Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi Kuu 2020 amewaongoza waamini katika Mkesha wa Pasaka ya Bwana: Amewataka waamini kuondoa hofu kwa kukazia matumaini na ujasiri! Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi Kuu 2020 amewaongoza waamini katika Mkesha wa Pasaka ya Bwana: Amewataka waamini kuondoa hofu kwa kukazia matumaini na ujasiri! 

Papa Francisko: Mahubiri ya Mkesha wa Sherehe ya Pasaka 2020

Baba Mtakatifu amewaongoza waamini kwenye liturujia ya Neno la Mungu, Liturujia ya Ubatizo na hatimaye, Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Katika mahubiri yake Papa amegusia umuhimu wa Kesha la Pasaka ambalo ni Mama wa mikesha yote inayoadhimishwa na Kanisa. Dhamana na Utume wa wanawake katika Fumbo la Ufufuko! Msiogope! Haki ya Matumaini na Ujasiri wa wanawake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 11 Aprili 2020 ameongoza “Kesha la Pasaka” kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika Liturujia ya Mwanga akabariki moto wa Pasaka na kuongoza maandamano kuingia Kanisani na baadaye ikaimbwa “Mbiu ya Pasaka” inayosimulia “Sifa ya Mshumaa wa Pasaka”, kielelezo cha Kristo Mfufuka. Baba Mtakatifu amewaongoza waamini kwenye liturujia ya Neno la Mungu, Liturujia ya Ubatizo na hatimaye, Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amegusia umuhimu wa Kesha la Pasaka ambalo ni Mama wa mikesha yote inayoadhimishwa na Kanisa. Dhamana na utume wa wanawake katika Fumbo la Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Msiogope! Haki ya Matumaini na Ujasiri wa wanawake!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kesha la Pasaka, pengine ni kati ya matukio ambayo hayapewi uzito wake kutokana na haraka ya kutaka kuondokana na Msalaba wa mateso ya Kristo Yesu, Ijumaa kuu, ili Jumapili ya Pasaka, waweze kuimba kwa shangwe ile Aleluiya kuu! Wanawake walishuhudia mateso na kifo cha Kristo Yesu Msabani, wakayabeba matukio yote haya na kuyahifadhi katika sakafu ya mioyo yao! Walishikwa na woga, kwani walishindwa kutambua hatima ya maisha yao, wakawa wanajipanga jinsi ya kujenga kesho yenye matumaini. Kumbu kumbu ya wanawake hawa ilikuwa imejeruhiwa sana, matumaini yao “yakaingia mchanga” kutokana na giza nene mbele ya macho yao kama ilivyo hata kwa wafuasi wa Kristo Yesu nyakati hizi!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, wanawake walionesha ujasiri wa ajabu, kiasi cha kutojifungia katika undani wao kwa maombolezo na hali ya kukata tamaa! Waliandaa manukato kwa ajili ya kuupaka mwili wa Yesu, kielelezo cha ushuhuda wa upendo unaowasha taa ya huruma ya Mungu katika maisha ya watu! Itakumbukwa kwamba, Jumamosi kuu ni Siku maalum iliyotengwa kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria ambaye katika majonzi na masikitiko yake makubwa, anajiaminisha na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Wanawake hawa anasema Baba Mtakatifu walikuwa wanaandaa bila kutambua mapambazuko ya Siku ya Kwanza ya Juma, ambayo ingeleta mabadiliko makubwa katika historia ya mwanadamu. Huu ni mwanzo wa maisha mapya yanayomwezesha mwanadamu kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Wanawake kwa njia ya sala na upendo wao wa dhati, walisaidia mchakato wa kuibua matumaini mapya! Baba Mtakatifu anawauliza watu wa Mungu, Je, ni watu wangapi ambao kweli katika janga hili la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 wamekuwa kweli ni mashuhuda na vyombo na  matumaini kwa watu waliokata tamaa? Je, ni wangapi wanaoendeleza moto huu kwa sala na matendo ya huruma? Asubuhi na mapema, Siku ya kwanza ya Juma, wanawake walikwenda kaburini na kukutana na Malaika aliyewaambia: “Msiogope ninyi! Hayupo hapa: kwani amefufuka kama alivyosema”. Ndani ya kaburi wazi, wanasikia maneno yenye kuwatia shime, faraja na matumaini. Msiogope ni tamko la matumaini. Leo hii ndilo neno ambalo Mwenyezi Mungu anapenda kuwaambia watoto wake wote, hasa katika kipindi hiki ambacho mwanadamu anapita katika giza nene kutokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kesha la Pasaka iwe ni fursa ya kujitwalia haki ya matumaini mapya yanayotoka kwa Mwenyezi kama zawadi kubwa, ambayo kamwe wasingeweza kujitwalia wenyewe! Yote yatakwenda vyema “Tutto andrà bene” ni maneno yanayosikika midomoni mwa watu wengi kama kielelezo cha matumaini, ingawa bado watu wengi wameelemewa na hofu pamoja na taharuki, kiasi hata cha kutishia matumaini kuweza kuyeyuka kama “ndoto ya mchana”. Matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu yanaweka ndani ya moyo wa mwamini uhakika kwamba, Mwenyezi Mungu atatenda yote vyema na kwamba, hata kaburini ataweza kuchipua maisha mapya!

