Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Jumapili ya Huruma ya Mungu na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000. Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Jumapili ya Huruma ya Mungu na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000. 

Papa Francisko: Mahubiri: Jumapili ya Huruma ya Mungu 2020

Huruma ya Mungu daima ni aminifu na inasimikwa katika uvumilivu, chemchemi ya ufufuko wa Mitume wa Yesu, waliomkana na kumkimbia wakati wa mateso na kifo chake Msalabani. Waamini wanaalikwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Madonda yake Matakatifu, ili Kristo Mfufuka aweze kuwaimarisha katika imani kama ilivyokuwa kwa Tomaso!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 23 Aprili 1995, Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea na kusali kwenye Kanisa la “Santo Spirito in Sassia”, yaani miaka 20 iliyopita. Hapa ni mahali ambapo mwaka 1994 Kardinali Camillo Ruini, Makamu wa Askofu Jimbo kuu la Roma kwa wakati ule, alikuwa ameanzisha Kituo cha Tasaufi ya Huruma ya Mungu. Baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Papa Yohane Paulo II akabariki Picha ya Huruma ya Mungu inayoheshimiwa Kanisani humo. Maadhimisho haya ni sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Mtakatifu Maria Faustina Kowalska alipotangazwa kuwa Mtakatifu na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 30 Aprili 2000. Hii ni kumbukumbu ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Jumapili ya Huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 19 Aprili 2020 ameadhimisha kumbukumbu ya matukio yote haya kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la“Santo Spirito in Sassia” liliko hatua chache kutoka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Huruma ya Mungu daima ni aminifu na inasimikwa katika uvumilivu, chemchemi ya ufufuko wa Mitume wa Yesu, waliomkana na kumkimbia wakati wa mateso na kifo chake Msalabani. Waamini wanaalikwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Madonda yake Matakatifu, ili Kristo Mfufuka aweze kuwaimarisha katika imani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Tomaso, Mtume, kielelezo cha wakristo wanaohangaika katika imani yao! Huruma ya Mungu na maisha ya Jumuiya ya kwanza ya Wakristo ni kati ya mambo msingi yaliyoguswa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake. Baba Mtakatifu anasema, Jumapili ya Pasaka, Kanisa limeadhimisha Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Jumapili ya Huruma ya Mungu ni ufufuko wa Mitume wa Yesu kutoka katika hofu, woga na mashaka yaliyowafanya kujifungia ndani kwa kuogopa “kipigo cha Wayahudi”.

Mitume bado walikuwa na mashaka kuhusu Ufufuko wa Kristo kwa wafu. Katika kipindi hiki cha patashika nguo kuchanika, Mtakatifu Tomaso, Mtume, hakuwepo, kwani waswahili wanasema “eti alikua ametokomea mahali pasipojulikana”. Katika muktadha huu, Kristo Mfufu anawatokea wanafunzi wake, milango ikiwa imefungwa kwa hofu ya Wayahudi na kusimama kati kati yao na kuwaambia “Amani iwe kwenu”. Huu ni mwanzo wa huruma ya Mungu ambayo daima ni aminifu na inasimikwa katika uvumilivu. Mwenyezi Mungu kamwe hachoki kuwanyooshea mikono yake, ili kuwasimamisha tena wale walioteleza na kuanguka. Waamini wanapaswa kumwangalia Mwenyezi Mungu kama Baba mwenye huruma. Anatambua fika uwepo wa dhambi na udhaifu wa moyo unaomwangusha mara kwa mara mwanadamu katika udhaifu wake. Mwenyezi Mungu anaweza kuwainua tena waja wake kwa mkono wa huruma, kwani bila huruma yake, mwanadamu hawezi kufua dafu wala kusimama kwa miguu yake mwenyewe!

Mwanadamu katika hija yake ya maisha, daima ataendelea kuteleza na kuanguka, lakini huruma ya Mungu itamshika mkono na kumwinua tena. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anawaangalia watoto wake walioanguka na kumezwa na malimwengu, lakini anawaangalia kwa jicho la huruma, ili waweze kusimama tena na kusonga mbele! Mwenyezi Mungu anawapenda watoto wake kwa upendo wenye huruma. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa la “Santo Spirito in Sassia” kwa sasa limegeuka kuwa ni Madhabahu ya Huruma ya Mungu, Jimbo kuu la Roma. Hii ni kumbu kumbu endelevu katika historia na maisha ya Kanisa, kwa Mtakatifu Yohane Paulo II kuanzisha Jumapili ya Huruma ya Mungu, miaka ishirini iliyopita. Mwaliko kwa waamini ni kuupokea ujumbe wa huruma ya Mungu kwa imani na matumaini makubwa kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Maria Faustina Kowalska alipoambiwa kwamba, Kristo Yesu ni upendo na huruma; na wala hakuna dhambi kubwa kiasi gani inayoweza kushinda huruma ya Mungu.

