Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Ujumbe wa Pasaka: Ni kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa watu wa Mataifa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto, kielelezo cha imani tendaji! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Ujumbe wa Pasaka: Ni kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa watu wa Mataifa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto, kielelezo cha imani tendaji!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Ujumbe wa Pasaka: Ushuhuda kwa Kristo Mfufuka!

Waamini wanaitwa kutangaza kwa maneno lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha kwamba, kwa hakika Kristo Yesu amefufuka. “Kristo tumaini langu amefufuka kwa wafu” ni ujumbe unaopaswa kusikika tena majumbani na katika nyoyo, ili kuimarisha imani kwa Wabatizwa na kuwatia shime wale wote wanaokabiliana na mateso pamoja na matatizo makubwa katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Mama Kanisa katika Kipindi cha Pasaka anajiunga na Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa kufurahia ushindi wa Kristo Mfufuka kutoka kwa wafu kwa Sala ya Malkia wa Mbingu inayotumika kipindi chote cha Pasaka! Baba Mtakatifu Francisko, katika tafakari yake, Jumatatu ya Pasaka, maarufu kama Jumatatu ya Malaika, tarehe 13 Aprili 2020 amesema kwamba, bado mwangwi wa furaha ya Pasaka unaendelea kusikika, Kristo Yesu hayupo tena kaburini! Wanawake wakaondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari. Na tazama, Yesu akakutana nao, akawasalimia na kuwapatia ujumbe maalum! “Msiogope; enendeni, mkawambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona” Mt. 28:10. Ni katika muktadha huu, Kristo Mfufuka anawaaminisha wanawake dhamana ya kimisionari mbele ya Mitume wake. Wanawake wameonesha kwa namna ya pekee uaminifu wao mbele ya Kristo Yesu; wakajitosa kimasomaso; wakamhudumia kwa upendo, Kristo Yesu katika maisha yake ya hadhara.

Wanawake wakamsindikiza katika Njia ya Msalaba kuelekea mlimani Kalvari na hatimaye, Yesu Kristo Mfufuka anawakirimia zawadi kubwa ya kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Ufufuko kutoka kwa wafu! Wanawake wakawa wa kwanza, akafuatia Mtakatifu Petro, Mtume! Kristo Yesu alikwisha kuwatangazia Mitume wake kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wake, lakini kwa bahati mbaya, Mitume hawakulifahamu Fumbo hili, kwa sababu anasema Baba Mtakatifu Francisko hawakuwa tayari. Imani yao ilipaswa kukua na kukomaa, baada ya Ufufuko na kushukiwa na Roho Mtakatifu! Mwanzoni mwa Kitabu cha Matendo ya Mitume, Mwinjili Luka, anasimulia ujasiri wa Mtakatifu Petro aliyethubutu kusema kwamba, Yesu huyo Mungu alimfufua, na wao ni mashuhuda wake! Rej. Mdo. 2:32. Tangu wakati huo habari kwamba, Kristo Yesu amefufuka kwa wafu ikaenea sehemu mbali mbali za dunia! Huu ukawa ni ujumbe wa matumaini kwa watu wote. Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu ni ushuhuda kwamba, kifo hakina nguvu tena; ufufuko ni ujumbe wa uhai. Kwa njia ya ufufuko wa Kristo Yesu, Mwana mpendwa wa Baba wa milele, Mwenyezi Mungu ameufunua utimilifu wa upendo na huruma yake kwa binadamu wa nyakati zote.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ikiwa kama Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, sasa inawezekana kabisa kuyaangalia matukio mbali mbali ya maisha ya mwanadamu kwa imani na matumaini makubwa. Hata kama binadamu anakabiliana na magumu, hofu na hali ya kutokuwa na uhakika wa hatima ya maisha yake kwa siku za usoni, bado anaweza kuendelea kuwa na matumaini. Ujumbe wa Pasaka ni huu, waamini wanaitwa na kuhamasishwa kutangaza kwa maneno lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha kwamba, kwa hakika Kristo Yesu amefufuka kwa wafu. “Kristo tumaini langu amefufuka kwa wafu” ni ujumbe unaopaswa kusikika tena na tena majumbani na katika sakafu ya nyoyo za waamini, ili kuimarisha imani kwa Wabatizwa na kuwatia shime wale wote wanaokabiliana na mateso pamoja na matatizo makubwa katika maisha.

Bikira Maria alikuwa ni shuhuda wa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, Mwanae wa pekee, katika hali ya ukimya! Bikira Maria awasaidie waamini kuamini kwa dhati kabisa kutoka katika undani wa mioyo yao kuhusu Fumbo hili la Ukombozi, linapopokelewa kwa imani thabiti, linaweza kuwa ni chachu ya mabadiliko makubwa katika imani. Huu ndio ujumbe wa Pasaka ambao Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuurudia tena kwa watu wote! Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka waamini chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kwa kusali pamoja ile Sala ya Malkia wa Mbingu.

Papa: Jumatatu ya Pasaka

 

13 April 2020, 14:26