Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana Jumapili tarehe 15 Machi 2020 amegusia kuhusu majadiliano kati ya Kristo Yesu na Mwanamke Msamaria: Nabihi na Masiha wa Bwana. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana Jumapili tarehe 15 Machi 2020 amegusia kuhusu majadiliano kati ya Kristo Yesu na Mwanamke Msamaria: Nabihi na Masiha wa Bwana. 

Papa Francisko: Kristo Yesu na Mwanamke Msamaria: Ufunuo: Nabii na Masiha wa Bwana!

Kiini cha majadiliano haya maji kama hitaji muhimu sana katika maisha ya binadamu; maji kama alama ya neema ya Mungu inayomkirimia mwamini maisha na uzima wa milele. Mwenyezi Mungu kama chemchemi ya maisha ya uzima wa milele. Manabii wanaonesha kwamba, kwa watu waliokengeuka na kumwasi Mwenyezi Mungu kwa kuacha Amri na Maagizo yake ni sawa na nchi kavu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye Maktaba yake binafsi, Jumapili tarehe 15 Machi 2020, amemshukuru na kumpongeza Askofu mkuu Mario Enrico Delpini wa Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia, eneo ambalo kwa sasa ni kitovu cha maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 nchini Italia ambavyo kwa sasa vinaendelea kupukutisha maisha ya watu wengi ndani na nje ya Italia. Katika kipindi hiki cha mahangaiko makubwa ya watu wa Mungu Jimbo kuu la Milano, Askofu mkuu Delpini ameendelea kushikamana na watu wake kwa kuwa karibu na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, huku akisali na kuwaaminisha watu wa Mungu katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Baba Mtakatifu anapenda pia kuwashukuru na kuwapongeza Mapadre ambao wameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma mbali mbali kwa watu wa Mungu kutoka huko Lombardia, ambako watu wengi wameathirika. Mapadre wameendelea kuonesha uwepo na ukaribu wao kwa watu wa Mungu ili kamwe wasidhani kwamba, wamebaki pweke katika shida na mahangaiko yao mbali mbali. Mapadre wametambua vyema kwamba, wakati huu wa mlipuko wa magonjwa, ni muda muafaka wa kushikamana na watu wa Mungu na wala si wakati wa kutokomea kule kusikojulikana, kiasi cha kutambulikana kuwa “Mapadre watoro”. Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu hiki ni kipindi cha majaribu makubwa katika maisha ya watu; changamoto inayojibiwa kwa kujikita katika fadhila ya imani, matumaini na mapendo.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kufanya tafakari ya kina kuhusu mahojiano kati ya Kristo Yesu na Mwanamke Msamaria. Yesu akiwa njiani pamoja na wanafunzi wake, wakielekea Galilaya naye alikuwa hana budi kupitia kati kati ya Samaria, Yesu kwa sababu alikuwa amechoka na kubanwa na kiu ya maji akaketi vivi hivi kisimani. Itakumbukwa kwamba, Wasamaria na Wayahudi walikuwa hawachangamani yaani “hawawezi kupikika chungu kimoja”. Wayahudi waliwadharau sana Wasamaria kwa kuwaona kuwa ni watu wa chini sana. Kristo Yesu, akiwa amejichokea na kusongwa na kiu, akaja Mwanamke Msamaria, akamwomba maji ya kunywa. Kwa maneno haya, Kristo Yesu alivunjilia mbali kuta za utengano kati ya Wasamaria na Wayahudi na kuanza mahojiano, kiasi cha kumfunulia yule Mwanamke Msamaria “Fumbo la Maji ya Uzima wa milele”, yaani Roho Mtakatifu, zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Yule Mwanamke Msamaria alipomwomba maji, kwa mshangao mkubwa Kristo Yesu akamwambia “Kama angeliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, “Nipe maji ninywe”, ungalimwomba yeye, naye angelikupa maji yaliyo hai”. Kiini cha majadiliano haya maji kama hitaji muhimu sana katika maisha ya binadamu; maji kama alama ya neema ya Mungu inayomkirimia mwamini maisha na uzima wa milele. Maandiko Matakatifu yanamwonesha Mwenyezi Mungu kama chemchemi ya maisha ya uzima wa milele. Manabii wanaonesha kwamba, kwa watu waliokengeuka na kumwasi Mwenyezi Mungu kwa kuziacha Sheria na njia zake ni sawa na ardhi inayokabiliwa na ukame wa kutisha. Wayahudi walipata mang’amuzi haya walipokuwa Jangwani kwa muda wa miaka 40. Katika safari ya ukombozi, Wayahudi walihisi kiu, wakamnung’unukia Mwenyezi Mungu na Musa, mtumishi wake. Kwa kutimiza mapenzi ya Mungu, Musa akawapa Wayahudi maji kutoka mwambani, kama alama ya uwepo endelevu wa Mungu kati pamoja nao, ili kuwakirimia maisha tele!

Kwa upande mwingine Baba Mtakatifu anasema, Mtakatifu Paulo, Mtume, anatafsiri mwamba huu kuwa ni Kristo Yesu kwa kusema, wote wakanywa kinywaji kilekile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata, na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Rej. 1 Kor. 10: 4. Hili ni fumbo linaloonesha uwepo endelevu wa Mungu kati pamoja na watu wake wanaosafiri huku bondeni kwenye machozi. Kristo Yesu ni Hekalu, kadiri ya mwono wa kinabii, chemchemi ya Roho Mtakatifu, yaani maji yanayotakasa na kuwapatia watu uhai. Kwa wale wote wenye kiu ya wokovu wanaweza kuzima kiu yao kwa njia ya Kristo Yesu na Roho Mtakatifu ambaye anageuka kuwa ni chemchemi ya maji yanayobubujikia utimilifu wa maisha na uzima wa milele.

Hii ndiyo ahadi ambayo Kristo Yesu alimtolea Mwanamke Msamaria na ikageuka kuwa uhalisia wa maisha katika Fumbo la Pasaka. Yesu alipochomwa ubavuni kwa mkuki mara ikatoka damu na maji. Yesu ndiye yule Mwanakondoo wa Mungu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa sasa ni chemchemi ya Roho Mtakatifu, anayewaondolea watu dhambi zao na kuwakirimia maisha mapya. Zawadi hii ni kiini cha ushuhuda. Kama ilivyokuwa kwa yule Mwanamke Msamaria, kwa mtu yeyote anayekutana na Kristo Mfufuka, anasukumwa kumtangaza na kumshuhudia Yesu kwa jirani zake, ili wote kwa pamoja waweze kukiri kwamba kwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu, kama walivyofanya wale Wasamaria.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwa kusema, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wanazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu, changamoto na mwaliko wa kushuhudia upya wa maisha na matumaini yaliyoko ndani mwao. Ikiwa kama jitihada za kumtafuta Kristo Yesu na kiu yao ya maisha ya ndani inapata kitulizo, wataweza kutambua kwamba, wokovu wao umekita mizizi yake ndani ya Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu, anayewapenda na kuwakirimia maji ya uzima wa milele. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa awasaidie waamini kuwa na kiu ya kumtafuta Kristo Yesu, chemchemi ya maisha ya uzima, ambaye ni yeye peke yake anayeweza kuzima kiu ya maisha na upendo walioubeba ndani ya mioyo yao!

Papa: Malaika wa Bwana

 

15 March 2020, 10:36