Tafuta

Papa Francisko anasema, Sanda Takatifu ni ushuhuda wa mateso na upendo wa Kristo Yesu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba! Papa Francisko anasema, Sanda Takatifu ni ushuhuda wa mateso na upendo wa Kristo Yesu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba! 

Papa: Onesho la Sanda Takatifu: Mateso na Upendo wa Kristo!

Sura iliyoko kwenye Sanda Takatifu ni kielelezo na ufunuo wa sura za wagonjwa, watu pweke, maskini wasiokuwa na uwezo wa kupata tiba muafaka. Hii ni sura ya watu wanaoteseka kutokana na vita pamoja na ghasia sehemu mbali mbali za dunia. Ni watu wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na viungo vyake, utumwa mamboleo; nyanyaso na dhuluma mbali mbali. Ni mateso!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Sanda Takatifu inayohifadhiwa Jimbo Kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia ni Kisakramenti kinachowasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuona sura ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wakfu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Sanda Takatifu ni kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani kwa waja wake na kwa njia hii, waamini pia wanaweza kuona sura ya ndugu zao wanaoteseka: kiroho na kimwili sehemu mbali mbali za dunia! Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino na Susa, Jumamosi kuu, tarehe 11 Aprili 2020, kuanzia majira ya Saa 11: 00 jioni kwa Saa za Ulaya atafanya Ibada ya Uonesho wa Sanda Takatifu kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii.

Hii ni fursa ya kutafakari huruma na upendo wa Kristo Yesu unaobubujika kutoka katika ukuu, utukufu sanjari na nguvu ya upendo wa Mungu unaofumbatwa kwenye Fumbo la Msalaba. Katika shida na mahangaiko ya binadamu kwa wakati huu kutokana na majanga mbali mbali yanayomwandama, Mama Kanisa anawaalika watoto wake kuwa na imani, matumaini na mapendo thabiti, kwani nguvu ya Kristo Mfufuka imeshinda dhambi na mauti! Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia barua Askofu mkuu Cesare Nosiglia akimwelezea nia yake ya kujiunga nao kwa njia ya vyombo vya mawasiliano kama jibu makini kwa kilio kinachotolewa na watu wa Mungu kwa wakati huu wa janga kubwa la maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Sanda Takatifu ni ufunuo wa Mtumishi wa Bwana aliyedharauliwa na kukataliwa na watu, mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko! Hakika ameyachukua masikitiko ya mwanadamu, akajitwika huzuni yake, akadhaniwa kuwa amepigwa, tena amepigwa na Mungu na kuteswa! Alichubuliwa na kuteswa kwa maovu ya binadamu. Adhabu ya amani ya binadamu ilikuwa juu yake na kwa kupigwa kwake, binadamu amepona! Rej. Isa. 53: 3. 4-5. Baba Mtakatifu anakaza kusema, sura iliyoko kwenye Sanda Takatifu ni kielelezo na ufunuo wa sura za wagonjwa na watu wanaoishi katika upweke; wagonjwa ambao hawana uwezo wa kupatiwa tiba muafaka kutokana na maradhi yanayowasibu.

Hii ni sura ya watu wanaoteseka kutokana na vita pamoja na ghasia sehemu mbali mbali za dunia; watu wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na viungo vyake, utumwa mamboleo; nyanyaso na dhuluma mbali mbali. Kama Wakristo katika mwanga wa Maandiko Matakatifu, wanatafakari Sura ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wakristo wana imani na matumaini kwa Kristo Yesu kwa sababu daima anasikiliza sauti na kilio cha waja wake wanaomlilia usiku na mchana naye anawaokoa! Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema watakaoshiriki katika Ibada hii kwa sala na tafakari, wajiunge na mateso ya Kristo, ili hatimaye, waweze kuonja neema na baraka ya ufufuko na uzima wa milele. Mwishoni, mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko ametoa baraka zake za kitume kwa washiriki wote!

Papa: sanda Takatifu
10 April 2020, 17:18