Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema, toba na wongofu wa ndani ni changamoto endelevu katika wito, maisha na utume wa kitawa! Baba Mtakatifu Francisko anasema, toba na wongofu wa ndani ni changamoto endelevu katika wito, maisha na utume wa kitawa!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Toba na wongofu wa ndani ni changamoto endelevu!

Shirikisho hili kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za Kanisa kwa sasa ni jipya, kwa kuzingatia umoja uliotekelezwa kunako mwaka 2014. Hija hii ya toba na wongofu wa ndani haina budi kuendelezwa, kwa kujiaminisha ili kupata msaada wa Mungu. Vongozi wanapaswa kutekeleza kwa dhati Katiba, kwa kufanya mang’amuzi yanayowahusisha viongozi wote hadi kuwafikia wanachama binafsi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 29 Februari 2020 katika ujumbe aliowaandikia washiriki wa mkutano mkuu wa Shirika la “Legionari di Cristo” pamoja na Jumuiya ya Kimataifa ya watawa na waamini walei wa Ufalme wa Kristo, “Regnum Christi! Amewataka kujizatiti zaidi katika kuendeleza mchakato wa upyaisho wa maisha yao ya kiroho, kwa kuzingatia kashfa kubwa iliyosababishwa na Muasisi wa Shirika hili Padre Marcial Maciel Degollado. Ingawa kihistoria ni muasisi, lakini si mfano bora wa kuigwa katika utakatifu wa maisha kutokana na ukweli kwamba, maisha yake yaligubikwa na vivuli vya utata katika maisha! Karama ya kuanzisha Shirika ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa iliyozingatia sheria, kanuni na taratibu za Kanisa, lakini utekelezaji wake uliacha ukakasi mkubwa katika masuala ya uongozi na maisha ya watu katika ujumla wake

Kanisa kama Mama na Mwalimu kwa kugundua udhaifu huu, lilijitokeza hadharani ili kurekebisha hali hiyo, kwa kuwatumia watu waliobarikiwa kuwa na tunu bora za kiutu, kichungaji na kisheria na matokeo yake ni kuandikwa kwa Katiba mpya ya Shirika mintarafu mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu maisha ya kuwekwa wakfu. Kazi hii ya miaka mitatu, imesaidia kurekebisha mawazo ya watu na hivyo kuanza kujikita katika toba na wongofu wa ndani. Yote haya yamewezekana kwa sababu wanashirika walijivika fadhila ya unyenyekevu na kuanza kutekeleza maagizo na ushauri uliotolewa na Mama Kanisa, kiasi hata cha kuweza kutoka katika dimbwi la ubinafsi walimokuwa wamezamishwa kwa miaka mingi!

Baba Mtakatifu anawapongeza kwa sababu, wamekuwa wazi kwa kazi ya Roho Mtakatifu na hivyo kuanza mchakato wa mang’amuzi, huku wakiwa wanasindikizwa na Mama Kanisa, katika hali ya uvumilivu na uwajibikaji mkubwa. Wakaweza kuvuka vikwazo, kinzani na mipasuko mikubwa iliyokuwa inajitokeza, ili kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano kati ya wanachama mbali mbali wa Ufalme wa Kristo “Regnum Christi”. Huu ni wakati wa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi ndani mwao, kwa kuondokana na uchoyo pamoja na ubinafsi, ili kujielekeza zaidi katika kutafuta na hatimaye, kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima!

Kazi hii kubwa ya kuunda Shirikisho la Wanachama wa Ufalme wa Kristo linaloundwa na Taasisi ya kitawa ya “Legione di Cristo”, Wanachama wa Shirika la Kazi za Kitume pamoja na Waamini walei waliojiweka wakfu kwa ajili ya Ufalme wa Kristo. Katika kundi hili wamo pia waamini walei wanaojiweka wakfu kutekeleza mashauri ya Kiinjili yaani: nadhiri ya utii, ufukara na usafi kamili. Shirikisho hili kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za Kanisa kwa sasa ni jipya kabisa, kwa kuzingatia umoja uliotekelezwa kunako mwaka 2014. Hija hii ya toba na wongofu wa ndani haina budi kuendelezwa, kwa kujiaminisha ili kupata msaada wa Mungu.

Dhana hii inawataka viongozi wa Shirikisho hili kutekeleza kwa dhati Katiba, kwa kufanya mang’amuzi yanayowahusisha viongozi wote hadi kuwafikia wanachama binafsi. Mang’amuzi haya yanahitaji kwa namna ya pekee kabisa: fadhila ya unyenyekevu na moyo wa sala unaorutubishwa na tafakari ya kina kuhusu Mafumbo ya Maisha ya Kristo Yesu. Daima viongozi wajitahidi kutenda katika umoja wa urika wao, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Shirikisho zima! Viongozi wakuu wapya na washauri wao, wasaidiane kutekeleza vyema dhamana na wajibu, kwa kutambua kwamba, wanawaongoza watu kwa kuzingatia Sheria za Kanisa na zile za Shirikisho katika ujumla wake. Viongozi wakuu wa Shirikisho watekeleze kwa dhati maamuzi yanayohitaji ushauri kisheria kabla ya kusonga mbele!

Mchakato wa upyaisho wa mawazo na mwono unahitaji muda mrefu ili kuweza kukita mizizi yake katika akili na nyoyo za watu. Kumbe, uvumilivu na udumifu ni mambo msingi yanayopaswa kutekelezwa, ili kuliwezesha Shirikisho hili kutokutumbukia tena katika historia yake iliyopita. Viongozi wapya watambue kwamba, katika kipindi chote cha miaka hii yote, Mama Kanisa ameonesha uwepo wake hali na mali. Huu ni wakati wa kuendeleza mchakato wa wongofu wa ndani, ili kuimarisha kwa ujasiri mkubwa matunda yaliyofikiwa hadi wakati huu, kwa kuzingatia dira na mwongozo uliotolewa na Mama Kanisa. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka wanashirika hawa kujiweka chini ya shule ya Roho Mtakatifu, ili kuondokana na hofu zisizo na mvuto wala mashiko!

Papa: Regnum Christi

 

 

02 March 2020, 10:45