Papa Francisko: Katekesi Kuhusu Heri za Mlimani: Heri wenye Moyo Safi maana hao watamwona Mwenyezi Mungu Papa Francisko: Katekesi Kuhusu Heri za Mlimani: Heri wenye Moyo Safi maana hao watamwona Mwenyezi Mungu 

Papa Francisko: Heri za Mlimani: Moyo Safi ili kumwona Mungu!

Dhambi inaharibu mwonekano wa maisha ya ndani, inaharibu tathmini na ukweli wa mambo. Kumbe, kuna haja ya kuwa na moyo safi ili kuweza kumwona Mwenyezi Mungu. Moyo ni mahali pa ndani kabisa panapomwonesha mtu jinsi alivyo. Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru, lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hotuba ya Mlimani au Heri za Mlimani ni: dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo. Ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake. Anawataka kwa namna ya pekee: Wawe na huzuni na umaskini wa roho; wawe na njaa na kiu ya haki; wawe na rehema, wenye moyo safi na wapatanishi. Heri nane ni faraja ya Roho Mtakatifu kwa wale ambao wamekombolewa na kuweka nyoyo zao wazi kwa ajili ya kupokea neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, wako huru. Heri za Mlimani ni chemchemi ya furaha ya upendo aminifu wa Mungu unayobubujikia maisha ya waamini! Hii ni furaha endelevu ambayo hakuna mtu wala mazingira yanayoweza kuwapokonya watoto wapendwa wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 1 Aprili 2020 amefafanua kuhusu Heri ya Nane isemayo: Heri wenye moyo safi, maana watamwona Mungu. Mt. 5:8. Na Mzaburi anasema “Nitafuteni uso wangu”, Moyo wangu umekuambia, “Bwana, uso wako nitautafuta”. Zab. 27:8-9. Lugha hii inaonesha kwa namna ya pekee kabisa kiu ya mahusiano na mafungamano binafsi kati ya mwamini na Mwenyezi Mungu! Naye Ayubu katika Kitabu chake anasema, “Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio, bali sasa jicho langu linakuona.” Ayu. 42:5. Baba Mtakatifu anasema, hii ni hija ya maisha inayojenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu.

Kwa bahati mbaya, watu wanaweza kumfahamu Mwenyezi Mungu kwa kuambiwa na kusikia kutoka kwa watu, lakini kwa njia ya mang’amuzi binafsi, waamini wanaweza kusonga mbele, kiasi hata cha kuweza kumfahamu zaidi. Lakini, jambo hili linawezekana tu, ikiwa kama waamini wataendelea kuwa waaminifu, kielelezo cha ukomavu katika roho! Hivi ndivyo ilivyojitokeza kwa wafuasi wa Emau ambao walikuwa wanajadiliana wao kwa wao yale yaliyotokea na ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Kristo Yesu akawakaribia na kuandamana nao. Macho yao yakafungwa wasimtambue! Kristo Yesu aliwafungua macho na kumtambua wakati alipokua anamega mkate. Lakini aliwakemea kwa kutofahamu kwao na kwa kuwa na mioyo mizito ya kuamini! Haya ndiyo mambo msingi yaliyowazuia na hivyo kushindwa kumwona na kumtambua Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anasema, hekima inayolala hapa ya kuweza kumwona Mungu, ni kwamba kuna haja ya kutengeneza mazingira na nafasi katika nyoyo zao. Hii inatokana na ukweli kama anavyosema Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa kwamba, Mwenyezi Mungu yuko ndani ya mtu kuliko hata mtu mwenyewe “Interior intimo meo”. Ili kumwona Mwenyezi Mungu hakuna sababu ya kubadilisha miwani au  mahali pa kuweza kumwangalia; au hata kutafuta wanataalimungu watakaowawezesha waamini kukita miguu yao katika safari hii, bali wanapaswa kuingia katika undani wa maisha yao ili kumtengenezea Mungu nafasi. Hii ndiyo njia pekee iliyoko mbele ya waamini wote. Hiki ni kielelezo cha ukomavu, kwa kumtambua adui ambaye mara nyingi anapenda kujificha ndani ya nyoyo zao. Waamini wawe na ujasiri wa kuanzisha mapambano dhidi ya adui anayewatumbukiza dhambini.

Baba Mtakatifu anasema, dhambi inaharibu mwonekano wa maisha ya ndani, inaharibu tathmini na ukweli wa mambo. Kumbe, kuna haja ya kuwa na moyo safi ili kuweza kumwona Mwenyezi Mungu. Moyo katika lugha ya Biblia ni mahali pa ndani kabisa panapomwonesha mtu jinsi alivyo. Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru, lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Mwenye moyo safi anaishi mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya dhati; katika umoja. Moyo safi ni matokeo ya mchakato wa majitoleo na sadaka unaofikia ukomavu wake kwa njia ya kujifunza; kwa kukataa kutenda maovu!

Huku ndiko lugha ya Biblia inasema kutahiri moyo kwa kutambua dhambi na madhara yake, ili hatimaye, kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza waja wake, ili kuweza kumwona Mwenyezi Mungu. Usafi wa moyo unawawezesha waamini kupenda kwa moyo mnyofu; kwa jicho la unyofu, mwamini anaweza kutekeleza mapenzi ya Mungu. Usafi wa kuona unawasaidia waamini kuwa na nidhamu ya vionjo na mawazo. Mambo yote haya yanamwezesha mwamini kumwona na kumtambua Kristo Yesu katika Sakramenti zake, lakini zaidi kati ya ndugu zake maskini na wahitaji zaidi. Baba Mtakatifu anawataka waamini kukuza kiu ya kutaka kumwona Mungu, kwa kuondokana na mambo yanayoleta uzito katika nyoyo zao. Wawe na ujasiri wa kumruhusu Roho Mtakatifu kutenda kazi ndani mwao, ili aweze kuwatakasa na hatimaye, kuwakirimia furaha na amani ya ndani. Hakuna sababu ya kuogopa kumfungulia Roho Mtakatifu, malango ya nyoyo zao kwa sababu atawasaidia kuwasafisha na kuwatakasa, ili hija ya maisha yao, iweze kupata utimilifu wa furaha ya kweli!

Papa: Heri za Mlimani: Moyo Safi
01 April 2020, 14:13