Tafuta

Vatican News
Ijumaa Kuu 2020: Ibada ya Ijumaa Kuu: Liturujia ya Neno, Kuabudu Msalaba na Liturujia ya Ekaristi Takatifu: Tafakari ya Njia ya Msalaba imetungwa na wafungwa kutoka mjini Padua, Italia. Ijumaa Kuu 2020: Ibada ya Ijumaa Kuu: Liturujia ya Neno, Kuabudu Msalaba na Liturujia ya Ekaristi Takatifu: Tafakari ya Njia ya Msalaba imetungwa na wafungwa kutoka mjini Padua, Italia.  (ANSA)

Papa Francisko: Ijumaa Kuu: Ibada na Njia ya Msalaba 2020: Sauti ya Wafungwa

Liturujia ya Ijumaa kuu imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Liturujia ya Neno la Mungu, Ibada ya Kuabudu Msalaba ambao wokovu wa ulimwengu umetundikwa juu yake na tatu ni Ibada ya Ekaristi Takatifu. Tafakari ya Njia ya Msalaba kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa Mwaka 2020 imetungwa na wafungwa kutoka Padua. Hiki ni kilio cha wafungwa sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa Kuu, tarehe 10 Aprili 2020, kuanzia majira ya Saa 12: 00 Jioni kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 1:00 kwa Saa za Afrika Mashariki, anatarajiwa kuongoza Maadhimisho ya Ibada ya Ijumaa kuu. Hii ni siku ambayo ulimwengu mzima unagubikwa giza la huzuni, majonzi na matumaini, ukikumbuka mateso na kifo cha Kristo Yesu pale juu Msalabani. Ibada hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza ni Liturujia ya Neno. Sehemu ya Pili ni Ibada ya Kuabudu Msalaba ambao ni Altare ya Kwanza ambapo Kristo Yesu aliadhimishia sadaka ya mateso na kifo chake, kwa kuyamimina maisha yake kuwa ni chemchemi ya wokovu na maondoleo ya dhambi. Yesu akiwa ametundikwa Msalabani alichomwa ubavu wake kwa mkuki, hapo ikatoka damu na maji; kielelezo cha Sakramenti za Kanisa. Hivyo kuabudu Msalaba kunafumbata uzito wa matukio na mafundisho makuu ya Kanisa kwani waamini wanamwabudu Kristo Yesu aliyetundika Msalabani! Sehemu ya tatu ni Liturujia ya Ekaristi Takatifu.

Ibada ya Njia ya Msalaba: Kutokana na kipeo cha maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 maadhimisho ya Njia ya Msalaba Ijumaa kuu, yatafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican badala ya kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma kama ilivyokuwa kawaida. Ibada ya Njia ya Msalaba itaanza 3:00 Usiku kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 4:00 kwa Saa za Afrika Mashariki. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso, mahangaiko na matumaini ya wafungwa sehemu mbali mbali za dunia, ameamua kwa dhati kwamba, tafakari ya Ijumaa Kuu, Njia ya Msalaba kwa Mwaka 2020, iandaliwe na wafungwa wanaotumikia adhabu yao kutoka katika magereza mawili yaliyoko mjini Padua, Kaskazini mwa Italia.Lengo la Kanisa ni kutoa sauti kwa watu wasiokuwa na sauti, ili hata wao waweze kusikika. Gereza ni mahali ambapo mtu anaonja unyonge na udhaifu wake wa kibinadamu kwa kunyimwa uhuru. Lakini, hii pia ni fursa ya kuweza kutubu na kumwongokea Mungu, ili baada ya Ijumaa kuu, aweze kufufuka tena.

Baba Mtakatifu anasema, wokovu wa binadamu ni kazi ya umoja na mshikamano inayotekelezwa na Jumuiya ya waamini, kielelezo cha mshikamano wa upendo unaomwilishwa katika haki na huruma. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa tafakari ya Ijumaa kuu imetungwa na wafungwa gerezani. Tafakari hii ina Vituo 14 vya Njia ya Msalaba kadiri ya Mapokeo ya Kanisa. Hii ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti, kielezo cha mapambano kati ya kifo na uhai. Ni wakati wa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake kwani hakuna linaloweza kushindikana mbele ya Mungu, kwani wokovu ni zawadi inayotolewa bure na Mwenyezi Mungu. Katika hali na mazingira haya, Njia ya Msalaba, “Via Crucis”, inageuka kuwa ni Njia ya Mwanga, “Via Lucis”. Kwa mara ya kwanza katika historia, sauti ya wafungwa wasiokuwa na majina inasikika na kuingia katika maskani ya watu sehemu mbali mbali za dunia!

Papa: Ijumaa Kuu 2020
09 April 2020, 15:43