Kaburi ni mahali ambapo mtu akiisha ingia humo hawezi kutoka tena. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka ili kuwakirimia waja wake maisha mapya! Kumbe, hakuna sababu ya kuogopa wala kuweka jiwe la mlango wa kaburi katika matumaini. Kristo yuko pamoja na waja wake na kamwe hawezi kuwaacha katika mateso, mahangaiko na kifo. Mwanga wake umeng’ara na kuliangazia giza la kaburi na leo hii anataka kuingia na kugusa undani wa giza la maisha ya waja wake, ili kupyaisha matumaini kwa sababu Mungu ni mkuu! Giza na uvuli wa mauti havina tena nguvu! Jipeni moyo watu wa Mungu kwani kwa kushikamana na Mwenyezi Mungu hakuna kitu kinachoweza kupotea!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu, daima anapenda kuwatia shime waja wake, ili wawe na ujasiri! Waweze kusimama tena na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu! Watu wanapoanguka wasikate tamaa kwa sababu Mwenyezi Mungu anapenda kuwanyooshea mkono na kuwasimamisha tena! Huu ni ujasiri wa kutoa na kupokea kama zawadi. Yote haya yanawezekana kwa mwamini kufungua hazina ya moyo wake kwa njia ya sala, ili kuondoa lile jiwe kwenye kaburi la moyo wake, ili hatimaye, mwanga wa Kristo Mfufuka uweze kupenya! Huu ni mwaliko kwa waamini kumkimbilia Kristo Yesu katika shida na mahangaiko yao, daima wakimtumainia kwani kwa kugusa Msalaba wa mateso yake, wanaweza kupata maisha mapya.

Mwenyezi Mungu anawasindikiza waja wake wanapokuwa wanapita katika giza na uvuli wa mauti kwani Yeye ni cheche za matumaini katika hali ya kukata tamaa! Ni neno lenye nguvu wakati wa kimya kikuu na daima anapenda kuwashibisha kwa upendo wake usiokuwa na mipaka na wala hakuna mtu awaye yote anayeweza kuthubutu kuwapoka! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mbiu ya Pasaka ni ujumbe wa matumaini. Yesu anawatuma waja wake “Nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake kwamba, amefufuka katika wafu. Tazama awatangulia kwenda Galilaya, ndiko watakakomwona! Yesu anawatangulia wanafunzi wake Galilaya, mahali ambapo kuna kumbu kumbu ya kudumu, mahali ambapo wanafunzi wake, walipata wito wao wa kwanza! Wanafunzi wanapaswa kurejea tena Galilaya, ili kukumbuka kwamba, kwa hakika wanapendwa na wameitwa na Mwenyezi Mungu. Kumbe, kuna haja ya kuendeleza mchakato wa safari kwa kupyaisha upendo. Hapa ndipo mahali pa kuanzia daima hasa nyakati zile za mateso na majaribu ya maisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua sifa za mji wa Galilaya kuwa: kijiografia ni mji uliokuwa mbali na utakatifu wa Mji Mtakatifu wa Yerusalemu. Huu ni mji uliokuwa unakaliwa na watu wa Mataifa. Ni mahali ambapo Kristo Yesu, alianzia na kukamilisha utume wake. Hapa ni mahali pa kukutana na Kristo Yesu, ambaye ni chemchemi ya maisha mapya! Inapendeza sana kwa Wakristo ikiwa kama wataendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya faraja, ujasiri na watangazaji wa Injili ya uhai. Galilaya ni mji wa wote kwa sababu wote ni ndugu na wanabeba ndani mwao wimbo wa maisha. Huu ni wakati wa kusimama kidete na kupiga kelele ili kusitisha vita!

Ni wakati wa kuondokana na utengenezaji, usambazaji na ulimbikizaji wa silaha, kwa sababu watu wengi wana njaa ya chakula na wala si mtutu wa bunduki. Ni muda wa kuachana na utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji na vizuia mimba vinavyofyekelea mbali maisha ya watu wasiokuwa na hatia. Watu wa Mungu waoneshe wema, upendo na ukarimu kwa kuwakunjulia mikono watu wenye shida na mahangaiko mbali mbali katika maisha; watu wanaokosa hata mahitaji msingi ya maisha. Baada ya mambo yote yale, wanawake wakakaribia, wakamshika miguu na kumsujudia. Hii ni miguu ambayo imesafiri sana ili kuweza kukutana na waja wake kwa kuingia na hatimaye, kutoka kaburini. Ni miguu inayovunjilia mbali utamaduni wa kifo na kuwafungulia waamini njia ya matumaini. Daima waamini ni mahujaji wanaotafuta fadhila ya matumaini! Ndio maana katika Kipindi hiki cha Pasaka, waamini wote wanataka kumzunguka Yesu Mfufuka, kwa kukipatia kifo kisogo na hatimaye, kumfungulia Kristo Yesu, nyoyo zao kwa sababu Yesu ni uzima!

Papa: Kesha la Pasaka

 

12 April 2020, 14:00