Tafuta

Vatican News
Mama Kanisa ni shuhuda na mtetezi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Waamini wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai! Mama Kanisa ni shuhuda na mtetezi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Waamini wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai!  (AFP or licensors)

Kanisa ni mtetezi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, adhabu ya kifo hii ni kielelezo cha ukatili wa hali ya juu kabisa na wala haiwezi kukubalika tena, kwani inakwenda kinyume cha mwanga wa Injili. Hii ni changamoto kwa Serikali na wadau mbali mbali kujizatiti katika kulinda, kutunza na kudumisha uhai wa binadamu ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Adhabu ya Kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika mwendelezo wa Mapokeo na Mafundisho hai ya Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kufanya marekebisho kwenye Katekisimu ya Kanisa Katoliki, kifungu namba 2267 kinachozungumzia kuhusu adhabu ya kifo na tafsiri mpya inapaswa kuingizwa katika vipengele mbali mbali vya Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Kanisa Katoliki limefuta adhabu ya kifo katika Mafundisho na Mapokeo yake kwa kukazia: njia zinazotetea na kulinda maisha ya watu, amani na usalama wao dhidi ya adui; kwani hizi ni njia zinazodumisha utu, ustawi na mafao ya wengi. Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ameendelea kuwa mstari wa mbele kupinga utamaduni wa kifo, unaodhalilisha utu heshima na haki msingi za binadamu. Amekuwa akitoa kipaumbele cha pekee kwa binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni  mwendelezo wa Mapokeo na Mafundisho yaliyotolewa na watangulizi wake, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Yohane Paulo II na hata Mtakatifu Paulo VI na katika nyaraka mbali mbali za Kanisa.

Kwa mabadiliko haya, Baba Mtakatifu Francisko anataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kutambua kwamba, haki ya kuishi ni msingi wa haki nyingine zote. Ikumbukwe kwamba, Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Sala. Kwa mara ya kwanza ilichapishwa kunako mwaka 1992 na kufanyiwa marekebisho kunako mwaka 1997 “Editio typica” iliyorekebisha kuhusu adhabu ya kifo kwa kusoma alama za nyakati! Lengo ni kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Hii ni amana ya imani ya Kanisa Katoliki mintarafu mwanga wa Injili. Adhabu ya kifo hii ni kielelezo cha ukatili wa hali ya juu kabisa na wala haiwezi kukubalika tena, kwani inakwenda kinyume cha mwanga wa Injili. Hii ni changamoto kwa Serikali na wadau mbali mbali kujizatiti katika kulinda, kutunza na kudumisha uhai wa binadamu ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa nchi zile ambazo bado zinaendekeza adhabu ya kifo, sasa ni wakati wa kutafuta adhabu mbadala, ili kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, changamoto ambayo Baba Mtakatifu Francisko anataka kuwarithisha vijana wa kizazi kipya.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na maendeleo makubwa juu ya tafsiri na uelewa wa Mafundisho ya Kanisa kuhusu utu na heshima ya binadamu kadiri ya mwanga wa Injili, hali ambayo imepelekea hata Baba Mtakatifu Francisko kuamua kufanya mabadiliko kwenye kifungu cha Katekisimu ya Kanisa Katoliki kinachofuta adhabu ya kifo kama sehemu ya Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Ikumbukwe kwamba, Baba Mtakatifu katika mawazo yake kuhusu adhabu ya kifo anakazia umuhimu wa kulinda uhai wa binadamu na kuuendeleza, changamoto na mwaliko wa kuleta mwono na mwelekeo mpya kuhusu: maisha, utu na heshima ya binadamu. Hii ni hatua kubwa na muhimu katika kutafsiri Mapokeo na Mafundisho hai ya Kanisa kadiri ya Mwanga wa Injili na kwa kusoma alama za nyakati. Kanisa anasema Askofu mkuu Fisichella, linatambua uchungu wa watu walioguswa na kutikiswa na matukio ambayo yamepelekea adhabu ya kifo kwa wahusika, lakini, Kanisa linavitaka vyombo vya sheria kutenda haki na kuwajibika barabara badala ya kuendeleza chuki, uhasama pamoja na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa njia ya adhabu ya kifo.

