Tafuta

Vatican News
Tarehe 13 Machi 2020 Baba Mtakatifu Francisko anaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 7 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Tarehe 13 Machi 2020 Baba Mtakatifu Francisko anaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 7 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. 

Papa Francisko Miaka 7 ya Maisha na Utume wake: Vipaumbele vyake

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Machi 2020 anaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 7 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro; kwa kujikita katika mambo makuu matatu: Maskini, Amani na Mazingira. Anahimiza utekelezaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” pamoja utume wa Kanisa miongoni mwa vijana pamoja na familia.

Na Padre Richard Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amejipambanua kwa kusimama kidete katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko na utamadunisho; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya umaskini ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Baba Mtakatifu anaendelea kuwasaidia waamini kubadilisha misimamo na mitazamo yao ya kiimani na kitamaduni, kwa kusoma alama za nyakati, ili kuliwezesha Kanisa kuachana na mazoea ya kujitafuta lenyewe kwa kujifungia sakristia, na badala yake liwe tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ari na moyo mkuu.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Machi 2020 anaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 7 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro; kwa kujikita katika mambo makuu matatu: Maskini, Amani na Mazingira. Baba Mtakatifu amendelea pia kutoa kipaumbele cha pekee katika utekelezaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” pamoja na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya kwa kujielekeza zaidi katika uchumi na elimu fungamanishi. Anawataka waamini kutangaza na kushuhudia ukuu, utakatifu na umuhimu wa ndoa na familia katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwa mashuhuda na watangazaji wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Anaendelea kumwilisha matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa kukazia “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”.

Maskini, Amani na Mazingira. Hizi ni amana na urithi mkubwa kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Baba Mtakatifu anasema, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa. Ili kuwaenzi maskini duniani, ameanzisha Siku ya Maskini Duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Baba Mtakatifu ameanzisha Idara ya Wakimbizi na Wahamiaji chini ya Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, Kanisa linakazia mambo makuu manne: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowakirimia. Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ni changamoto changamani katika maisha na utume wa Kanisa kwa nyakati hizi!

Upendeleo wa pekee kwa Maskini; Wagonjwa na Wazee: Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na kwa mara ya kwanza imeadhimishwa kunako mwaka 2017. Siku ya Maskini Duniani ni fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki, umoja na udugu unaovunjilia mbali kuta za utengano kwa sababu mbali mbali. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa daima limekuwa likisikiliza na kujibu kilio cha maskini na wahitaji kama inavyoshuhudiwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume, kwa kuwachagua Mashemasi saba walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho na hekima, ili waweze kutoa huduma kwa maskini. Neno la Mungu ni alama ya kwanza ya huduma kwa maskini kutokana na utambuzi kwamba, maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika udugu na mshikamano. Yesu mwenyewe aliwapatia maskini kipaumbele cha kwanza katika Heri za Mlimani kwa kusema, “Heri maskini, maana hao watairithi nchi”.

Jumuiya ya kwanza ya Wakristo iliuza mali na vitu vyake na kuwagawia watu kadiri ya mahitaji yao! Baba Mtakatifu anatoa kipaumbele cha pekee kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko lake kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo Yesu ni kiini cha furaha ya Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika ushuhuda. Wosia wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” ni ramani inayotoa dira na mwongozo thabiti wa shughuli za kichungaji zinazopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa sasa na kwa siku za mbeleni kwa kuwa na mwono wa kinabii na mwelekeo chanya, licha ya vikwazo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, ili Kristo Mfufuka aendelee kupeperusha bendera ya ushindi hadi kieleweke!

Utunzaji bora wa mazingira na wongofu wa kiekolojia: Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa “Laudato Si”  yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, anapembua kwa kina na mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiekolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji bora wa nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa na kwa ajili ya ustawi, maendeleo mafao ya watu wote duniani. Baba Mtakatifu katika Wosia wake wa “Laudato si” anakazia: umuhimu wa kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora; Injili ya Kazi ya Uumbaji; Anabainisha vyanzo vya mgogoro wa Ekolojia na mahusiano na watu; Ekolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda; pamoja na Elimu ya Ekolojia na maisha ya kiroho!

