Tafuta

Papa Francisko anawaalika waamini kujiunga pamoja kuadhimisha Juma la "Laudato si" kuanzia tarehe 16-24 Mei, 2020, kumbu kumbu ya miaka 5 ya Waraka wa Kitume, "Laudato si". Papa Francisko anawaalika waamini kujiunga pamoja kuadhimisha Juma la "Laudato si" kuanzia tarehe 16-24 Mei, 2020, kumbu kumbu ya miaka 5 ya Waraka wa Kitume, "Laudato si". 

Papa Francisko: Maadhimisho ya Juma la "Laudato si" 16-24 Mei 2020

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 24 Mei, 2020 kuadhimisha Juma la “Laudato si” kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya miaka mitano, tangu kuchapishwa kwa Waraka huu wa kitume ambao umekuwa ni dira na mwongozo makini katika mchakato wa wongofu wa kiekolojia. Miaka 5 ya "Laudato si"!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayokita miziz yake katika misingi ya haki na amani kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato Si” uliozinduliwa hapo tarehe 18 Juni 2015 mjini Vatican. Kichwa cha Waraka huu kinapata chimbuko lake kutoka katika wimbo wa Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa ajili ya viumbe na unaweza kutafsiriwa kuwa ni “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Baba Mtakatifu anaonekana kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi. Anaungana naye kuimba utenzi wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia. Anapenda kukazia umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu, anapembua kwa kina na mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiekolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa na kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote! Ni katika mukadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 24 Mei, 2020 kuadhimisha Juma la “Laudato si” kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya miaka mitano, tangu kuchapishwa kwa Waraka huu wa kitume ambao umekuwa ni dira na mwongozo makini katika mchakato wa wongofu wa kiekolojia.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa makini, Je, ni ulimwengu gani wanaopenda kuwaachia watoto wao kama urithi kwa siku za usoni? Baba Mtakatifu kwa moyo wa unyenyekevu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Juma la “Laudato si” kama sehemu ya kumbu kumbu ya kimataifa ya Miaka mitano tangu kuchapishwa kwa Waraka huu wa kitume unaolenga utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Lengo ni kuweza kujibu kwa vitendo kipeo cha kiekolojia. Kamwe kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini hakiwezi kuendelea bila kusikilizwa! Ni wakati wa kujizatiti zaidi katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa moyo shukrani, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusherehekea kwa pamoja Juma la “Laudato si”.

Katika kipindi cha miaka mitano tangu kuchapishwa kwa Waraka huu wa Kitume, Jumuiya na watu mbali mbali wameendelea kumwilisha waraka huu katika uhalisia wa maisha wakiwa na mwono wa ekolojia fungamani. Jambo la kusitikisha ni kuona kwamba, kasi ya uharibifu wa mazingira kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kubwa sana, kiasi kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza kwa vitendo ushauri unaotolewa na wanasayansi. Waraka huu wa kitume ni jibu makini linalotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ili kupambana na uchafuzi pamoja na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anapenda kuchukua fursa hii kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema sehemu mbali mbali za dunia kuchukua hatua madhubuti na endelevu katika maadhimisho ya Juma la “Laudato si” kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 24 Mei, 2020. Huu ni muda muafaka wa kufanya tafakari ya kina kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, uliopitishwa Jijini Paris, nchini Ufaransa, Desemba 2015. Nchi nyingi duniani ziliahidi kudhibiti viwango vya ongezeko la joto duniani na kuhakikisha hakizidi nyuzi joto mbili kwa kipimo cha Selsiasi, na kuendeleza msukumo unaolenga kufikia nyuzi joto moja na nusu kwenye kipimo hicho.

Utekelezaji wa Mkataba huu unafanyika katika ngazi ya kitaifa na kimataifa, kwa ajili ya ustawi na maendeleo mapana zaidi ya Jumuiya ya Kimataifa. Waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wajitahidi kufanya tafakari ya kina katika mwanga wa ukweli na uwazi kuhusu vitendo vyao, tayari kujichimbia katika mchakato wa wongofu wa kiekolojia kwa kuchukua hatua madhubuti, ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika majanga na umaskini wa hali ya juu. Hii ni fursa pia kwa watu binafsi na Jumuiya mbali mbali kushirikisha maamuzi na hatua walizofikia kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Itakumbukwa kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kutafuta njia zitakazosaidia kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Serikali mbali mbali katika Kipindi cha Mwaka 2020 zinatakiwa kuonesha sera na mbinu mkakati wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kwa kuutekeleza kwa makini.

Papa: Juma la Laudato si

 

03 March 2020, 13:54