Tafuta

Papa Francisko asema, Kanisa linatumia silaha na amana ya utajiri wake wa maisha ya kiroho kupambana na homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Papa Francisko asema, Kanisa linatumia silaha na amana ya utajiri wake wa maisha ya kiroho kupambana na homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. 

Papa Francisko: Vita Dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19!

Katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19, Kanisa linatumia silaha zifuatazo: Kufunga na kusali; Ibada ya Misa Takatifu; Tafakari ya Neno la Mungu; Matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na Rozari Takatifu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia sanjari na kukimbilia faraja na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa kwa miaka ya hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, iliyoambatana na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kutoa baraka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Ijumaa tarehe 27 Machi 2020. Kimya kikuu kilitawala, huku mvua ikinyeesha, Baba Mtakatifu ameongoza sala kwa watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliofuatilia tukio hili kwa njia ya vyombo vya mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii, ili kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika kipindi hiki maalum katika historia ya mwanadamu kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Mama Kanisa anatumia silaha zifuatazo: Kufunga na kusali; Ibada ya Misa Takatifu kwa nia mbali mbali; Tafakari ya Neno la Mungu; Matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na Ibada ya Rozari Takatifu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia ya mwanadamu sanjari na kukimbilia faraja na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ulikuwa tupu, watu wachache sana waliokuwa wanahusika na ulinzi na usalama pamoja na mawasiliano ndio walionekana katika maeneo haya. Jumuiya ya Kimataifa imeingia katika Vita kuu ya Dunia isiyokuwa na mshindi, kwani kila mtu ameguswa na kutikiswa kwa namna yake. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amejikita zaidi katika Injili kama ilivyoandikwa na Marko: 4:35 jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyotuliza dhoruba kali, lakini wanafunzi wake walidhani kwamba alikuwa amelala na wala hakujali kwamba, walikuwa wanaangamia. Lakini Yesu akawakemea kwa sababu walikuwa na imani “haba kama kiatu cha raba”.

Hata katika hali na dhoruba ya maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kuna watu wanadhani kwamba, Yesu amelala na wala hajishughulishi hata kidogo na kusahau kwamba, daima anawajali na kuwasumbukia waja wake; anawaokoa na kuwarejeshea tena imani na matumaini ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Hii ni changamoto ya kurejea tena kwenye mambo msingi ya imani na maisha kwa kuondokana na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka, vita na kinzani pamoja na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Ni muda muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani, kwa kuzingatia na kuambata mambo msingi katika maisha. Ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki zao msingi. Huu ni wakati wa kuwashukuru madaktari, wauguzi, wafanyakazi katika sekta ya afya, vikosi vya ulinzi na usalama, watu wa kujitolea, mapadre na watawa wanaoendelea kusadaka maisha yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni wakati wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa watu wa Mungu!

Sala inayomwilishwa katika huduma ya upendo ni silaha madhubuti katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Hiki ni kipindi ambacho mwanadamu amegundua udhaifu wake! Kumbe, anapaswa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa kuonesha mshikamano wa upendo ili kukabiliana na dhoruba hii. Ni wakati wa kupyaisha imani katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, kwani ukombozi wa mwanadamu umefumbatwa juu ya Msalaba, chemchemi ya: imani, matumaini, nguvu na ujasiri wa kusonga mbele bila kugubikwa na woga unaosababisha taharuki kwa watu wa Mungu. Bikira Maria, Mama wa Mungu na afya ya wagonjwa kwa maombezi na tunza yake ya kimama asaidie kutuliza dhoruba mbali mbali zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo! Hakuna sababu ya kuogopa na kukataa tamaa! Kristo Yesu, anaongoza Jahazi hadi bandari salama!

Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza waamini kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19, Vatican imenunua vifaa 30 vya kupumulia, ili kuchangia juhudi za kuokoa maisha ya watu wanaopambana na kifo kwa kukosa vifaa hivi! Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka mkuu wa Kipapa ndiye aliyekabidhiwa dhamana na jukumu hili. Majimbo na vyama mbali mbali vya kitume, vimefungua malango ya majengo yake ili yatumike kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Majimbo yameunda vikosi kazi kwa ajili ya kuwasaidia wazee na maskini wanaotunzwa kwenye nyumba za wazee na watoto yatima, bila kuwasahau watu wasiokuwa na makazi maalum! Mama Kanisa amekuwa ni kimbilio kwa watu kama hawa! Lengo ni kujenga na kudumisha mshikamno wa upendo, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai katika kipindi hiki cha dhoruba kali ya Virusi vya Corona.

Tangu mlipuko wa Virusi vya Corona, COVID-19 kutokea sehemu mbali mbali za dunia na kusababisha Makanisa kufungwa na hivyo waamini kukosa Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu ameendelea kusali kwa nia mbali mbali kwa ajili ya kuwaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na Virusi vya Corona. Amekuwa akitoa tafakari kila siku asubuhi kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican; Ibada ambazo zimekuwa zikirushwa moja kwa moja na vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii inayomilikiwa na kuongozwa na Vatican. Juhudi hizi zinaendelezwa pia na Makanisa mahalia. Huu ni wakati wa kusali kutoka katika undani wa maisha ya waamini kwa kusaidiwa na vyombo vya mawasiliano ya jamii! Katika kipindi hiki cha dhoruba kali ya maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Mama Kanisa amefungua hazina yake, thamani isiyokuwa na mipaka wala ukomo, yenye malipo na mastahili ya Kristo Yesu, mbele ya Mwenyezi Mungu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hatimaye, aweze kupata maisha na uzima wa milele.

Katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19, Kanisa linatoa Rehema kamili kwa waamini watakaojiandaa na kufuata masharti yaliyowekwa na Kanisa. Kwa ufupi hizi ndizo silaha ambazo Mama Kanisa anazitumia katika mapambano ya vita dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hapa ushuhuda wa kila mwamini ni muhimu sana kama kielelezo cha imani tendaji!

Papa: Mchango wa Kanisa

 

 

28 March 2020, 11:29