Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa ambalo ni Sakramenti ya Wokovu wa watu, linapaswa kuwa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wanaoteseka duniani! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa ambalo ni Sakramenti ya Wokovu wa watu, linapaswa kuwa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wanaoteseka duniani! 

Papa Francisko: Mama Kanisa na changamoto za Virusi vya Corona!

Hiki ni kipindi ambacho Mama Kanisa anapaswa kukitumia vyema kwa kujikita katika utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ubunifu mkubwa! Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya binadamu pamoja na Mtunza Sadaka ya Kipapa, watakuwa na majukumu makubwa katika kipindi cha awamu ya pili, baada ya janga la Virusi vya Corona, COVID-19 kupita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Wafanyakazi wa Vatican wameendelea kutekeleza dhamana na utume wao kwa kutumia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia inayowawezesha baadhi yao kufanya kazi wakiwa majumbani mwao bila ya kuwa na ulazima wa kwenda mjini Vatican. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuendelea na shughuli zake kwa kuzingatia itifaki ya kinga dhidi ya mlipuko wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu ameendelea kuongoza Ibada ya Misa Takatifu inayorushwa moja kwa moja kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican na vyombo vya mawasiliano pamoja na mitandao ya jamii. Kimekuwa ni kipindi cha sala, tafakari, toba na wongofu endelevu.

Ni wakati wa kutafakari na kuweka sera na mikakati ya utekelezaji katika maisha na utume wa Kanisa baada ya janga hili la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hiki ni kipindi ambacho Mama Kanisa anapaswa kujipanga vyema, ili kuwasindikiza kwa hali na mali waathirika wote wa Virusi vya Corona. Sera hizi hazina budi kusimikwa katika sala inayonafsishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kuwasaidia na kuwahudumia wagonjwa na wale wote wanaoteseka kwa njaa na upweke. Ni kipindi ambacho Mama Kanisa anapaswa kukitumia vyema kwa kujikita katika utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ubunifu mkubwa! Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya binadamu pamoja na Mtunza Sadaka ya Kipapa, watakuwa na majukumu makubwa katika kipindi cha awamu ya pili, baada ya janga la Virusi vya Corona, COVID-19 kupita!

Hii ni sehemu ya majibu yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Bwana Austen Ivereigh na kuchapishwa kwenye Gazeti la “The Tablet, London, “Commonweal, New York” na “Civiltà Cattolica, Italia”. Katika mahojiano haya, Baba Mtakatifu anapembua kwa kina na mapana kuhusu maisha na utume wa Kanisa katika kipindi hiki cha janga la Virusi vya Corona, COVID-19; Sera na mikakati inayopaswa kutekelezwa na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa ili kulinda uhai, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Janga hili ni changamoto kwa watu wa Mungu kuangalia tena mtindo wa maisha, vipaumbele vyao na kujikita katika wongofu wa kiekolojia, ili kukuza uchumi shirikishi unaokidhi mahitaji msingi ya binadamu! Huu ni muda muafaka kwa Mama Kanisa kujikita katika wongofu wa kimisionari na kuendeleza dhamana, maisha na utume wa Kanisa unaokita mizizi yake katika familia Kanisa dogo la nyumbani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa lina ujumbe wa imani, matumaini na mapendo kwa waathirika wote wa ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19! Kunako mwaka 1630, Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia lilikumbwa na maambukizi ya ugonjwa Tauni na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu wa Mungu! Kanisa likajipambanua kuwa ni Sakramenti ya wokovu kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya faraja, imani na matumaini kwa watu waliopondeka na kuvunjika moyo. Ili kuweza kukabiliana na changamoto za maambukizi makubwa ya magonjwa yanayosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, kuna haja kwa viongozi wa Kanisa kuwa karibu zaidi na watu wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Kardinali Federico Borromeo wa Jimbo kuu la Milano wakati wa maambukizi makubwa ya ugonjwa wa Tauni kunako mwaka 1630. Ni muda muafaka wa kusali na kumwilisha sala hii katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni muda wa kuweka sera na mikakati ya shughuli za kichungaji ili kupambana na madhara yaliyojitokeza kutokana na maambukizi ya magonjwa haya. Kanisa liwahudumie watu wanaoteseka na kujipanga zaidi, ili kusaidia maboresho ya kesho yenye matumaini na iliyo bora zaidi. Huu si wakati wa kuwageuzia watu kisogo, bali kushikamana nao kwa hali na mali, kama kielelezo cha ushuhuda wa Kanisa linalojali na kuwasumbukia watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza baadhi ya viongozi wa Serikali na Jumuiya ya Kimataifa waliochukua hatua muhimu za kulinda maisha ya watu wao. Watu wapende, wasipende, lakini sera na itifaki nyingi zimekita mizizi yake katika masuala ya kiuchumi na hivyo kusahau: utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kukumbatia utamaduni wa kifo, sera na mikakati isiyowajali maskini. Katika kipindi hiki cha janga la Virusi vya Corona, COVID-19, wazee wengi wamekumbwa na kifo laini au Eutanasia. Mtakatifu Paulo VI alikuwa na upeo mpana na uwezo wa kuona mbali, akagundua changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa; akabainisha wajibu wa Kanisa kama Mama na Mwalimu na kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo ni kati ya mafundisho mazito ya Mtakatifu Paulo IV. Leo hii kumeibuka utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani.

