Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuonesha mshikamano wa kiroho kwa wale wote wanao mkimbilia Mama Kanisa kwa imani na matumaini wakati wa raha na magumu ya maisha! Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuonesha mshikamano wa kiroho kwa wale wote wanao mkimbilia Mama Kanisa kwa imani na matumaini wakati wa raha na magumu ya maisha! 

Mshikamano wa Papa Francisko kwa wanao mtumainia Mama Kanisa katika shida zao!

Mapadre na Watawa wanatakiwa kuonesha uwepo wao wa karibu kwa wagonjwa, wazee na maskini pamoja na familia zinazohitaji msaada wa wa hali na mali kutokana na hali tete ilivyo kwa sasa. Hiki ni kipindi cha kuonesha mshikamano wa: imani, huruma na upendo kwa watu wa Mungu, wanaokimbilia kwa Kanisa wakiomba msaada katika mahangaiko na mateso yao: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anawaalika Mapadre na Watawa kuonesha uwepo wao wa karibu kwa wagonjwa, wazee na maskini pamoja na familia zinazohitaji msaada wa wa hali na mali kutokana na hali tete ilivyo kwa sasa. Hiki ni kipindi cha kuonesha mshikamano wa huruma na upendo kwa watu wa Mungu, wanaokimbilia kwa Kanisa wakiomba msaada katika mahangaiko na mateso yao: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko ameamua kuwasindikiza watu wa Mungu kwa sala na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; kwa kuwaaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, afya ya wagonjwa. Katika kipindi hiki cha hofu na mashaka ya maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona sehemu mbali mbali za dunia, Baba Mtakatifu ataendelea kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Ibada hii inaanza kila siku majira ya Saa 1: 00 za asubuhi kwa Saa za Ulaya na kutangazwa moja kwa moja na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican pamoja na mitandao ya jamii.

Baba Mtakatifu anawaalika Mapadre kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu wanapata huduma msingi za maisha ya kiroho kama chemchemi ya imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Tarehe 15 Machi 2020, Baba Mtakatifu anaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, ili kutoa nafasi kwa waamini ambao wako kwenye karantini walau kuonja faraja ya Neno la Mungu katika kipindi hiki kigumu cha ukame wa maisha ya kiroho! Ibada ndani na nje ya Vatican zinazingatia na kuheshimu itifaki ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 iliyotolewa na Serikali ya Italia. Tarehe 18 Machi 2020, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuendeleza Katekesi yake, itakayotangazwa moja kwa moja kutoka kwenye Maktaba yake na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Huduma hii inaweza pia kutolewa kwa vituo vya televisheni sehemu mbali mbali za dunia, ikiwa kama vitawasilisha maombo yao mjini Vatican.

Lengo ni kutaka kuhakikisha kwamba, ujumbe wa imani, matumaini na mapendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko unawafikia watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia! Itakumbukwa kwamba, tarehe 19 Machi 2020, Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria, atakuwa anakumbukia mwaka wa nane wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

 

14 March 2020, 14:07