Tafuta

Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 22 Aprili 2020 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia. Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 22 Aprili 2020 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia. 

Jubilei ya Miaka 50 ya Siku ya Mama Dunia 22 Aprili 2020

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda dunia dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na vitendo vyote vinavyotishia maisha na usalama wa viumbe hai. Kwa wakati huu, kuna uharibifu mkubwa sana wa mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 22 Aprili, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia. Hii ni fursa muhimu ya kutanabaisha uhusiano tegemezi uliopo baina ya watu na viumbe mbalimbali ambavyo vinashirikiana katika dunia hii. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Katika Sura ya kwanza ya Waraka wa Kitume “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote anaonesha madhara makubwa yanayotokana na uchafuzi wa mazingira pamoja na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu unaoendelea kuleta mabadiliko makubwa katika uso wa dunia, nyumba ya wote, kiasi cha kuigeuza kuwa ni shimo la takataka.

Hali hii inaweza kubadilishwa kwa kuwa na mwelekeo mpya wa uzalishaji unaojikita katika matumizi bora ya rasilimali za dunia pamoja na teknolojia rafiki. Mabadiliko ya tabianchi ni janga la kimataifa anasema Baba Mtakatifu Francisko, kama ilivyo pia haki ya maji safi na salama; yanayopaswa kutunzwa vyema kwani ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kwa ajili ya wote na kwamba, haki hii inaambata utu wa mwanadamu. Kiini cha yote haya anasema Baba Mtakatifu ni kutunza utofauti unaojitokeza katika bayianuai kwani kutokana na utunzaji mbaya wa mazingira kila mwaka kunatoweka jamii za mimea na za wanyama, ambazo kamwe kizazi kijacho hakitaziona tena.

Kuna deni kubwa la ekolojia, kati ya Nchi za Kaskazini na zile zilizoko Kusini; zinazounganishwa kutokana na uwiano duni wa biashara. Nchi changa duniani zinaelemewa na deni la nje, hali ambayo inatumiwa sasa kama chombo cha kudhibiti maendeleo, jambo ambalo halifanyiki katika deni la kiekolojia. Kutokana na kuendelea kumong’onyoka kwa mazingira na jamii anasema Baba Mtakatifu waathirika wakuu ni maskini duniani ambao hawapewi uzito unaostahili. Kumbe, mwelekeo sahihi wa kiekolojia hauna budi kufumbatwa katika mwelekeo wa kijamii na wala si kwa kudhibiti kiwango cha watu kuzaliana; bali kwa kuwa na mtazamo mpya juu ya ulaji wa kupindukia na tabia ya kuchagua vyakula kupita kiasi hali ambayo inaendelea sehemu nyingine za dunia. Kuna haja ya kuwa na mabadiliko katika mawazo yanayomwajibisha mtu katika ulimwengu mamboleo, ili kujenga mfumo wa sheria utakaohakikisha usalama wa mifumo ya mazingira.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres katika kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda dunia dhidi ya homa kali inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na vitendo vyote vinavyotishia maisha na usalama wa viumbe hai. Kwa wakati huu, kuna uharibifu mkubwa sana wa mazingira. Kuna majanga ya moto sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee nchini Australia. Kuna ongezeko la kiwango kikubwa cha joto duniani kinachotishia usalama wa maisha ya watu na mali zao kutokana na ongezeko la kina cha maji baharini, ukame na mafuriko ya kutisha. Leo hii janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni gonjwa ambalo linahusianishwa na ekolojia. Kuna uchafuzi mkubwa wa vyanzo vya maji na pamoja na hewa.

Kuna athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi zinazotokana na shughuli zinazofanywa na binadamu. Kwa mfano ufyekaji mkubwa wa misitu, kilimo kisichozingatia: sheria na kanuni za kilimo bora pamoja na magonjwa yanayowashambulia binadamu na wanyama. Yote haya yanaonesha kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya: binadamu, wanyama na mazingira katika ujumla wake. Kuna haja ya kusimama kidete ili kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa sababu madhara yake ni makubwa katika mchakato wa ukuaji wa uchumi kitaifa na kimataifa. Ilikuwa ni tarehe 22 Aprili 1970, miaka 50 iliyopita, wananchi wa Marekani “walipotinga barabarani” kudai sera makini za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Hii ni changamoto endelevu inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake.

Siku ya Mama Dunia 2020

 

21 April 2020, 13:13