wakati akiwa kwenye Njia ya Msalaba. Kwa hakika anasema, amegusa huruma ya Mungu katika maisha yake. Msalaba wa Upadre wake, ukang’arishwa zaidi! Padre huyu anawaombea wale wote wanaoendelea kuweka matumaini yao kwa Kristo Yesu, mpaka dakika ya mwisho, ili kupokea ahadi yake, “Amini, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi” Lk. 23: 43.

Kituo cha Kumi na Mbili: Yesu Anakufa Msalabani. Sehemu hii ya tafakari imeandaliwa na Hakimu anayesema kwamba, kazi yake haimruhusu kumhukumu mtu mara mbili kwani kwa kufanya hivyo ni kumwongozea mtu maumivu ya kiroho na kimaadili. Haki inafumbatwa katika huruma; kwa kuwasaidia wengine kusimama na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu; kwa kukazia tunu msingi katika maisha ya binadamu; mambo ambayo kamwe hayawezi kufutika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Wafungwa wajitahidi kuona uzuri kutoka kwa jirani zao, ili kupyaisha tena maisha yao. Wafungwa wawe na ujasiri wa kuandika upya historia yao kama mtu binafsi na kama kundi la watu, daima wakikuza na kudumisha Injili ya matumaini katika maisha yao. Wafungwa watambue udhaifu wao na makosa waliyotenda. Watubu na kumwongokea Mungu, tayari kuanza kuandika kurasa mpya wanapotoka gerezani, kwa sababu hata wafungwa wanaendelea kubaki kuwa ni watoto wa familia kubwa ya binadamu.

Kituo cha Kumi na Tatu: Yesu Anashushwa Msalabani: Tafakari hii imeandaliwa na Mtawa wa kiume anayefanya shughuli za kujitolea gerezani. Anakiri kwamba, wafungwa wamekuwa ni walimu wake wazuri katika hija ya maisha yake. Hawa ni watu ambao wamekuwa ni chemchemi ya baraka kwani anatambua kwamba, gereza halichagui mtu kamwe, kwani wakati wowote unaweza kujisikia “umeswekwa ndani”. Kumbe, hakuna sababu ya kuwahukumu na kuwashutumu wafungwa magerezani. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliamua kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Katika hija ya maisha yao, akawaonjesha: huruma na upendo wake wa daima; akawaonesha uwepo wake mwanana na kuwafariji katika maisha yao. Huu ni mwaliko wa kujenga utamaduni wa kuwatembelea wafungwa, ili kuwasikiliza na kuwafariji. Analiombea Kanisa ili liendelee kuwa ni Sakramenti ya Wokovu; kwa kushuhudia na kuwatangazia watu Injili ya furaha na matumaini.

Kituo cha Kumi na Nne! Yesu anazikwa Kaburini! Askari magereza katika kituo hiki anaandika kwamba, kila siku ya maisha yake, anagusa mateso na mahangaiko ya wafungwa gerezani! Katika hali na mazingira kama haya, kuna tabia ya watu kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zao, hali ambayo inagumisha zaidi maisha ya wafungwa gerezani. Gerezani ni mahali pa ajabu sana, kwani panaweza kumgeuza mtu mwema kuwa katili sana; na mtu mbaya, kutubu na kumwongokea Mungu na hivyo kuwa ni mtu mwema na mfano bora wa kuigwa. Yote haya yanategemea mambo mbali mbali katika maisha ya wafungwa gerezani. Gereza linapaswa kuwa ni mahali pa kumpatia mtu nafasi ya kuweza kuandika tena ukurasa mpya wa maisha yake baada ya kuanguka katika makosa. Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa uzito wa pekee. Gerezani humo, amekuwa akitekeleza dhamana na wajibu wake kama Shemasi wa kudumu. Amekuwa ni faraja kwa wale wanaoteseka; chemchemi ya matumaini kwa wafungwa waliokata tamaa na kuelemewa na woga. Mbele ya Mwenyezi Mungu, dhambi zote zinapata msamaha na maondoleo yake. Askari magereza anawaombea waamini ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na matumaini kwa jirani zao, lakini zaidi kwa wafungwa magerezani!

Njia ya Msalaba: Ijumaa Kuu 2020
07 April 2020, 13:17