Tafuta

Vatican News
Papa Francisko ameadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu George, Mtakatifu somo wake kwa kutoa zawadi ya vifaa tiba nchini Romania, Hispania na Italia dhidi ya COVID-19. Papa Francisko ameadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu George, Mtakatifu somo wake kwa kutoa zawadi ya vifaa tiba nchini Romania, Hispania na Italia dhidi ya COVID-19.  (Vatican Media)

Mtakatifu George, Shahidi, Somo wa Papa Francisko: Umwombee!

Kardinali Krajewski, anasema, maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Gregory, Somo wa Baba Mtakatifu Francisko yamepambwa na zawadi ya vifaa tiba kwa ajili ya waathirika wa ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona nchini Romania, Hispania na Italia. Hiki ni kielelezo cha upendo na mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, Baba wa maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Mama Kanisa tarehe 23 Aprili ya kila mwaka, anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu George sanjari na kumbu kumbu ya Mtakatifu somo wa Papa Jorge Mario Bergoglio, yaani Baba Mtakatifu Francisko. Mtakatifu George anakumbukwa sana kwa kujifunga kibwebwe kupambana na nguvu za giza kwa watu wa nyakati zake, kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyofanya katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni kiongozi anayependa kupandikiza mbegu ya uzuri, wema na utakatifu wa maisha, ili watu wengi waweze kujisikia kuwa kweli ni watoto wanaopendwa na Mungu licha ya udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu! Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wanafarijika wanapokutana na kuzungumza Baba Mtakatifu Francisko kwani watu wengi wanapenda kumwita, “Mtu wa watu, kiongozi wa wanyonge na maskini”.

Ni kiongozi anayependa kushirikisha wengine ile furaha ya Injili kwa watu wanaokabiliana na magumu katika maisha, na kuwatia moyo wale wote wanaoendelea kujisadaka katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili na manyoofu. Ni mtu wa sala na tafakari ya kina; anayetaka kutekeleza dhamana na utume wake, kwa kusoma alama za nyakati. Ni kiongozi anayejitahidi kujenga madaraja ya watu kukutana na kuanzisha mchakato wa umoja, udugu wa kibinadamu na mshikamano wa dhati unaoongozwa na kanuni auni. Kwa Baba Mtakatifu Francisko adhimisho la Ekaristi Takatifu ni kiini cha maisha na utume wake, ndiyo maana anapenda kuwashirikisha wengine: matumaini na furaha ya Injili kila siku wakati wa Ibada ya Misa Takatifu na hasa wakati huu wa maambukizi makubwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID.

Baba Mtakatifu anapoadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu somo wake, Familia ya Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, inamtakia heri na baraka katika maisha na utume wake, aendelee kuwa Mchungaji mwema, mwaminifu, mtakatifu, mkweli na muwazi. Mtakatifu George amlinde na kumsimamia katika mapambano ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu katika haki na kweli! Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka ya Kipapa, anasema, maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu George, Somo wa Baba Mtakatifu Francisko yamepambwa kwa zawadi ya vifaa tiba kwa ajili ya waathirika wa ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona nchini Romania, Hispania na Italia. Hiki ni kielelezo cha upendo na mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayeguswa na mahangaiko ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Radio Vatican inamtakia pia kheri na baraka katika maisha na utume wake kwa maneno yafuatayo "Dominus conservet et vivificet eum".

Mtakatifu George

 

23 April 2020, 14:16