Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza na kuwashukuru wanawake kwa mchango wao mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza na kuwashukuru wanawake kwa mchango wao mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Papa: Shukrani na pongezi kwa wanawake kwa sadaka na huduma!

Papa Francisko anawashukuru na kuwapongeza wanawake wanaojisadaka bila ya kujibakiza katika kipindi hiki cha kipeo cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona. Hawa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaotekelezwa na madaktari na wauguzi wanawake; Askari wa kike wa vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na wafanyakazi wanaotoa huduma mbali mbali za kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya tafakari kuhusu dhamana na utume wa wanawake katika Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu pamoja na utume wao kwa Kanisa katika ujumla wake, Jumatatu ya Malaika, katika Kipindi cha Oktava ya Pasaka, tarehe 13 Aprili 2020 ameyaelekeza mawazo na shukrani zake kwa wanawake wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza katika kipindi hiki cha kipeo cha maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hawa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaotekelezwa na madaktari na wauguzi wanawake; bila kuwasahau wanawake walioko kwenye vikosi vya ulinzi na usalama; Askari magereza pamoja na wafanyakazi wanaoendelea kutoa huduma mbali mbali za kijamii.

Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa wanawake na wasichana ambao wako karantini, lakini wanaendelea kuhudumia familia zao; wanawatunza watoto, wazee na walemavu! Kwa bahati mbaya, wanawake ni kati ya wahanga ambao wanaweza kukumbwa na mashambulizi na nyanyaso mbali mbali. Ni watu wanaobeba sadaka kubwa katika kuzitegemeza familia zao. Baba Mtakatifu anawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka na kuwaombea wanawake na wasichana, ili Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuwakirimia nguvu na ujasiri wa kutekeleza dhamana na majukumu yao katika familia na jamii katika ujumla wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia watu wote baraka na furaha ya Sherehe ya Pasaka. Katika kipindi hiki, Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea wakiwa wameungana katika sala pamoja na kusaidiana kama ndugu wamoja!

Papa: Wanawake

 

 

13 April 2020, 14:02