Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anaunga mkono jitihada za Umoja wa Mataifa za kutaka kusitisha vita, ili kuunganisha nguvu kuokoa maisha ya watu wengi wanaoshambuliwa kwa Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko anaunga mkono jitihada za Umoja wa Mataifa za kutaka kusitisha vita, ili kuunganisha nguvu kuokoa maisha ya watu wengi wanaoshambuliwa kwa Virusi vya Corona, COVID-19.  (AFP or licensors)

Papa Francisko aunga mkono wito wa UN wa kusitisha vita duniani

Hivi karibuni, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres ambaye ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kusitisha mara moja vita sehemu mbali mbali za dunia, ili kutoa nafasi kwa Jumuiya ya Kimataifa kupambana fika na janga la maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni ugonjwa usiotambua mipaka ya dunia. Papa anaunga mkono hoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani, utulivu, ustawi na maendeleo ya wengi na hasa zaidi mapambano ya silaha. Kuna ongezeko kubwa la watu wanaoendelea kupekenywa na milipuko ya magonjwa ya kutisha na baa la njaa duniani, lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, umoja, upendo na mshikamano katika mapambano dhidi ya majanga yote haya unazidi kumong’onyoka kila kukicha. Umefika wakati wa kutekeleza kwa vitendo sera na mikakati inayopania kufutilia mbali: umaskini, magonjwa na njaa.

Ni wakati wa kuwekeza katika mchakato wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi, kwa kuhakikisha kwamba, biashara haramu ya silaha duniani pamoja na vita vinakoma, kwani vita ni mama wa majanga makubwa ya binadamu! Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana na tafakari yake, Jumapili tarehe 29 Machi 2020, ameunga mkono juhudi zinazofanywa na Umoja wa Mataifa. Hivi karibuni, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kusitisha mara moja vita sehemu mbali mbali za dunia, ili kutoa nafasi kwa Jumuiya ya Kimataifa kupambana fika na janga la maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni ugonjwa usiotambua mipaka ya dunia.

Baba Mtakatifu anaungana na wale wote wanaoendelea kuunga mkono juhudi hizi za Umoja wa Mataifa, kwa kuondokana na chuki, uhasama na tabia ya kutaka kulipizana kisasi kwa njia ya mtutu wa bunduki. Lengo ni kuanzisha mchakato wa huduma za kibinadamu; kwa kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidiplomasia, daima kipaumbele cha kwanza kikiwa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni wakati wa kuunganisha nguvu dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Watu watambue umuhimu wa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu kwa kutambua fika kwamba, kwa pamoja wanajenga familia kubwa ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anawasihi viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanapyaisha dhamana na wajibu wao wa kusitisha na hatimaye, kuondokana na dhana ya uadui pamoja na baadhi ya Mataifa kutaka kujimwambafai. Badala yake, tofauti zinazojitokeza zishughulikiwe kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; daima wakilenga kutafuta na kudumisha amani duniani.

Baba Mtakatifu amewakumbuka pia watu wanaolazimika kuishi katika makundi makubwa makubwa: hawa ni wazee wanaohudumiwa kwenye nyumba za wazee, askari wa vikosi vya ulinzi na usalama, lakini zaidi wafungwa magerezani. Changamoto kubwa ni magereza kuendelea kufurika kupita kiasi, jambo ambalo ni kinyume cha haki msingi za binadamu. Kutokana na muktadha huu, maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosabanishwa na Virusi vya Corona, COVID yanatishia usalama na maisha ya wafungwa wengi magerezani. Ugonjwa huu ukiingia magerezani, litakuwa ni janga jingine tena. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na wakuu wanchi kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kadiri ya uwezo wao kuhakikisha kwamba, wafungwa magerezani hawaambukizwi Virusi vya Corona, COVID-19.

Papa: Vita

 

 

29 March 2020, 15:19