Tafuta

Vatican News
Papa Francisko. Ujumbe wa Pasaka: Ni uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Papa Francisko. Ujumbe wa Pasaka: Ni uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Pasaka: Uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake!

Papa Francisko anasema Ujumbe wa Pasaka ya Bwana ni mwaliko kwa waamini wote kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kwa kutekeleza ahadi zao za Ubatizo, lakini zaidi kwa kuwa ni mashuhuda wenye furaha na vyombo vya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Kipindi cha Pasaka ni wakati muafaka wa kumwilisha upendo wenye huruma kwa maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano, tarehe 22 Aprili 2020 kwa kuungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia amewatakia heri na baraka, watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia waliokuwa wamejiunga naye kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya jamii ili kufuatilia katekesi yake. Ujumbe wa Pasaka ya Bwana ni mwaliko kwa waamini wote kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kwa kutekeleza ahadi zao za Ubatizo, lakini zaidi kwa kuwa ni mashuhuda wenye furaha na vyombo vya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti na hivyo anawakirimia waja wale nguvu ya kupokea mateso na mahangaiko katika maisha kama fursa ya wokovu. Kwa njia ya Ubatizo, waamini wanazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu. Pasaka ni wakati muafaka wa kunafsisha upendo kwa kuendelea kuthamini kazi ya uumbaji sanjari na kuwahudumia watu wote wanaounda familia kubwa ya binadamu!

Kipindi cha Sherehe ya Pasaka ya Bwana ni wakati muafaka wa kumwilisha upendo wenye huruma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Sherehe ya Pasaka ni mwanzo wa maisha mapya, changamoto na mwaliko wa kulinda na kutunza mazingira. Katika kipindi hiki cha hofu, mashaka na taharuki kutokana na ugonjwa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Baba Mtakatifu anawaombea waamini kuwa na matumaini, upendo na mshikamano na watu wote! Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Hii ni Amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu tangu alipowaumba Adamu na Eva! Utunzaji bora wa mazingira ni jukumu la kila mtu kadiri ya nafasi na uwezo wake ndani ya jamii!

Papa: Mazingira
22 April 2020, 12:31