Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujiunga naye Ijumaa tarehe 27 Machi 2020 ili kukimbilia huruma na upendo wa Mungu dhidi ya Virusi vya Corona. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujiunga naye Ijumaa tarehe 27 Machi 2020 ili kukimbilia huruma na upendo wa Mungu dhidi ya Virusi vya Corona. 

Ungana na Papa Francisko: 27 Machi 2020: Kuomba Huruma ya Mungu dhidi ya Virusi vya Corona

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye kwa imani na matumaini, ili kukimbilia huruma ya Mungu dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo vimekwisha kusababisha maafa makubwa na taharuki kubwa kwa watu sehemu mbali mbali za dunia! Ni kipindi cha Sala!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ijumaa tarehe 27 Machi 2020, Saa 12:00 za Jioni kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 2: 00 Usiku kwa Saa za Afrika mashariki, Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuongoza Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu kutoka katika Injili kama ilivyoandikwa na Marko 4: 35-41 na baadaye kufuatiwa na Tafakari ya Neno la Mungu. Sehemu ya Pili ya Ibada hii ni Kuabudu Ekaristi Takatifu iatakayofuatiwa na baraka ya Sakramenti kuu ya Ekaristi Takatifu kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake yaani “Urbi et Orbi”. Katika kipindi hiki, Baba Mtakatifu atatoa Rehema kamili kwa waamini waliojiandaa barabara na kutimiza masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa. Rehema hii inatolewa kwa waamini ambao wamewekewa karantini wakiwa hospitalini au majumbani mwao. Ikiwa kama kutoka katika undani wa mioyo yao wataweza kutubu na hatimaye, kujiunga na vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Kwa kusali Rozari Takatifu, Kufanya Njia ya Msalaba au kuhudhuria Ibada nyingine zinazotolewa na Mama Kanisa. Wajitahidi walau kusali: Kanuni ya Imani, Baba Yetu na Salam Maria kwa kutolea mahangaiko yao kwa Mwenyezi Mungu katika imani na upendo kwa jirani zao, kama njia ya kutimiza malipizi ya dhambi zao pamoja na kusali kwa njia za Baba Mtakatifu, pale itakapowezekana.

Rehema hii inatolewa pia kwa wafanyakazi katika sekta ya afya na wanafamilia wote wanaowahudumia wagonjwa kwa kufuata mfano wa Msamaria mwema. Rehema hii inatolewa kwa waamini watakaoweza pia kuabudu Ekaristi Takatifu, watakaoweza kusoma walau Neno la Mungu kwa muda wa nusu saa, au kusali Rozari, kufanya Njia ya Msalaba au kusali Rozari ya Huruma ya Mungu, ili kuomba huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka, ili kuwaondolea watoto wake balaa la ugonjwa huu wa Virusi vya Corona, COVID-19. Mama Kanisa anaendelea kusali kwa ajili ya waamini ambao hawataweza kupata fursa ya kupokea Mpako wa Wagonjwa, kwa kuwaweka chini ya huruma ya Mungu, nguvu na umoja wa watakatifu, ili hatimaye, waweze kupokea fumbo la kifo kwa amani na utulivu wa ndani. Kanisa linakimbilia ulinzi wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na wa Kanisa, Afya ya wagonjwa likiomba tunza yake ya kimama, ili kuwaombea watoto wake wote ili waweze kupona dhidi ya ugonjwa huu.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa namna ya pekee kabisa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaoendelea kufunga na kusali kwa ajili ya kuomba huruma ya Mungu dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 bila kujali, dini, imani na mapokeo yao. Sala hii ya pamoja kwa watu wa Mungu inapatikana kwa kufuata #PrayForTheWorld. Mwenyezi Mungu awaangalie waja wake kwa jicho la huruma na kuwasaidia katika kipindi hiki kigumu, kumwilisha huruma na upendo, kama kielelezo cha uwepo wa karibu kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na ugonjwa huu hatari. Njia za mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii, iwasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwafikia wale wote wanaoteseka kutokana na ugonjwa huu. Baba Mtakatifu anasema, hiki ni kipindi cha kuonesha umoja, upendo na mshikamano kwa kujikita katika huruma na wema. Umoja na mshikamano huu uonekane kwa wale wote walioathirika.

Mama Kanisa anapenda kuwa karibu zaidi na madaktari, wafanyakazi katika sekta ya afya, wauguzi pamoja na watu wa kujitolea. Umoja huu uwaguse hata viongozi wenye mamlaka mbali mbali, wanaoweka sera na mikakati kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Umoja huu uwe ni kielelezo cha mshikamano na vikosi vya ulinzi na usalama, vinavyosimamia ulinzi na usalama wa watu na mali zao pamoja na kutekeleza sera na mikakati ya kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

27 March 2020, 14:12