Tafuta

Vatican News
Papa Francisko ashindwa kuhudhuria mafungo ya Kwaresima kwa mwaka 2020 huko Ariccia kutokana na kubanwa na mafua makali! Papa Francisko ashindwa kuhudhuria mafungo ya Kwaresima kwa mwaka 2020 huko Ariccia kutokana na kubanwa na mafua makali!  (Vatican Media)

Papa Francisko ashindwa kuhudhuria Mafungo ya Kwaresima 2020

Wasaidizi wa karibu wa Papa Francisko, "Curia Romana" Jumapili tarehe 1 Machi 2020, huko Ariccia nje kidogo ya mji wa Roma na mafungo haya yatahitimishwa hapo tarehe 6 Machi 2020. Lakini kutokana na kubwana sana na mafua, Baba Mtakatifu Francisko amesema, ataendelea kushiriki mafungo haya akiwa mjini Vatican. Mafungo yanaongozwa na Padre Pietro Bovati, SJ.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima, tarehe 1 Machi 2020, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alitambua uwepo wa mahujaji na wageni kutoka ndani na nje ya Italia. Akatumia fursa hii kuwatakia, mfungo mwema wa Kipindi cha Kwaresima, ili kweli uwasaidie kujichotea matunda ya Roho Mtakatifu kwa kujikita zaidi katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anasema, anasikitishwa sana na taarifa kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuhusu watu wengi wasiokuwa na makazi maalum, wanaokimbia vita, majanga asilia na umaskini wakitafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi wanavyotseka. Baba Mtakatifu amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka na kuwaombea katika sala zao hasa katika Kipindi hiki cha Kwaresima.

Baba Mtakatifu amewaomba waamini pia kumsindikiza kwa sala yeye pamoja na wasaidizi wake wa karibu, walioanza mafungo ya maisha ya kiroho, Jumapili tarehe 1 Machi 2020, huko Ariccia nje kidogo ya mji wa Roma na mafungo haya yatahitimishwa hapo tarehe 6 Machi 2020. Lakini kutokana na kubwana sana na mafua, Baba Mtakatifu Francisko amesema, ataendelea kushiriki mafungo haya akiwa mjini Vatican. Anapenda kujiunga na wasaidizi wake wa karibu, “Curia Romana” pamoja na watu wote wanaofanya mafungo wakiwa majumbani mwao!

Tafakari wakati wa mafungo haya ya maisha ya kiroho inaongozwa na Padre Pietro Bovati, SJ, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa ya Biblia na Mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Mtakatifu. Kauli mbiu inayoongoza mafungo haya ni “Kile kijiti kiliwaka moto: mkutano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu mintarafu mwanga wa Kitabu cha Kutoka, Injili ya Mathayo na Sala ya Zaburi”. Utamaduni wa kumsikiliza Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha ya mtu ni mang’amuzi ya kinabii kama yanavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu. Vielelezo vikuu hapa ni kijiti kilichokuwa kinawaka moto, Neno la Mungu lililokuwa linatoka katika moto huu na kuiangazia njia hii ya maisha. Mafungo ya kiroho ni fursa muafaka ya kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha ya mwamini.

Papa: Mafungo 2020
01 March 2020, 12:38