Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa! Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa!  (ANSA)

Papa awashukuru na kuwapongeza waandishi wa habari!

Watangazaji wa RAI wamemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Ijumaa kuu, imekuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kufanya tafakari ya kina kuhusu: Fumbo la mateso na kifo cha Kristo Yesu, kililetacho wokovu kutoka katika dhambi na uvuli wa mauti! Anaguswa na mateso ya watu wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Mawasiliano yanayotekelezwa na Mama Kanisa si matangazo ya biashara wala wongofu wa shuruti. Kanisa linakuwa, linakomaa na kupeta kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa yanafumbatwa katika ushuhuda; ukweli, uzuri na wema. Huu ndio ushuhuda wa wafiadini na waungama imani; watu walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mawasiliano ndani ya Kanisa ni mchakato unaofumbatwa katika ujasiri pasi ya kukata wala kukatishwa tamaa na hatimaye, kumezwa na malimwengu na hiki ni kishawishi cha Shetani, Ibilisi, hata katika karne ya ishirini na moja. Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa Kuu, tarehe 10 Aprili 2020 amepiga simu na kuzungumza mubashara na watangazaji wa Kipindi cha kidini kijulikanacho kama “A Sua Immagine” kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Taifa nchini Italia, RAI, ili kuwapongeza na kuwashukuru kwa kazi kubwa wanayoifanya hasa wakati huu ambapo familia, Kanisa dogo la nyumbani linategemea sana matangazo kutoka kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii.

Kwa namna ya pekee kabisa, watangazaji wa RAI wamemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu amewahakikishia uwepo wake wa daima kwa njia ya sala, sadaka na tafakari ya kina ya Neno la Mungu. Ijumaa kuu, imekuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kufanya tafakari ya kina kuhusu: Fumbo la mateso na kifo cha Kristo Yesu, kililetacho wokovu kutoka katika dhambi na uvuli wa mauti! Imekuwa ni nafasi pia ya kuendelea kutafakari sadaka na maisha ya watu wanaojitosa kimasomaso kwa ajili ya kuwasaidia jirani zao hasa katika mapambano dhidi ya maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, CVID-19. Hawa ni madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya. Katika orodha hii, wamo pia watawa na mapadre ambao wameyamimina maisha yao kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Bikira Maria, chini ya Msalaba. Hata leo hii, bado kuna watu wanajisadaka kama kielelezo cha Injili ya upendo kwa jirani zao.

Baba Mtakatifu anasema katika maadhimisho ya Liturujia ya Ijumaa Kuu pamoja na Njia ya Msalaba, amewakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu katika shida na mahangaiko yao. Lakini zaidi, amewaombea ili waweze kuwa na imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19. Pasaka ya Bwana iwe ni fursa ya kupyaisha tena amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa Mungu. Katika kipindi hiki cha ukame wa maisha ya kiroho kutokana na itifaki inayozuia mikusanyiko ya watu, Baba Mtakatifu ameendelea kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyokuwa inarushwa moja kwa moja kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha mjini Vatican. Amekuwa na matukio ya sala na hija kwa ajili ya kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Baba Mtakatifu amewahakikishia wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kwamba, anawapenda na kuthamini sana mchango wao katika maisha na utume wa watu wa Mungu!

Papa: RAI 2020
11 April 2020, 17:06