Hii ni huruma inayonafsishwa katika sadaka na majitoleo bila ya kujibakiza hata kidogo. Kristo Yesu anawataka waamini kusadaka dhambi na udhaifu wao wa moyo; kwa kumwonesha jinsi ambavyo wameteleza na kuanguka dhambini. Kristo Yesu anawataka watubu na kumwongokea kwa kuacha dhambi; kwa kuondokana na makovu ya majeraha yaliyopita; kwa kuondoa chuki na hasira dhidi ya jirani zao pamoja na hali ya kuwadhania wengine vibaya! Kristo Yesu anaendelea kuwasubiri waja wake, ili wamwendee na kumpelekea dhambi na udhaifu wa moyo, tayari kugundua chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani! Baba Mtakatifu amerejea tena kwa Mitume wa Yesu waliomkana na kumkimbia wakati wa mateso na kifo chake Msalabani! Walisutwa sana na dhamiri zao, wakapata madonda makubwa ndani mwao, lakini Kristo Mfufuka alipowatokea, akawaonesha Madonda yake Matakatifu. Tomaso, asiye amini na aliyekuwa “ametokomea kusikojulikana” akagusa na kugundua chemchemi ya upendo iliyokuwa inabubujika kutoka katika mateso na kifo cha Kristo Msalabani.

Mtume Tomaso aliyekuwa amechelewa, lakini anapokumbatia huruma ya Mungu, anakuwa wa kwanza na hivyo kuwapita Mitume wengine wote. Anakiri na kuungamana imani katika Fumbo la Ufufuko na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa kusema “Bwana wangu na Mungu wangu”. Huu ndio ufufuo wa Mtume anayetambua dhambi na udhaifu wake wa moyo unaopenya na kuingia ndani ya Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu. Hofu na mashaka yakatoweka na Mwenyezi Mungu akawa ni “Mungu wangu”. Huu ni mwanzo wa Mtume kujikubali jinsi alivyo na kuanza kujipokea, kiasi hata cha kuyapenda maisha yake! Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha watu wa Mungu kwamba, janga kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni jambo linalowatumbukiza watu wengi katika hofu na mashaka kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Tomaso. Mwanadamu amenyong’onyea sana na kwa hakika anahitaji uwepo wa Mungu anayeangalia uzuri wake, licha ya udhaifu wake wa kibinadamu. Mwanadamu ni dhaifu sana, lakini anayo thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mwanga wa huruma ya Mungu kwa njia yao, unaendelea kung’ara ulimwenguni. Mtakatifu Petro anasema: “mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa kwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbali mbali” (1Pet. 1:6). Ujumbe wa Sherehe ya Huruma ya Mungu unatangazwa kwa kuchelewa kutokana na kutokuwepo kwa Mtakatifu Tomaso, lakini, Kristo Yesu, mwingi wa huruma na mapendo, anamsubiri, kwa sababu huruma ya Mungu, kamwe haiwezi kumwacha mtu nyuma! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, hakuna kirusi kibaya sana ulimwenguni kama cha ubinafsi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Wengi wanatamani mambo yaende vyema, ikiwa kama yanawanyookea wao binafsi. Huu ndio mwanzo wa ubaguzi kwa kuwakumbatia matajiri na kuwatelekeza maskini na wale wanaosua sua katika kiwango cha maendeleo. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 ni changamoto inayowakumbusha walimwengu kwamba, ugonjwa huu haubagui wala kuweka ukuta kati ya mgonjwa na mtu mzima!

Binadamu wote ni sawa na ni dhaifu lakini wote wana thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Huu ni wakati wa kung’oa vitendo vyote vinavyosababisha mifumo mbali mbali ya ubaguzi; ni wakati muafaka wa kutakasa vitendo vyote vinavyopelekea uvunjifu wa haki msingi za binadamu zinazohatarisha afya ya familia nzima ya binadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka katika Jumuiya ya Kwanza ya Wakristo kama inavyoshuhudiwa kwenye Kitabu cha Mtendo ya Mitume. Ni waamini waliojiaminisha kwenye huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Hii ni Jumuiya iliyosimikwa kwenye mihimili mikuu minne yaani: Fundisho la Mitume, Ushirika, Adhimisho ya Ekaristi Takatifu na Maisha ya Sala. Katika Jumuiya ile, Mtume Tomaso peke yake, ndiye aliyekuwa amebaki nyuma, akichechemea! Sehemu ndogo sana ya familia ya binadamu inaonekana kupiga hatua kubwa ya maendeleo, lakini watu wengi, bado wanasuasua. Hii ni changamoto kwa kila mtu kujifunga kibwebwe ili kuwasaidia na kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kama anavyosema Mtakatifu Maria Faustina Kowalska: waamini wajitahidi kumwona Kristo anayeteseka kati ya jirani zao na wala kamwe wasionekane kama wategemezi. Ni wakati wa kunafsisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu. Watu wawe na huruma na upendo hata kama kuna wakati huruma na upendo hautendewi haki. Ustawi, mafao na ustawi wa wengi, kiwe ni kipaumbele cha kwanza kwa kila mtu! Janga hili liwe ni fursa ya kuibua sera na mbinu mkakati kwa ajili kesho iliyo bora kwa watu wote, bila ya mwelekeo huu ni vigumu sana kuwa na kesho iliyo bora zaidi. Upendo wa Kristo Mfufuka umewafufua Mitume wake. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Tomaso, waamini nao wanapaswa kupokea huruma ya Mungu, chachu ya ujenzi wa ulimwengu mpya!

Papa: Huruma ya Mungu
20 April 2020, 14:38