Vatican News
Virusi vya Corona, COVID-19: Jimbo kuu la Roma, tarehe 11 Machi 2020 ni Siku ya Kufunga na Kusali kwa ajili ya kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu dhidi ya Corona! Virusi vya Corona, COVID-19: Jimbo kuu la Roma, tarehe 11 Machi 2020 ni Siku ya Kufunga na Kusali kwa ajili ya kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu dhidi ya Corona! 

Virusi vya Corona, COVID-19: Roma:Toba, Kufunga na Kusali, 11 Machi 2020!

Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, Jumatano tarehe 11 Machi 2020, majira ya saa 1:00 Usiku kwa saa za Ulaya, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea Jiji la Roma na Italia katika ujumla wake dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Ibada ya Misa Takatifu itaadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria “Divino Amore”.

Na Padre Richard Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza wafanyakazi wote katika sekta ya afya wanaowahudumia wagonjwa, viongozi wa serikali na wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kuhakikisha kwamba wanadhibiti kikamilifu kuenea kwa ugonjwa huu ambao unaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Imani, matumaini na mapendo ni silaha kubwa! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Kwaresima ni kipindi kilichokubalika kwa waamini kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wagonjwa ambao wanashindwa kupata huduma na msaada kutokana na sababu mbali mbali.

Huu ni wakati uliokubalika wa kumwilisha huruma na upendo kama ushuhuda wa mshikamano, kielelezo makini cha imani tendaji kwa kujiweza chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu. Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, Jumatano, tarehe 11 Machi 2020, majira ya saa 1:00 Usiku kwa saa za Ulaya, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea Jiji la Roma na Italia katika ujumla wake dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Ibada hii ya Misa Takatifu itaadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa “Divino Amore” yaliyoko Jimbo kuu la Roma. Hii ni siku ya kusali na kufunga, ili kuomba huruma ya Mungu kwa ajili ya waathirika.

Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko atatoa ujumbe wake kwa njia ya video, kama kielelezo cha uwepo wake wa karibu kiroho kwa waathirika wa Virusi vya Corona, CODIV-19. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1944 Papa Pio XII alikwenda kusali katika Madhabahu haya ili kuomba ulinzi na tunza ya Bikira Maria dhidi ya mashambulizi ya Kinazi. Miaka 75 baadaye, anasema Baba Mtakatifu Francisko, familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma, inataka kukimbilia tena ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, ili kuombea afya njema.

Kwa Ibada hii ya Misa takatifu, Jimbo kuu la Roma litakuwa limefungua maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu itakayokuwa inarushwa kila siku jioni kupitia Kituo cha Televisheni cha Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI TV2000 pamoja na kusambazwa kwenye mitandao mbali mbali ya kijamii. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa kufunga na hatimaye, kuchangia fedha itakayotumika kwa ajili ya kuwasaidia wahudumu katika sekta ya afya wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na waathirika wa Virusi vya Corona, CODIV-19. Hii ni siku ya mshikamano wa kiroho kwa njia ya sala, kufunga na Ibada ya Misa Takatifu.  

Kardinali De Donatis

 

11 March 2020, 11:22