Baba Mtakatifu Francisko Sherehe ya Pasaka 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Kutoa Ujumbe wake wa Pasaka: Urbi et Orbi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mt. Petro uliokuwa tupu! Baba Mtakatifu Francisko Sherehe ya Pasaka 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Kutoa Ujumbe wake wa Pasaka: Urbi et Orbi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mt. Petro uliokuwa tupu! 

Papa Francisko: Urbi et Orbi: Ujumbe wa Pasaka Mwaka 2020

Papa asema, Pasaka ya mwaka 2020 imegubikwa na upweke, majonzi pamoja na athari kubwa za: kiroho, kimwili na kijamii ambazo zimesababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Waamini wengi wameshindwa kuchota huruma, upendo na baraka za Mwenyezi Mungu kutoka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na ile ya Upatanisho. Hata katika muktadha huu, Mwenyezi Mungu bado yupo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 12 Aprili 2020, ameadhimisha Sherehe ya Pasaka ya Bwana, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baadaye ametoa ujumbe wa Pasaka: “Urbi et Orbi”. Itakumbukwa kwamba, Ilikuwa ni tarehe 17 Aprili 1949, Mtumishi wa Mungu Papa Pio XII, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, alipotuma Ujumbe wa Pasaka “Urbi et Orbi” kwa njia ya Televisheni ya Ufaransa, akiwatakia waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema heri na baraka za Sherehe ya Pasaka. Katika ujumbe huo, alikazia umuhimu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na waamini katika ujumla wao, kukutana katika uwanja wa mawasiliano na kwa wakati huo, Televisheni. Katika muktadha huu, njia za mawasiliano na mitandao ya jamii imekuwa ni msaada mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa na hasa wakati huu wa janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.  

Baba Mtakatifu katika Ujumbe wake wa Pasaka kwa Mwaka 2020 anasema kwa hakika Kristo Yesu Amefufuka kweli kweli! Huu ni ujumbe wa matumaini hata katika nyakati hizi ambazo mwanadamu anakabiliwa na changamoto kubwa ya janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19! Kwa hakika familia kubwa ya binadamu imeguswa na kutikiswa sana, lakini Kanisa linatangaza kwamba, Kristo Yesu, tumaini lake, kweli amefufuka! Huu ni wakati wa “kuambukizana” fadhila ya matumaini, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya ushindi wa upendo, dhidi ya mateso na kifo; ushindi ambao umegeuza ubaya kuwa wema kama kielelezo cha nguvu ya Mungu inayookoa. Kristo Yesu ndiye yule aliyeteswa, akafa na sasa amefufuka kwa wafu. Katika mwili wake mtukufu anabeba Madonda Matakatifu, chemchemi ya matumaini yanayoganga, kuponya na kutakasa madonda ya mwanadamu. Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa katika Salam zake za Pasaka amewakumbuka wale wote walioguswa na kutikiswa na homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hawa ni wagonjwa, watu waliofariki dunia na familia zao zinaendelea kuwakumbuka na kuwaombolezea.

Baba Mtakatifu anawaombea marehemu wote ili waweze kupokelewa na Bwana wa uzima na kuwakirimia matumaini wale ambao bado wanateseka na kujaribiwa sana, yaani wazee na watu wanaoishi katika hali ya upweke. Wapate faraja wale wote wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika mazingira hatarishi; hawa ni wale wanaowahudumia wagonjwa na wazee, wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama bila kuwasahau wafungwa. Pasaka ya mwaka 2020 imegubikwa na upweke, majonzi pamoja na athari kubwa za: kiroho, kimwili na kijamii ambazo zimesababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Waamini wengi wameshindwa kuchota huruma, upendo na baraka za Mwenyezi Mungu kutoka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na ile ya Upatanisho. Hata katika muktadha huu, Mwenyezi Mungu bado ameendelea kuwa na waja wake, changamoto na mwaliko ni kuendelea kushikamana katika sala, kwani kwa hakika, atawanyooshea mkono wake na kuwatia shime, wasiogope kwani Kristo Mfufuka yuko daima pamoja nao! Kristo Pasaka ya watu wake, awakirimie nguvu na matumaini madaktari na wauguzi wanaotoa ushuhuda wa huduma ya upendo hadi tone la mwisho, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao.

