Mabadiliko Makubwa: Siku ya X ya Familia Duniani kuadhimishwa Juni 2022. Siku ya XXXVII ya Vijana Ulimwenguni kuadhimishwa sasa Mwezi Agosti mwaka 2023. Mabadiliko Makubwa: Siku ya X ya Familia Duniani kuadhimishwa Juni 2022. Siku ya XXXVII ya Vijana Ulimwenguni kuadhimishwa sasa Mwezi Agosti mwaka 2023. 

Mabadiliko: Siku X Familia: 2022! Siku ya XXXVII ya Vijana 2023!

Siku ya X ya Mkutano wa Familia Duniani iliyokuwa imepangwa kuadhimishwa Jimbo kuu la Roma kuanzia tarehe 23-27 Juni sasa imesogezwa mbele kwa mwaka mmoja na itaadhimishwa mwezi Juni 2022. Maadhimisho ya Siku ya XXXVII ya Vijana Ulimwenguni yaliyokuwa yafanyike Mwaka 2022 huko Lisbon, Ureno sasa yamesogezwa mbele na yataadhimishwa mwezi Agosti mwaka 2023.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya X ya Mkutano wa Familia Duniani iliyokuwa imepangwa kuadhimishwa Jimbo kuu la Roma, nchini Italia, kuanzia tarehe 23-27 Juni 2021 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu” sasa imesogezwa mbele kwa mwaka mmoja na itaadhimishwa mwezi Juni 2022. Uamuzi huu mgumu umefanywa na Baba Mtakatifu Francisko baada ya kujadiliana kwa kina na mapana na viongozi wa kuu wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Hii itakuwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka sita tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, dira na mwongozo wa maisha na utume wa familia. Kanisa litakuwa pia linakumbuka miaka minne tangu Baba Mtakatifu achapishe Waraka wake wa kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”. Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani Yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli.

Lengo la Wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu katika ulimwengu mamboleo; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu Francisko anasema, lengo la kuchagua tema hii ni kutaka kukazia mchakato wa utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika uhalisia wa kila siku wa mahusiano ndani ya familia. Nyaraka hizi mbili za Kipapa ziwe ni rejea mahususi katika maandalizi ya Siku ya X ya Mkutano wa Familia Duniani kwa mwaka 2022 utakaofanyika jimbo kuu la Roma. Upendo wa wanandoa ndani ya familia ni kielelezo cha zawadi kubwa inayowaunganisha wanandoa ili kurutubisha umoja na hivyo kubadilisha mwelekeo wa tabia ya ubinafsi, ulaji wa kupindukia pamoja na tabia ya kutojali: “Uzuri wa upendo unadhihirishwa kwa ile namna ya “kutazama” kunakowatafakari wengine kuwa ni malengo kama walivyo” (AL 128). Wakati huo huo kutambua watu wengine ndani ya familia takatifu kama: mume, mke, baba, mama, mtoto, binti, babu au bibi.

Ndoa na familia inatoa sura kamili ya upendo na kushuhudia maana ya mahusiano ya kibinadamu ambamo furaha na mapambano ya maisha yanakuwa ni sehemu ya vinasaba vya kila siku, vinavyowaongoza watu ili kukutana na Mwenyezi Mungu. Wanandoa wanapoiishi safari hii kwa uaminifu na udumifu, wanaimarisha upendo na wito wa utakatifu wa maisha unaomilikiwa na kila mmoja wao na kumwilishwa katika mahusiano ya ndoa na familia. Kwa maana hii basi, maisha ya familia ya Kikristo ni wito na njia ya utakatifu, “kielelezo makini cha sura ya Kanisa inayovutia” (GE  9). Hii ni taarifa iliyotolewa na Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican. Anaendelea kufafanua kwamba, Maadhimisho ya Siku ya XXXVII ya Vijana Ulimwenguni yaliyokuwa yafanyike Mwaka 2022 huko Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39 sasa yamesogezwa mbele na yataadhimishwa mwezi Agosti mwaka 2023.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni cheche ya mwanga wa imani, matumaini na zawadi kubwa ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II ameliachia Kanisa na kwamba, matunda ya maadhimisho haya ni juhudi za mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kabla, wakati na baada ya maadhimisho haya! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni maabara au karakana za imani, kama alivyopenda kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II, enzi zake!  Hapa pamekuwa ni chemchemi na chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba, Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, limejikuta likiwa na sura ya ujana, pasi na makunyanzi; Kanisa ambalo limewasukuma vijana kuendelea kujiaminisha kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vijana wamekuwa kweli ni wadau wa Heri za Mlimani, Manabii wa nyakati hizi na vyombo vya ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Vijana watambue kwamba, Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa lake; mahali ambapo vijana wanaweza kuchota tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni; ni chombo muhimu sana cha unjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; mahali ambapo wenye kiu na njaa ya maisha ya uzima wa milele wanaweza kushibishwa!  Hili ni Jukwaa la majadiliano kati ya Kanisa na Vijana, changamoto kwa pande hizi mbili anasema Mtakatifu Yohane Paulo II, ni kusikilizana kwa makini. Hii ni Epifania na ufunuo wa imani; ni mahali pa kupanga na kutekeleza mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya vijana. Hii ni amana na urithi mkubwa kutoka kwa Papa Yohane Paulo II kwa ajili ya Kanisa.

Siku ya Familia na Vijana
21 April 2020, 13:48