Tafuta

Itifaki ya kudhibiti ugonjwa wa Virusi vya Corona umeababisha vurugu, ghasia na mauaji katika magereza 27 nchini Italia! Hali kwa sasa ni shwari Itifaki ya kudhibiti ugonjwa wa Virusi vya Corona umeababisha vurugu, ghasia na mauaji katika magereza 27 nchini Italia! Hali kwa sasa ni shwari 

Virusi vya Corona, COVID-19: Ghasia kwenye Magereza ya Italia!

Itifaki ya udhibiti wa Virusi vya Corona, COVID-19 imezua taharuki kubwa kwenye Magereza 27 nchini Italia, kiasi cha kusababisha fujo na ghasia kubwa zilizopelekea watu sita kupoteza maisha, baadhi ya Askari magereza na wahudumu wa sekta ya afya kutekwa nyara; na magereza kuchomwa moto kiasi kwamba, baadhi yake kwa sasa hayafai tena kwa ajili ya huduma za magereza.

Na Padre Richard Mjigwa, - Vatican.

Majukumu ya msingi ya Jeshi la Magereza ni kuwapokea na kuwahifadhi gerezani watu wote wanaoletwa gerezani kwa mujibu wa sheria za nchi na kuendesha programu mbalimbali zenye kulenga kuwarekebisha wafungwa waliohukumiwa ili hatimaye, watoke gerezani wakiwa raia wema. Katika kutekeleza majukumu hayo Jeshi la Magereza linawajibika kufuata na kuheshimu sheria zote za nchi pamoja na sheria mbalimbali za kimataifa zinazohusu haki za binadamu. Kwa upande mwingine, wafungwa wanatakiwa pia kuondokana na misimamo mikali ya kiitikadi, kidini na kiimani ambayo imekuwa wakati mwingine chanzo kikuu cha mateso na mahangiko yao gerezani. Serikali ya Italia kwa kuzingatia itifaki ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19, imeamua kuchukua hatua kadhaa ili kudhibiti kusambaa kwa Virusi vya Corona, COVID-19.

Kati ya hatua hizi kwa upande wa Magereza nchini Italia kuanzia sasa, wafungwa hawataweza tena kukutana mubashara na ndugu zao na badala yake wanashauriwa kutumia simu! Wafungwa kwa upande wao wanaomba kuchunguzwa afya zao dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo kwa sasa vimekuwa ni tishio kubwa nchini Italia, kwa kushika nafasi ya pili kwa maambukizi duniani. Wafungwa wanaitaka Serikali ya Italia kuangalia tena uwezekano wa kupunguza mlundikano wa wafungwa magerezani! Itifaki hii imezua taharuki kubwa kwenye Magereza 27 nchini Italia, kiasi cha kusababisha fujo na ghasia kubwa zilizopelekea watu sita kupoteza maisha, baadhi ya Askari magereza na wahudumu wa sekta ya afya kutekwa nyara; na magereza kuchomwa moto kiasi kwamba, baadhi yake kwa sasa hayafai tena kwa ajili ya huduma za magereza.

Kuna baadhi ya wafungwa wameteka nyara magari na kutokomea kusikojulikana. Ghasia hizi zimedumu kwa takribani saa kumi na hatimaye, vyombo vya ulinzi na usalama vikafanikiwa kuzidhibiti. Takwimu zinaonesha kwamba, magereza nchini Italia yamefurika sana kuliko uwezo wake. Kuna zaidi ya wafungwa 10, 000 kinyume kabisa cha uwezo wa magereza. Kati ya mapendekezo yaliyotolewa na wafungwa ni kuwapatia wafungwa wanaokaribia kumaliza adhabu zao kifungo cha nje. Kufurika kwa wafungwa magerezani nchini Italia ni kati ya changamoto changamani kwa wakati huu, hali ambayo inachangia pia kudhohofisha maisha ya Askari magereza, kiasi hata cha kukosa imani, amani na utulivu wa ndani. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, wafanyakazi na wafungwa wanaishi maisha yenye hadhi na utu wa kibinadamu, vinginevyo, magereza yatageuka kuwa nyumba cha chuki na uhasama badala ya kuwa ni mahali pa kurekebisha tabia na mwenendo wa wafungwa. Baba Mtakatifu Francisko anawataka wadau wa huduma mbali mbali magerezani kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili, tayari kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.

Wanapokumbana na umaskini wa wafungwa magerezani, watambue kwamba, hawa ni watu wanaohitaji kwanza kabisa msamaha na huruma ya Mungu. Wawe na ujasiri wa kusamehe kama mashuhuda waaminifu wa msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu; wawe ni watu wa faraja na kamwe wasimwache mtu hata mmoja kutumbukia katika upweke hasi, unaoweza kusababisha watu kumezwa na utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi magerezani kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuokoa maisha ya wafungwa kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha ya Zakayo Mtoza ushuru. Wawe na ujasiri unaobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao na kamwe, wasiruhusu kugubikwa na giza totoro katika maisha na nyoyo zao. Katika shida na mahangaiko ya ndani, wamkimbilie Kristo Yesu chini ya Msalaba na kumwelezea mahangaiko yao katika ukweli na uwazi. Msalaba ni chemchemi ya ujasiri, amani na utulivu wa ndani. Kamwe wasikubali kuzima utambi wa matumaini katika maisha yao. Hii ni dhamana na wajibu wa watu wote.