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa watu wa Mungu kujikita katika mchakato wa wongofu wa kiekolojia kwa kujenga na kudumisha uchumi shirikishi unaokidhi mahitaji msingi ya binadamu. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na wote. Kuna uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea kutendeka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na majanga ya moto! Kuna miamba ya barafu inayoendelea kuyeyuka na hivyo kina cha maji ya bahari kuongezeka maradufu, hali inayotishia usalama wa maisha ya watu na mali zao. Kuna watu wamepigishwa magoti kutokana na mafuriko ambayo yamewatumbukiza katika umaskini mkubwa! Lakini, matukio yote haya yamewekwa pembeni mwa vipaumbele vya Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa, lakini madhara yake ni makubwa anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Tarehe 12 Agosti 2019, Jumuiya ya Kimataifa iliadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa Geneva kunako mwaka 1949. Mkataba huu ni chombo cha sheria kimataifa kinachodhibiti matumizi ya nguvu wakati wa vita, umuhimu wa kuwalinda raia na wafungwa wakati wa vita. Tukio hili lilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa, lakini wakasahau kwamba, miaka 70 iliyopita kuna vijana 10, 000 waliopoteza maisha. Watu wanakumbukwa kwa kuandikwa majina kwenye makaburi na wala hakuna cha ziada! Papa Benedikto XV, wakati huo akasema kwamba: Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia yalikuwa ni maafa “yasiyokuwa na mashiko”. Kuna wanajeshi wengi waliopoteza maisha! Hawa ni watu waliokuwa na familia! Sera za kibaguzi zimeendelea kusababisha maafa na majanga makubwa kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Watu wajenge utamaduni wa kuwa na kumbu kumbu endelevu kuhusu asili, tamaduni, mapokeo na upendo, ili kudumisha pia wongofu wa kumbu kumbu! Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 halichagui wala kubagua, limekuwa ni “kumba kumba kwa watu wote, maskini na matajiri”. Ni unafiki mkubwa kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kufuta baa la njaa duniani, kwa sababu hao wanaoweka sera na mikakati ya kupambana na baa la njaa, ndio wale wale wanaotengeneza silaha za vita! Watu wanapaswa kuonesha kwa vitendo sera na mikakati inayopangwa na Jumuiya ya Kimataifa kwani maneno matupu, kamwe hayawezi kuvunja mfupa! Jumuiya ya Kimataifa ikiangalia kwa mtazamo mpana zaidi inaweza kuona kwamba uzalishaji unohusisha ubunifu na bidhaa za aina mbali mbali na usioleta athari kwenye mazingira waweza kuleta faida kubwa. Jambo la msingi ni kukuza na kudumisha uwazi na ubunifu kwa kuelekeza nguvu hizi kwenye njia mpya. Huu ni wakati muafaka kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika wongofu wa kiekolojia. Matumizi mabaya ya rasilimali na utajiri wa dunia, yatawatumbukiza watu wa Mungu katika majanga na maafa makubwa!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, umefika wakati wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wengi wao hawana makazi ya kudumu na wala si rahisi kuonekana kwa sababu ya aibu! Watu wengi wanawapita bila hata ya kuwaangalia usoni. Mama Theresa wa Calcutta alionesha ujasiri, akasimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na utandawazi usiojali utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kuna haja ya kuibua mbinu mkakati wa kuwasaidia na kuwahudumia maskini na kamwe wasigeuzwe kuwa kama “Mbwa koko” wanaotupiwa mawe kila mara wanapoonekana! Hawa ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wanapaswa kuheshimiwa, kupendwa na kuthaminiwa!

