Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Papa Francisko: Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu!  (Vatican Media)

Madonda Matakatifu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu

Huruma ya Mungu inabubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Kristo Mfufuka. Huruma hii inabubujika na kupitia kwenye Madonda yake Matakatifu, ili kuwakirimia waja wake msamaha na faraja. Fadhila ya huruma ya Kikristo isaidie kujenga na kudumisha mshikamano kati ya Mataifa na taasisi mbali mbali, ili kupambana na Virusi vya Corona, COVID-19 kwa njia ya mshikamano wa Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la “Santo Spirito in Sassia” mjini Roma, ambalo kwa sasa limegeuka kuwa ni Madhabahu ya Huruma ya Mungu, Jimbo kuu la Roma, Jumapili tarehe 19 Aprili 2020, amewaongoza waamini katika Sala ya Malkia wa Mbingu. Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu katika maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu kama alivyotamani Mtakatifu Yohane Paulo II. Majibu ya waamini katika dhoruba za maisha na historia ya mwanadamu ni huruma ya Mungu. Huu ni upendo wenye huruma unaonafishwa miongoni mwa watu wote, lakini zaidi kati ya maskini, wanaoteseka na wale wanaotelekezwa. Huruma na upendo wa Mungu upate chimbuko lake kutoka katika sakafu ya nyoyo za watu na wala si jambo la ibada, wala mtu kujisikia. Huruma ya Mungu inabubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Kristo Mfufuka.

Huruma hii inabubujika na kupitia kwenye Madonda yake Matakatifu, ili kuwakirimia waja wake msamaha na faraja. Fadhila ya huruma ya Kikristo isaidie kujenga na kudumisha mshikamano kati ya Mataifa na taasisi mbali mbali, ili kupambana na janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kwa njia ya mshikamano wa Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kuwatakia heri na baraka waamini wa Makanisa ya Mashariki wanaoadhimisha Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2020. Ujumbe kwa watu wote wa Mungu ni kwamba, “Bwana amefufuka kweli kweli”. Katika kipindi hiki cha mateso na majaribu makubwa katika maisha ya mwanadamu, ujumbe wa matumaini unabubujika kwa wale wote waliokufa na kufufuka na Kristo Yesu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Wakristo wa Makanisa ya Mashariki wanaoadhimisha Pasaka ya Bwana pamoja na waamini wa Kanisa la Kiorthodox. Hiki ni kielelezo cha umoja na udugu hasa katika maeneo ambayo Wakristo ni kundi dogo, ikilinganishwa na idadi ya watu katika maeneo hayo!

Papa: Madhabahu
20 April 2020, 14:26