Jimbo kuu la Roma, tarehe 11 Machi 2020 limeitumia siku hii kwa kusali na kufunga. Baba Mtakatifu Francisko ametoa pia sala yake kwa ajili ya kuwaombea watu wa Mungu, Jijini Roma Jimbo kuu la Roma, tarehe 11 Machi 2020 limeitumia siku hii kwa kusali na kufunga. Baba Mtakatifu Francisko ametoa pia sala yake kwa ajili ya kuwaombea watu wa Mungu, Jijini Roma 

Virusi vya Corona, COVID-19: Sala ya Papa kwa ajili ya mji wa Roma

Baba Mtakatifu anapenda kuwaweka wagonjwa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya wagonjwa. Bikira Maria chini ya Msalaba, alijiguswa kwa namna ya pekee na mateso ya Mwanaye mpendwa, Yesu, lakini akabaki thabiti katika imani yake. Bikira Maria wokovu wa watu wa Mungu mjini Roma, anatambua fika mahitaji ya watoto wake kwa wakati huu. Wana imani na B. Maria.

Na Padre Richard Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza wafanyakazi wote katika sekta ya afya wanaowahudumia wagonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19, viongozi wa serikali na wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kuhakikisha kwamba wanadhibiti kikamilifu kuenea kwa ugonjwa huu ambao unaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Imani, matumaini na mapendo ni silaha kubwa katika kipindi hiki cha ukame wa maisha ya kiroho. Kwaresima ni kipindi kilichokubalika kwa waamini kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wagonjwa ambao wanashindwa kupata huduma na msaada kutokana na sababu mbali mbali. Huu ni wakati uliokubalika wa kumwilisha huruma na upendo kama ushuhuda wa mshikamano, kielelezo makini cha imani tendaji kwa kujiweza chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu. Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, Jumatano, tarehe 11 Machi 2020, majira ya saa 1:00 Usiku kwa saa za Ulaya, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea Jiji la Roma na Italia katika ujumla wake, dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa “Divino Amore” yaliyoko Jimbo kuu la Roma. Hii ilikuwa ni siku ya kusali na kufunga, ili kuomba huruma ya Mungu kwa ajili ya waathirika. Baba Mtakatifu Francisko  katika sala yake kwa njia ya video kama kielelezo cha uwepo wake wa karibu kiroho kwa waathirika wa Virusi vya Corona, CODIV-19 amemshukuru Bikira Maria nyota ang’avu katika mapito ya waamini; alama ya wokovu na matumaini. Baba Mtakatifu anapenda kuwaweka wagonjwa wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya wagonjwa. Bikira Maria chini ya Msalaba, aliguswa kwa namna ya pekee, na mateso ya Mwanaye mpendwa, Kristo Yesu, lakini akabaki thabiti katika imani yake. Bikira Maria wokovu wa watu wa Mungu mjini Roma, anatambua fika mahitaji ya watoto wake kwa wakati huu. Watu wa Mungu wanayo imani kubwa kwamba, kama ilivyokuwa kwenye Arusi ya Kana ya Galilaya, atawawezesha watu wa Mungu mjini Roma na Italia katika ujumla wake, kuwa tena na furaha na hivyo kusherekea zawadi ya maisha baada ya kipindi hiki kigumu cha majaribu. 

Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria, kielelezo cha upendo wa Mungu kuwasaidia ili waweze kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yao na kufanya yale yote wanayo ambiwa na Kristo Yesu, ambaye amejitwika mateso na mahangaiko ya binadamu, ili kwa njia ya Fumbo la Msalaba, aweze kuwafikisha katika ufufuko na maisha ya uzima wa milele. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1944 Papa Pio XII alikwenda kusali katika Madhabahu haya ili kuomba ulinzi na tunza ya Bikira Maria dhidi ya mashambulizi ya Kinazi. Miaka 75 baadaye, anasema Baba Mtakatifu Francisko, familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma, inapenda kukimbilia tena ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, ili kuombea afya njema. Kwa Ibada hii ya Misa takatifu, Jimbo kuu la Roma litakuwa limefungua maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu itakayokuwa inarushwa kila siku jioni kupitia Kituo cha Televisheni cha Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI TV2000 pamoja na kusambazwa kwenye mitandao mbali mbali ya kijamii. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa kufunga na hatimaye, kuchangia fedha itakayotumika kwa ajili ya kuwasaidia wahudumu katika sekta ya afya wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na waathirika wa Virusi vya Corona, CODIV-19. Hii ni siku ya mshikamano wa kiroho kwa njia ya sala, kufunga na Ibada ya Misa Takatifu.

Sala ya Papa Francisko

 

12 March 2020, 09:43