Tafuta

Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa sasa litaadhimishwa Mwezi Septemba 2021 Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa sasa litaadhimishwa Mwezi Septemba 2021 

Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Sasa Kuadhimishwa Sept. 2021 Hungaria

Muhimu sana: Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa lililokuwa limepangwa kuadhimishwa kuanzia tarehe 13-20 Septemba 2020, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7 sasa limesogezwa mbele hadi mwezi Septemba 2021. Uamuzi huu umetolewa na Papa Francisko na viongozi wahusika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa lililokuwa limepangwa kuadhimishwa kuanzia tarehe 13-20 Septemba 2020, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7 sasa limesogezwa mbele hadi mwezi Septemba 2021. Maamuzi haya mazito yametolewa na Baba Mtakatifu Francisko baada ya kushauriana na Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Hungaria. Haya yamebainishwa na Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican, tarehe 23 Aprili 2020. Janga kubwa la maambuki ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ndicho chanzo kikuu cha kusogezwa mbele kwa maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa.

Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa ilianzishwa rasmi na Papa Leo XIII kunako mwaka 1876 ili kusaidia mchakato wa kumwezesha Kristo Yesu: kufahamika, kupendwa na kutumikiwa kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na mioyo ya watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake.  Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na shule ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani.

Hili ni Fumbo kubwa linalopaswa kuadhimishwa vyema; Kuabudiwa na Kutafakariwa kikamilifu. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume, “Kaa Nasi Bwana”: Mane, Nobiscum Domine”, anawaalika waamini kujenga utambuzi hai wa uwepo halisi wa Kristo Yesu, katika adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu na katika Ibada nje ya Misa. Itakumbukwa kwamba, Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, kuanzia tarehe 25-31 Januari 2016 huko Cebu, nchini Ufilippini yaliongozwa na kauli mbiu “Kristo ndani mwenu, matumaini ya utukufu”.  Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai 1: 27.  Hii ilikuwa ni fursa makini ya kukuza na kuimarisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu nchini humo sanjari na Maadhimisho ya Miaka 500 tangu walipoinjilishwa kwa mara ya kwanza.  Hii ni changamoto ya kuhamasisha mchakato wa uinjilishaji mpya, ari na moyo wa kimissionari ili kumshuhudia Kristo Yesu kwa kina na mapana zaidi. Kwa mara ya kwanza, Hungaria ilikuwa mwenyeji wa Kongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa kunako mwaka 1938.

Kardinali Peter Erdo’ Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, Hungaria anasema, maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa yanapaswa kugusa hali halisi ya maisha ya watu wa Mungu ndani na nje ya Hungaria. Lengo ni kutangaza na kushuhudia uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi, ili kuwawezesha waamini kutambua na kukiri kwamba, kwa hakika Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho haya ni fursa kwa waamini kujichotea nguvu, ari na mwamko mpya wa maisha na utume wao katika medani mbali mbali za maisha na hasa wakati huu, hofu kubwa ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, inapoendelea kutishia usalama na maisha ya watu wengi duniani. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha umoja, udugu na mshikamano kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa walemavu ndani ya jamii.

Ekaristi Takatifu ni kikolezo makini cha Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya utume wa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kongamano hili litawawezesha waamini kutambua umuhimu wa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ili kukoleza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Kumbe, maadhimisho ya Makongamano la Ekaristi Takatifu katika ngazi mbali mbali ni fursa makini inayopania kupyaisha imani inayomwilishwa katika maisha ya watu, kielelezo makini cha imani tendaji.

kongamano Ekaristi Takatifu
23 April 2020, 14:36