Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kukimbilia huruma ya Mungu na maombezi ya Mtakatifu Yohane Paulo II katika shida na mahangaiko yao! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kukimbilia huruma ya Mungu na maombezi ya Mtakatifu Yohane Paulo II katika shida na mahangaiko yao! 

Papa Francisko: Kimbilieni huruma ya Mungu katika shida zenu!

Katika kipindi hiki kigumu cha wasi wasi na hofu ya maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID, Baba Mtakatifu anawataka waamini kukimbilia Huruma ya Mungu kwa njia ya maombezi ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Mama Kanisa anapoadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 15 tangu alipofariki dunia, hapo tarehe 2 Aprili 2005.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake kuhusu Heri za Mlimani, Jumatano tarehe 01 Aprili 2020, amegusia kuhusu alama za kifo zinazomzunguka mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Watu wanaishi katika hofu na taharuki kubwa! Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumkimbilia Kristo Yesu kwa kutambua kwamba, hawako peke yao. Kwa hakika Yesu, atawasindikiza na kuwaongoza kwa sababu kamwe hawezi kumdanganya mtu. Katika kipindi hiki kigumu cha wasi wasi na hofu ya maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID, Baba Mtakatifu anawataka waamini kukimbilia Huruma ya Mungu kwa njia ya maombezi ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Mama Kanisa anapoadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 15 tangu alipofariki dunia, hapo tarehe 2 Aprili 2005.

Baba Mtakatifu amewakumbuka watu na makundi mbali mbali yaliyokuwa yamejiandaa kukutana naye kwa ajili ya katekesi, lakini kutokana na hali halisi, yote haya yamesndikana. Anawatakia heri na baraka vijana kutoka Jimbo kuu la Milano, Italia ambao walikuwa wamejiunga naye kwa njia ya Televisheni, lakini, hata katika hali na mazingira kama haya, anaonja uwepo wao! Anawashukuru kwa ujumbe na matashi mema waliomwandikia na kwamba, anawaombea katika safari ya maisha yao na wao, wasichoke kumsindikiza kwa sala na sadaka yao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Waendelee kutambua uwepo wa Kristo kati yao, wajitahidi kuwa marafiki waaminifu ili aweze kuwakirimia furaha na utimilifu wa maisha hata katika nyakati hizi ngumu. Amewataka waamini kujiandaa vyema katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, ili kila mmoja wao, aweze kuonja uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika hija ya maisha yake ya kila siku!

Papa: Huruma ya Mungu

 

01 April 2020, 14:00