Tafuta

Vatican News
Mpango Mkakati wa Saa 24 kwa Ajili ya Bwana ni Muda wa Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Toba na Msamaha wa Dhambi. Mpango Mkakati wa Saa 24 kwa Ajili ya Bwana ni Muda wa Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Toba na Msamaha wa Dhambi. 

Papa Francisko: Mpango Mkakati wa Saa 24 kwa Ajili ya Bwana 2020

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” kwa mwaka huu wa 2020 waamini mjini Roma, Italia na sehemu nyingi za dunia hawataweza kuuadhimisha kadiri ya Mapokeo ya Kanisa kutokana na kipeo cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, CODIV-19. Pale inapowezekana, waamini washiriki kwa uchaji, ibada na toba!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujizatiti kikamilifu katika hija ya Kipindi cha Kwaresima, yaani Siku 40 katika Jangwa la maisha ya kiroho kwa njia ya: toba na wongofu wa ndani; kufunga, kusali, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu pamoja na kulinafsisha katika matendo ya huruma:kiroho na kimwili. Mama Kanisa anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika Sakramenti ya Upatanisho kama mahali muafaka pa kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, tayari kusimama tena na kuendelea na safari ya: imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima na kwa mwaka huu ni tarehe 20-21 Machi 2020. Kila Jimbo linapaswa kufanya maadhimisho haya ili kuwapatia waamini nafasi ya kuweza kuchunguza dhamiri zao, kujuta, kuungama na hatimaye kutimiza malipizi, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kadiri ya mazingira na hali halisi ya wakati huu wa mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, CODIV-19.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, Mpango Mkakati wa“Saa 24 kwa ajili ya Bwana” kwa mwaka huu wa 2020 kwa waamini mjini Roma, Italia na sehemu nyingi za dunia hawataweza kuuadhimisha kadiri ya Mapokeo ya Kanisa kutokana na kipeo cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, CODIV-19. Pale inapowezekana, Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kushiriki Ibada hii kwa uchaji, kama njia ya kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Waamini watambue kwamba, huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wa Mungu kwa binadamu. Kwa njia hii, waamini nao wanapaswa kuwa ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao   Hii ni huruma inayopaswa pia kushuhudiwa katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho inayogusa undani wa mtu, kwani hili ni chimbuko la amani na utulivu wa ndani. Ni huruma inayosamehe na kuokoa. Mapadre waungamishi wanao wajibu wa kuwa ni watumishi waaminifu wa huruma na msamaha wa Mungu kwa binadamu, kwa kuwapokea waamini wanaokimbilia kiti cha huruma ya Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma katika mfano wa Mwana mpotevu!

Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena anapenda kuwakumbusha Mapadre waungamishaji kwamba, wao ni vyombo vya upatanisho, huruma na upendo wa Mungu na kamwe si wamiliki wa dhamiri za waamini. Wajenge utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini, ili wawasaidie waamini wao kufanya mang’amuzi ya kina, kuhusu maisha na wito wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho  ya Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima. Ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kumrudia Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Hii ni Sakramenti inayomfanya mtu aguse kwa mkono wake ukubwa wa huruma ya Mungu, ili kupata amani na utulivu wa ndani!

Katika Kesha la Pasaka, Mama Kanisa atawasha Mshumaa wa Pasaka kwa moto mpya ambao pole pole utalifukuza giza na kuwaangaza waamini watakaokuwa kwenye maadhimisho ya Liturujia. Mwanga wa Kristo Mfufuka katika utukufu unaofukuzia mbali giza la moyo na roho, ili wote waweze kuishi katika mang’amuzi ya wanafunzi wa Emmau: kwa kusikiliza Neno la Mungu na kulishwa kwa Ekaristi Takatifu itakayoiwezesha mioyo yao kuweza kuwaka tena moto wa imani, matumaini na mapendo!

Papa: Mpango Mkakati 24 HRS

 

18 March 2020, 16:08