Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya Matawi, tarehe 5 Aprili 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu sanjari na Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwenguni bila uwepo wa waamini wengi. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya Matawi, tarehe 5 Aprili 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu sanjari na Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwenguni bila uwepo wa waamini wengi. 

Papa Francisko: Mahubiri ya Jumapili ya Matawi, 2020: Huduma!

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Framcisko amekazia kuhusu dhana ya mtumishi mwadilifu wa Mungu. Yesu aliwapenda na kuwahudumia watu bila ya kujibakiza, lakini hatima yake, akaonja usaliti na hata kukimbiwa na wale aliowapenda na kuwahudumia. Kristo Yesu alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu. Huduma ya upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumapili ya Matawi, tarehe 5 Aprili 2020 ni mwanzo wa maadhimisho ya Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Jumapili ya Matawi, Kanisa linaadhimisha Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwengu katika ngazi ya kijimbo. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Mwaka 2020 unaongozwa na kauli mbiu “Kijana, nakuambia: Inuka.” Lk. 7:14.  Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kufanya tafakari ya kina kuhusu: uwezo wa kuona maumivu na kifo; vijana wawe na moyo wa huruma; waoneshe ujasiri wa kujongea mbele na kugusa, vijana wajitanabaishe na yule kijana ambaye alifufuliwa na Kristo Yesu, kwa kuinuka na kuanza kuishi maisha mapya kama watu waliofufuliwa!

Vijana wakumbushwa kuhusu Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyofanyika mwezi Oktoba 2018 mjini Vatican, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito. Kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, hakukufanyika maandamano makubwa kama ilivyokuwa imezoeleka na badala yake, Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, huku ikihudhuhuriwa na watu wachache sana. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekazia kuhusu dhana ya mtumishi mwadilifu wa Mungu. Kristo Yesu aliwapenda na kuwahudumia watu bila ya kujibakiza, lakini hatima yake, akaonja usaliti na hata kukimbiwa na wale aliowapenda na kuwahudumia. Kristo Yesu alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu.

Kristo Yesu, Mtumishi mwadilifu na mwaminifu wa Mungu, ndiye yule Siku ya Alhamisi kuu, aliyewaosha Mitume miguu na Ijumaa kuu anawekwa mbele ya macho ya imani kama Mtumishi wa Bwana, anayetegemezwa na Mwenyezi Mungu ambaye amewakomboa wanadamu kwa njia ya huduma. Mara nyingi inadhaniwa kwamba, mwanadamu ndiye anayemhudumia Mwenyezi Mungu, lakini ukweli wa mambo ni kwamba, Mungu ndiye anayewahudumia kwa sababu ndiye alianza kuwapenda. Ni vigumu sana kuhudumia ikiwa kama mwanadamu hatatengeneza mazingira ya kuhudumiwa na Mungu. Kristo Yesu amewahudumia wanadamu kwa kuyamimina maisha yake, kwa sababu alipenda upeo, kiasi cha kusadaka maisha yake! Hili ni jambo ambalo linawacha watu wengi wakiwa wameshikwa na bumbuwazi.

Baba Mtakatifu anaendelea kudadavua kwamba, Mwenyezi Mungu amemkomboa mwanadamu kwa kujitwisha dhambi zake, bila kujitetea hata kidogo, bali akaonesha uvumilivu na utii kama Mtumishi mwaminifu na mwadilifu; aliyeyatekeleza yote haya kwa nguvu ya upendo. Mungu Baba, akaenzi huduma iliyokuwa ikitolewa na Kristo Yesu, akaonja mateso na hatimaye kuibuka kidedea kwa kutenda mema, kwa kukita mizizi yake katika upendo mkamilifu. Kristo Yesu aliwapenda waja wake, kiasi hata cha kuonja usaliti na hata kukimbiwa na wafuasi wake. Aliuzwa kwa vipande thelathini vya fedha na baadhi ya wanafunzi wake wakamkana; akasalitiwa na watu aliokuwa anawahudumia, wao wakamgeuzia kibao na kuanza kupiga kelele “Asulubiwe”. Alisalitiwa na taasisi ya kidini iliyomhukumu kinyume cha haki pamoja na taasisi ya kisiasa iliyonawa mikono.

Hata leo hii anasema Baba Mtakatifu Francisko bado kuna usaliti mkubwa katika maisha kwa kutokuaminiana pamoja na udanganyifu unaoibuka kutoka katika sakafu ya moyo wa mtu. Yote haya yanatendeka kwa sababu mwanadamu ameumbwa kwa ajili ya kupenda ili aweze kupenda. Inasikitisha sana moyoni ikiwa kama usaliti unafanywa kwa uhakika na mtu ambaye yuko karibu nawe. Usaliti huu mbele ya Mwenyezi Mungu ulikuwa ni mkubwa sana kwa sababu Mungu ni upendo. Waamini wanaalikwa kuchunguza dhamiri zao na kuangalia ikiwa kama kweli ni waaminifu. Kwa bahati mbaya maisha ya mwanadamu yamesheheni uwongo, unafiki na undumila kuwili, kiasi hata cha kusaliti nia njema; kutoweza kutekeleza ahadi wala kutumia fursa zinaoijitokeza. Mwenyezi Mungu anawatambua fika waja wake kuliko wao wenyewe wanavyo jitambua, kwa sababu ni dhaifu kiasi kwamba, hawana mwendelezo wa maisha; wanaanguka, lakini si rahisi sana kuweza kusimama na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu na kwamba, wakati mwingine si rahisi sana kuganga na kuponya baadhi ya madonda.

Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, amekuja kuwakomboa watu wake kwa kuwaponya kutokana na kushindwa kuwa waaminifu, ili aweze kuwapenda upeo pamoja na kuwaondolea usaliti wao. Huu ni wakati wa kuinua kichwa na kumwangalia Kristo Msalabani, ili aweze kuwakumbatia! Waamini wawe tayari kumshirikisha Kristo Yesu, hali yao ya ukosefu wa uaminifu, ili Kristo Yesu aweze kuwakumbatia na kuwahudumia kwa upendo sanjari na kuwatia shime. Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu alipokuwa juu Msalabani, alilia kwa sauti kuu “Eloi Eloi, lama sabakthan? Yaani: “Mungu wangu, Mungu wangu mbona umeniacha?. Hata katika hali ya mateso na uchungu mkubwa, Kristo Yesu alibaki akiwa ameungana na Baba yake wa mbinguni! Sala inayouliza swali la msingi, Je, hata wewe Mungu Baba umeniacha? Kwa hakika Kristo Yesu alionja usaliti mkubwa na kukimbiwa na wanafunzi wake kama inavyoshuhudiwa kwenye Maandiko Mtakatifu kwa kuweka maneno asili ya Kristo Yesu “Eloi Eloi, lama sabakthan? Yote haya yametendeka kwa ajili ya kumhudumia mwanadamu.

Katika hali ya majonzi na kukata tamaa ya maisha; pale mwanadamu anapotumbukia katika giza nene na wala asiwe na upenyo wa kutokea; pale anapodhani kwamba, Mwenyezi Mungu hamsikilizi na wala hawezi kujibu sala na kilio chake; lakini mwanadamu daima anakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu yupo daima katika maisha yake. Kristo Yesu ameonja usaliti mkubwa na hali ya kukimbiwa ili kuwaonjesha waja wake mshikamano wa dhati pamoja na kuwatia shime, huku wakitambua kwamba, Kristo Yesu anatembea nao bega kwa bega. Amezama katika lindi la mateso na mahangaiko ya binadamu, wakati wa mauaji ya kimbari, usaliti na hata kukimbiwa. Leo hii ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni changamoto inayowatesa watu wengi duniani: kwa kukosa kuwa na uhakika wa maisha kwa siku za usoni; kuna matumaini ambayo yamesalitiwa; pamoja na mambo yote haya, lakini Kristo Yesu anapenda kuwakaribisha moyoni mwake, ili kuonja upendo wake usiokuwa na kifani; kiasi cha kusijikia faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu anaye waenzi!

Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutojitumbukiza katika kishawishi cha kumsaliti Mungu, kwa sababu wameumbwa ili kupendwa na kupenda: Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza na pili ni jirani, kwani mengine yote yatapita na kutoweka, lakini upendo utadumu daima. Kipeo cha Virusi vya Corona, COVID-19 ni fursa ya kufanya maamuzi machungu kwa kuzingatia mambo msingi, ili kutambua kwamba, maisha hayana maana, ikiwa kama si kwa ajili ya huduma. Hii inatokana na ukweli kwamba, maisha yanapimwa kwa njia ya upendo. Msalaba ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa binadamu. Mbele ya Mwenyezi Mungu anayewahudumia wanadamu, kiasi cha kuyamimina maisha yake, awasaidie watu wa Mungu kuishi ili wahudumie. Wawe na ujasiri wa kuwaendea na kuwasaidia kadiri ya uwezo wao: watu wanaoteseka, walio pweke na wahitaji zaidi. Watu wasijifikirie wao wenyewe kwa kutafuta yale mambo ambayo wamepungukiwa, bali wajizatiti kutafuta mambo yale wanayoweza kutekeleza.

Mwenyezi Mungu alimtegemeza Kristo Yesu katika Mateso yake na anawatia shime waamini kujenga na kudumisha moyo wa huduma. Pamoja na kuendelea kujikita katika upendo, maisha ya sala, msamaha pamoja na huduma ndani ya familia na jamii katika ujumla wake. Mchakato huu unaweza kuonekana kana kwamba, ni Njia ya Msalaba, lakini hii ndiyo Njia ya Huduma ambayo Kristo Yesu ameitumia kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anataka ujumbe huu wa huduma uzame na kuota mizizi katika maisha ya vijana wa kizazi kipya, wanapoadhimisha Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwenguni, inayoadhimisha na Mama Kanisa katika ngazi ya kijimbo. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kuwaangalia mashujaa wa kweli, ambao wanaendelea kujipambanua kila kukicha. Hawa si watu maarufu wala “vigogo”, hawana fedha wala “vijisenti vya mboga”, ni watu wa kawaida ambao hawana mafanikio makubwa katika maisha, lakini wamejisadaka kwa ajili ya huduma kwa wengine. Vijana wasiogope kusadaka maisha yao kwa ajili ya Mungu na jirani zao, kwani inalipa! Kwa sababu maisha ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu yanayopokelewa kwa kuyasadaka. Furaha kubwa kupita zote ni kupenda bila masharti kama alivyofanya Kristo Yesu, kwa waja wake!

Papa: Jumapili ya Matawi
05 April 2020, 14:27