Baba Mtakatifu anawakumbuka wafanyakazi wanaoendelea kujisadaka ili kuhakikisha kwamba, watu wanapata huduma muhimu katika maisha yao ili kudumisha utulivu. Anawakumbuka wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama wanaoendelea kutoa huduma mbali mbali ili kuwasaidia wananchi wanaoteseka; wote hawa wanapaswa kupewa shukrani na kuheshimiwa. Itifaki ya kudhibiti maambukizi mapya ya Virusi vya Corona, COVID-19 imewalazimisha watu kubaki majumbani mwao, changamoto ambayo imebadili kwa ghafla mtindo wa maisha ya watu wengi. Imekuwa ni nafasi ya kufurahia uwepo watu wengine katika maisha yao. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wanasiasa na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa watende kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wao, kwa kuwajengea uwezo na kuwapatia nyenzo msingi zitakazowasaidia kuishi katika utu wema na pale hali itakapokuwa imetulia waweze kuanzisha mchakato wa shughuli za kila siku.

Baba Mtakatifu anasema, huu ni muda wa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano unaokita mizizi yake katika matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka. Yesu awe ni matumaini kwa maskini, watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum. Maskini sehemu mbali mbali za dunia, wapewe mahitaji msingi katika maisha pamoja na huduma bora ya afya. Ni wakati wa kuondoa vikwazo vya kiuchumi vinavyodidimiza maisha ya watu wengi katika nchi zile ambazo zimewekewa vikwazo na Jumuiya ya Kimataifa. Mshikamano wa huduma ya upendo uoneshwe hata katika Nchi changa duniani, kwa kuzifutia madeni yake. Ubinafsi ni dhana ambayo kwa sasa imepitwa na wakati. Baba Mtakatifu anaikumbusha Jumuiya ya Ulaya kwamba, nchi nyingi ziliweza kusimama tena baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia kutokana na mshikamano uliowasaidia kuvuka kinzani na misigano ya zamani. Umoja na mshikamano uwe ni utambulisho wa watu wa Mungu Barani Ulaya, kwa kusaidiana kwa hali na mali. Hii ni changamoto changamani kwa Jumuiya ya Ulaya na Ulimwengu katika ujumla wake.

Huu ni muda muafaka wa kujenga na kudumisha mshikamano kwa kujikita hata katika suluhu mpya. Watu wasilogwe kwa kutaka kuyakumbatia yaliyopita, kwa sababu mwelekeo wa namna hii unaweza kuhatarisha amani, mafungamano ya kijamii pamoja na maendeleo fungamani kwa vizazi vijavyo! Huu si muda wa kuendekeza kinzani na migawanyiko, bali kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Baba Mtakatifu Francisko anasema si wakati hata kidogo wa kuendelea kutengeneza, kulimbikiza na kutumia silaha na badala yake, rasilimali fedha hii, itumike kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu. Ni muda muafaka wa kusitisha vita ambayo kwa muda mrefu imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao huko Siria, Yemen, Iraq na Lebanon. Ni muda uliokubalika kwa Waisraeli na Wapalestina kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kisiasa katika ukweli na uwazi, ili kupata suluhu ya kudumu itakayoziwezesha nchi hizi mbili kuishi kwa amani. Vita ikomeshwe huko Ukraine ya Mashariki sanjari na vitendo vya kigaidi vinavyotishia maisha ya watu wasiokuwa na hatia huko Barani Afrika.

Dharura ya wakati huu kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 usiifanye Jumuiya ya Kimataifa ikasahau majanga mbali mbali yanayoendelea kuwakumba watu wengi sehemu mbali mbali za dunia. Bwana wa uzima awe karibu na familia ya Mungu Barani Afrika na Asia inayokabiliwa na mateso makubwa ya kibinadamu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amelitaja Jimbo la Cabo Delgado, lililoko Kaskazini mwa Msumbiji linakobaliwa na changamoto kubwa! Baba Mtakatifu amewakumbuka: Wakimbizi na wahamiaji, wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao kutokana na vita, majanga asilia na umaskini. Mwenyezi Mungu awalinde na kuwapatia tunza yake ya daima wakimbizi, wahamiaji na hasa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi huko Libia na katika mipaka kati ya Ugiriki na Uturuki. Ameiombea Venezuela iweze kupata suluhu ya kudumu pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kutoa misaada ya hali na mali kwa watu wa Mungu nchini humo wanaoteseka kutokana na mipasuko ya kisiasa, kijamii, athari za kiuchumi pamoja na huduma duni zinazotolewa!

Katika kipindi hiki, watu wa Mungu hawapendi hata kidogo kusikia maneno ya watu kutojali, ubinafsi, kinzani na usahaulifu. Ni wakati wa kuondokana na hofu ya kifo na kumwachia nafasi Kristo Yesu, ili aweze kupata ushindi katika sakafu ya mioyo na maisha yao. Kristo Yesu aliyeshinda dhambi na mauti kwa kuwafungulia njia ya wokovu wa milele, avunjilie mbali giza na umaskini wa binadamu; awaongoze katika Siku yake ya Utukufu isiyokuwa na machweo!

Papa: Urbi et Orbi

 

12 April 2020, 14:18