Haki, matumaini, upatanisho pamoja na mchakato wa wafungwa kurejea tena katika maisha ya kawaida ndani ya jamii ni mambo msingi yanayotegemeana na kukamilishana. Wadau katika huduma ya wafungwa  magerezani wasikubali kujifungia katika gereza lisilokuwa na matumaini katika maisha. Kila mtu anayo haki ya matumaini  na haki ya kuanza kuandika tena ukurasa wa maisha yake kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema, taswira inayotolewa na magereza sehemu mbali mbali za dunia inaonesha ukweli wa jamii ambamo uchoyo, ubinafsi na utandawazi wa kutoguswa na mahangaiko ya jirani vinatawala. Kuna maamuzi ambayo yamefanywa kisheria lakini yanakiuka utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kujidai kukuza na kutaka kudumisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Matokeo yake ni watu kutengwa na kutupwa magerezani kama suluhu ya matatizo mbali mbali yanayoisonga jamii. Lakini ikumbukwe kwamba, kuna kiasi kikubwa cha rasilimali na utajiri wa nchi unaotumika kwa ajili ya kuwahudumia wafungwa magerezani, ikilinganishwa na kiasi cha fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuchochea kasi ya maendeleo fungamani ya binadamu, ambayo yangewezesha idadi kubwa ya wafungwa kupata kazi na kipato halali badala ya kujiingiza kwenye vitendo vya uvunjaji wa sheria.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni rahisi sana kufumbia macho umuhimu wa elimu na malezi makini kwa jamii, sanjari na kushindwa kuona ukweli halisi wa matatizo na ukosefu wa haki na hivyo suluhu ya haraka inayoweza kupatikana ni ujenzi wa magereza, ili “kuwashikisha adabu wale wote wanaovunja sheria za nchi”. Umefika wakati wa kutoa msukumo wa pekee kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu kwa raia wote. Kwa bahati mbaya, magereza mengi yameshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuweza kutoa mafunzo bora zaidi, ili wafungwa wanapomaliza adhabu zao na kutoka magerezani waweze kuwa ni watu wema zaidi kuliko walivyoingia magerezani. Ni ukweli usioweza kufumbiwa macho kwamba, kuna uhaba mkubwa wa rasilimali fedha na watu ili kukabiliana na changamoto za kijamii, kisaikolojia na kifamilia wanazokabiliana nazo wafungwa magerezani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, magereza yamegeuka kuwa ni mahali hatari sana, ambapo utu na heshima ya binadamu vinasiginwa. Mafunzo makini kwa wafungwa yanaanza pale ambapo wafungwa wanapewa fursa ya kushiriki katika mchakato wa maendeleo, wanapopewa elimu makini na kufanyishwa kazi zenye staha. Yote haya lazima pia yazingatie huduma bora za afya kwa wafungwa pamoja na kuunda mazingira ambayo, wafungwa wataweza pia kushirikiana kwa karibu na raia wengine. Jamii inapaswa kuwa na mwelekeo tofauti sana kwa wafungwa magerezani, kwa kuwapatia msaada wa hali na mali, ili kuboresha maisha yao, kama sehemu ya faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa bahati mbaya sana, wafungwa wamekuwa wakiangaliwa kwa “jicho la kengeza” kiasi kwamba, si rahisi sana kuthamini utu na heshima yao. Wafungwa waonjeshwe matumaini na kupewa tena fursa ya kufanya kazi, ili kujipatia mahitaji yao msingi. Pale ambapo wafungwa baada ya kumaliza adhabu yao wanashindwa kutambuliwa utu na heshima yao, wanajikuta wakiwa kwenye majaribu makubwa kati ya kutafuta fursa za kazi, kutenda uhalifu pamoja na kujenga mazingira yasiokuwa salama. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya waamini kuwaonjesha wafungwa huruma na mapendo, dhamana na utume unaopaswa kutekelezwa na Makanisa mahalia. Kila mwamini awe ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa wafungwa, ili kuiwezesha jamii kukita mizizi yake katika misingi ya haki na amani.

Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema, matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni nyenzo thabiti katika mchakato wa huduma kwa wafungwa magerezani. Huu ni mchakato unaowawezesha watu wa Mungu kutoa huduma kwa wafungwa na hivyo kujenga ndani mwao matumaini. Waamini waendelee kumtambua Kristo Yesu anayejitambulisha kati ya wafungwa magerezani. Baba Mtakatifu anawapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wafungwa pamoja na familia zao, hasa katika kipindi hiki kigumu cha majaribio. Baba Mtakatifu mwishoni anawaombea heri na baraka wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wafungwa magerezani sehemu mbali mbali za dunia, kwani kwa kufanya hivi, wanaendeleza utume ambao Kristo Yesu ameliachia Kanisa lake. Mwishoni mwa maisha yao hapa dunia, wataweza kusikia “Njooni mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu”. Mt. 25:35.

Ghasia Magereza ya Italia

 

10 March 2020, 09:49