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 24 Mei, 2020 kuadhimisha Juma la “Laudato si” kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya miaka mitano, tangu kuchapishwa kwa Waraka huu wa kitume ambao umekuwa ni dira na mwongozo makini katika mchakato wa wongofu wa kiekolojia. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa makini, Je, ni ulimwengu gani wanaopenda kuwaachia watoto wao kama urithi kwa siku za usoni? Baba Mtakatifu kwa wa moyo wa unyenyekevu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Juma la “Laudato si” kama sehemu ya kumbu kumbu ya kimataifa ya Miaka mitano tangu kuchapishwa kwa Waraka huu wa kitume unaolenga utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Lengo ni kuweza kujibu kwa vitendo kipeo cha kiekolojia. Kamwe kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini hakiwezi kuendelea bila kusikilizwa! Ni wakati wa kujizatiti zaidi katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa moyo shukrani, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusherehekea kwa pamoja Juma la “Laudato si”.

Injili ya Haki na Amani Duniani: Baba Mtakatifu Francisko anasema: Siasa safi ni huduma ya amani, ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, yanayowashirikisha wadau mbali mbali mbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani. Amani ya kweli inalinda na kuheshimu haki msingi; utu na heshima ya binadamu kama unavyofafanuliwa kwenye Tamko la Haki Msingi za Binadamu. Hizi ni haki ya: uhai, elimu, afya, utamaduni, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kidini. Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” uliochapishwa kunako mwaka 1963 anakazia: Ukweli, haki, upendo na uhuru na kwamba, haki na wajibu ni sawa na chanda na pete ili kujenga na kudumisha jamii inayofumbatwa katika msingi wa amani inayodumishwa katika upendo na msamaha.

Baba Mtakatifu anapenda kuwachangamotisha wanasiasa, kuhakikisha kwamba, wanaondokana na mizizi ya dhambi inayowatumbukiza watu wengi katika majanga na badala yake, wajikite katika ujenzi wa siasa safi na amani kwa kukataa kishawishi cha uchu wa mali na madaraka; unafsia wa haki msingi za binadamu; maamuzi mbele, ubaguzi wa rangi; hofu zisizokuwa na mvuto wala mashiko; sera potofu dhidi ya wakimbizi na wahamiaji; kwani yote haya ni mambo ambayo yanasigana kimsingi na siasa safi kama huduma ya amani. Uwajibikaji na utunzaji wa amani unafumbatwa katika siasa safi kukita mizizi yake katika sakafu ya moyo wa mtu. Heri yao wanaojitaabisha katika ujenzi wa amani; amani jamii, amani katika utunzaji bora wa mazingira na amani katika dhamiri za watu! Baba Mtakatifu anaendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya haki na amani duniani kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Haya ni mambo ambayo anayashuhudia katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Injili ya amani ni muhtasari wa upendeleo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Kwani uchafuzi wa mazingira pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ni chanzo kikuu kinachowatumbukiza watu wengi katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato, hali inayotishia amani na mafungamano ya kijamii duniani! Mtumishi wa Mungu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania aliwahi kusema kwamba, ili nchi iweze kuendelea na watu wake kufurahia maendeleo yao, inahitaji mambo makuu manne: watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Siasa safi inajikita katika dhamana ya kuwawakilisha watu kikamilifu.

Majadiliano ya Kiekumene na Kidini ili kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu: Baba Mtakatifu anakazia sana majadiliano ya kiekumene na ya kidini kama yanavyofafanuliwa kwa kina na mapana katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.Hati hii ina umuhimu wake kihistoria, kimaadili, kitamaduni na kijamii, kwa sababu ni hati ambayo imewashikirisha viongozi wakuu wa dini mbali mbali duniani, ambao wanaendelea kuhimiza umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita zaidi katika majadiliano ya kidini, ili kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja licha ya tofauti msingi zinazojitokeza kati yao. Lengo ni kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa: Sinodi ya XVI ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2022 itaongozwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, ushiriki na utume”. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji!

Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni: Ufahamu wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Dhana ya Sinodi ni wazo lililotolewa na Mtakatifu Paulo VI, linaloihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuanza kumwilisha dhana hii katika maisha ya Makanisa mahalia; Mabaraza ya Maaskofu; Mashirikisho ya Kanda hadi kufikia Kanisa la Kiulimwengu. Sinodi ya Kanisa ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa wa kutaka kutembea kwa pamoja chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu kama sehemu ya mchakato wa utambulisho wa Kanisa na uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ndio ufafanuzi wa kina uliotolewa na Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Sinodi ni chombo cha uinjilishaji unaolisaidia Kanisa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari na mang’amuzi mbali mbali.

Papa Francisko 7 Years

 

12 March 2020, 10:16