Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuondoa jiwe la kifo, ubaguzi, unafiki na umbea ili maisha yaweze kuchanua tena kama maua ya kondeni! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuondoa jiwe la kifo, ubaguzi, unafiki na umbea ili maisha yaweze kuchanua tena kama maua ya kondeni! 

Papa Francisko: Ondoeni Jiwe la kifo, unafiki na ubaguzi kwa njia ya imani

Hata leo hii, Kristo Yesu anawaambia wafuasi wake, ondoeni jiwe hilo! Mungu hakumuumba mwanadamu kwa ajili ya kifo, bali kwa ajili ya maisha, mazuri na yenye furaha. Kifo kimeingia ulimwenguni kutokana na usuda wa Shetani, Ibilisi. Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kuondoa jiwe la unafiki, ili waweze kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo! JIWE LA KIFO!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima, Mwinjili Yohane anamleta Lazaro wa Bethania aliyekuwa kaka yake na Martha pamoja na Mariamu, rafiki zake na Yesu. Lazaro alikuwa amefariki dunia, yapata siku nne na Mariamu aliposikia kwamba, Kristo Yesu amekwenda kuwatembelea, alikimbia kumlaki na kumwambia kwamba, kama angelikuwapo hapo, ndugu yao Lazaro hangalikufa. Lakini, Yesu akamwambia ndugu yako atafufuka kwa sababu Kristo Yesu ndiye ufufuo, na uzima. Ni Bwana na chemchemi ya maisha mapya hata kwa wale ambao walikuwa wamekwisha kufariki dunia. Kwa namna ya pekee kabisa, Kristo Yesu aliguswa na kilio cha waombolezaji, kiasi cha kutokwa na machozi.

Baada ya kuliondoa lile jiwe, Kristo Yesu akatumia fursa ile kwa ajili ya kumshukuru Baba yake wa mbinguni kwa vile anamsikiliza na anatambua kwamba, anamsikia siku zote, lakini aliyasema yote haya kwa ajili ya mkutano ili wapate kusaidiki kwamba, kweli ametumwa na Mwenyezi Mungu. Akamwita Lazaro aje nje ya kaburi, akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi na uso wake umefungwa leso! Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 29 Machi 2020 kutoka katika Maktaba yake ya kitume. Maandiko Matakatifu yanamwonesha Mwenyezi Mungu kuwa ni chemchemi ya uhai na hatima ya maisha ya mwanadamu.

Ugonjwa na hatimaye kifo cha Lazaro, kilikuwa ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili na Mwana wa Mungu atukuzwe kwa ugonjwa huo. Hapa imani kwa Mwenyezi Mungu inakutana na nguvu na upendo wa Mungu dhidi ya kifo. Imani kwa Mwenyezi Mungu inaoneshwa kwa namna ya pekee na Mariamu, Martha na wale waombolezaji. “Kama ungalikuwepo hapa” hiki ni kilio cha imani dhidi ya Fumbo la kifo linalomwandama mwanadamu! Na Kristo Yesu anajibu kwa uhakika kwamba, “Yeye ndio huo ufufuo, na uzima! Kumbe, jambo la msingi kwa waamini ni kuwa na imani kwa Kristo Yesu, kwani kifo kilichokuwa kinaonekana kana kwamba, kimeshinda, mbele ya Kristo Yesu, hakiwezi kufua dafu! Jambo la msingi ni kuondoa jiwe katika nyoyo zao, ili kuruhusu Neno la Mungu liweze kuingia na kuleta maisha mapya, pale ambapo kifo kilikuwa kimeanza kutawala.

Hata leo hii, Kristo Yesu anawaambia wafuasi wake, ondoeni jiwe hilo! Mwenyezi Mungu hakumuumba mwanadamu kwa ajili ya kifo, bali kwa ajili ya maisha, mazuri na yenye furaha. Kifo kimeingia ulimwenguni kutokana na usuda wa Shetani, Ibilisi. Kristo Yesu amekuja ulimwenguni ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika makucha ya Shetani, Ibilisi. Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kuondoa jiwe la unafiki, ili waweze kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo! Waondoe jiwe la kifo na shutuma dhidi ya jirani zao; waondoe jiwe la umbea na uzandiki; jiwe linalowatenga na kuwasukumizia maskini pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, ili maisha yaweze kuchanua tena “kama maua ya kondeni”. Kristo anaishi, anayempokea na kuandamana pamoja na kuambatana naye katika maisha, atakutana na Injili ya uhai. Bila Kristo Yesu, watu wengi wataanguka na kutumbukia katika kifo!

Ufufuko wa Lazaro ni alama ya mchakato wa maisha mapya yanayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo inayofumbatwa kikamilifu katika Fumbo la Pasaka ya Kristo Yesu. Kwa njia ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, Mkristo anakua ni mtu anayetembea katika maisha, kielelezo cha kiumbe kipya, kinachoelekea katika uhai. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumkimbilia Bikira Maria, ili kwa njia ya upendo wa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, awasaidie kuwa na huruma na upendo kama alivyofanya Kristo Yesu kwa waja wake. Hiki ni kipindi cha kuonesha umoja, upendo na mshikamano kwa watu walioguswa na kutikishwa na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virus vya Corona, COVID-19. Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu inayomwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la kifo na kuhakikisha kwamba, Injili ya uhai inaibuka kidedea!

Papa: Kilio cha Yesu
30 March 2020, 15:37