Huruma ni fadhila inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu! Watu wa Mungu waanze kujikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani kwa ajili ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Kuna umati mkubwa wa madaktari, wauguzi, mapadre na watawa wamesadaka na kuyamimina maisha yao kwa ajili ya huduma makini kwa wagonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Ni watu ambao wamefariki dunia, kwa kuhudumia! Toba na wongofu wa ndani ni changamoto na mwaliko katika kipindi hiki cha janga kubwa la Virusi vya Corona. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa katika muundo wake ni la Kierakia ni Mama na Mwalimu. Wakleri wamewekwa wakfu ili kutoa huduma ya kimama katika maisha ya kiroho. Utume huu unajionesha kwa namna ya pekee kwa Maaskofu wanaotakiwa kuiongoza Jumuiya ya Kikristo kama kielelezo hai cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake. Kama ilivyokuwa kwa Mitume ambao Maaskofu ni waandamizi wao, wanaunda urika na Baba Mtakatifu ambaye ni Khalifa wa Mtakatifu Petro. Muundo huu wa Kanisa ni kazi ya Roho Mtakatifu na daima linapaswa kusoma alama za nyakati.

Viongozi wa Kanisa wanayo dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kanisa linapaswa kutoka, kuwaendea na kuwahudumia watu wa Mungu. Ikumbukwe kwamba, Sheria za Kanisa ni kwa ajili ya wokovu wa roho za waamini! Huu ni wakati wa kukuza na kuendeleza dhamana na utume wa familia, Kanisa dogo la nyumbani, ili ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbali mbali za Kikristo, kiutu, kijamii na kitamaduni. Familia inapaswa kuwa ni shuhuda wa matumaini katika kipindi cha shida na mahangaiko makubwa!

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kuna umati mkubwa wa wazee ambao wanaishi katika hali ya upweke na kukata tamaa ya maisha si tu kwa sababu ya maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID, bali tangu mwanzo, kuna baadhi ya watoto, ndugu na jamaa waliwatelekeza wazee kwenye nyumba za kutunza wazee kama “magari mabovu”. Wazee wengi wanafariki dunia kutokana na upweke hasi, umbali pamoja na kutelekezwa na watoto, ndugu na jamaa. Wazee ni kundi linalohitaji kupendwa, kuthaminiwa na kutunzwa. Wazee wamekuwa mstari wa mbele katika dhamana ya kurithisha imani, tamaduni na mapokeo katika Jamii. Wazee ni kundi linaloshuhudia matumaini hata kwa vijana wa kizazi kipya!

Wazee watambue kwamba, wao ni mzizi wa maisha ya jumuiya, kumbe, ni wajibu wao kurithisha uzoefu na kumbu kumbu za maisha. Wazee wawasaidie watoto kung’amua maana ya maisha na tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu na kwamba, uzoefu wao, tayari ni shahada tosha kabisa katika maisha. Wazee na wagonjwa waendelee kusali kwa ajili ya kuliombea Kanisa, watoto na vijana; waendelee kuwa karibu na Kanisa na waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, hadi dakika ya mwisho wa maisha yao! Vijana wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa unyenyekevu na wajitahidi kuzungumza kwa ujasiri kama sehemu ya mchakato wa kujenga na kukuza sanaa na utamaduni wa kusikilizana na kusindikizana katika maisha. Wazee wana ndoto, lakini ni watu ambao kwa sasa wanateseka sana kwa kukosa mambo mengi, lakini wasikate tamaa, bali wachukue ndani mwao mambo msingi kutoka katika mila, desturi na mapokeo na kupanda nayo kwenda mlimani! “Cessi, et sublato montem genitore petivi”.

Papa: Corona

 

09 April 2020, 16:10