Kanisa linayasema yote haya kwa kutoa fursa kwa wale waliotenda makosa kama haya yanayostahili kupewa adhabu ya kifo, kupata muda wa toba na wongofu wa ndani, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao; tayari kuanza kuandika ukurasa mpya kwa kujivika utu mpya na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Toba na wongofu wa ndani; msamaha, upatanisho na haki ni mambo msingi yanayozingatiwa na Mama Kanisa katika mchakato wa kufutilia mbali adhabu ya kifo. Hii ni hatua mpya katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Ni wakati wa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na familia inayofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mauaji ya aina yoyote ile ni jambo ambalo haliwezi kukubalika katika mwanga wa Injili.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella anawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuitumia Katekisimu ya Kanisa Katoliki kama kitabu cha rejea katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Maisha ya Sala. Hiki ni chombo muhimu sana katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Katekesimu itawawezesha waamini kuzama kwa kina katika Mapokeo ya Kanisa, ili hatimaye, waweze kuwa tayari kuitangaza na kuishuhudia katika medani mbali mbali za maisha na wala kisiwe ni kitabu kinachoelea kwenye ombwe na fikira za binadamu! Mama Kanisa anataka kutangaza na kushuhudia mbiu ya wokovu, ili kwa kusikia watu waweze kusadiki, na kwa kusadiki waweze kutumaini na kwa kutumaini, waweze kupenda. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema,  kwa njia ya ufunuo, ukweli kamili juu ya Mwenyezi Mungu na juu ya wokovu wa mwanadamu unang’ara kwa binadamu katika Kristo Yesu, ambaye Yeye mwenyewe ndiye mshenga na utimilifu wa ufunuo wote.

Mtakatifu Paulo VI hapo tarehe 25 Julai 1968, alichapisha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu”. Ni waraka wa kinabii unaobainisha dhamana na wajibu wa wanandoa wanaoushiriki katika kazi ya uumbaji, ili kuendeleza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni dhamana ambayo inapaswa kumwilishwa katika furaha ya maisha na utume wao ndani ya familia. Papa Paulo VI alikuwa na upeo mpana na uwezo wa kuona mbali, akagundua changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa; akabainisha wajibu wa Kanisa kama Mama na Mwalimu na kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo ni kati ya mafundisho mazito ya Mtakatifu Paulo IV. Anakita mawazo yake katika dhamana na wajibu wa uumbaji, malezi, makuzi na elimu ya watoto. Wanandoa wanapaswa kufikiri, kujiandaa kikamilifu, kusindikizana na hatimaye, kupokea mtoto kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, dhamana inayowawajibisha! Hizi ni changamoto zilizoibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, zinazotaka waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema, sadaka na majitoleo binafsi. Mtakatifu Paulo VI alikuwa mwamba wa Injili ya familia na kamwe hakutikisika katika maamuzi na mafundisho yake ya kina!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 18 Oktoba 2018 amezindua kitabu cha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu” kilichoandikwa na Monsinyo Gilfredo Marengo, Rais wa Taasisi ya Yohane Paulo II kwa ajili ya Ndoa na Familia anasema, Mtakatifu Paulo VI alikuwa mwamba wa Injili ya familia na kamwe hakutikisika katika maamuzi na mafundisho yake ya kina! Ndiyo maana anakumbukwa kama “Papa wa familia” aliyekita mafundisho yake katika tasaufi ya Kikristo, wito na dhamana ya wazazi ndani ya familia, ili waweze kuwa mashuhuda wa upendo wa Kikristo, changamoto inayoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko licha ya matatizo, shida na changamoto katika maisha ya ndoa na familia! Kardinali Parolin anasema, Waraka huu wa kitume ulikabiliwa na changamoto kubwa kwa wakati huo baada ya kuibuka “dhana ya kudhibiti uzazi” ili kupunguza idadi ya watu duniani na baadhi ya wanataalimungu wakajikuta wakitumbukia katika mtego huu kwa kulitaka Kanisa kusoma alama za nyakati kwa kusahau kwamba, walikuwa wanakwenda kinyume cha Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Injili ya uhai, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Mtakatifu Paulo VI katika changamoto hii, akaonesha hekima ya kichungaji na kuungwa mkono na Kardinali Karol Wojtyla, aliyekuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia, Poland, ambaye baada ya kuteuliwa kwake kuliongoza Kanisa, akasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Mtakatifu Paulo VI amewawezesha waamini kutambua kwamba, Mafundisho ya Kanisa ni endelevu na daima, Kanisa linapenda kusoma alama za nyakati kwa kuzingatia amana na utajiri wa Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Kumbe, kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na mshikamano wa dhati kati ya taalimungu na shughuli za kichungaji; kati ya imani na uhalisia wa maisha! Kulinda Mafundisho tanzu ya Kanisa kunahitaji uaminifu kwa viongozi na upendo unaoshuhudiwa na waamini. Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu” ni ushuhuda endelevu wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaosimikwa katika upendo na uwajibikaji, utu na heshima ya wanandoa katika kutangaza na kushuhidia Injili ya familia kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Kwa bahati mbaya, wanasiasa wamejimwambafai na kujichukulia madaraka makubwa ya kuamua hatima ya utu wa binadamu na maisha yake, jambo ambalo anasema Kardinali Parolin, si sahihi ingawa linaendelea kutendeka hadi leo hii. Katika unyenyekevu wa kichungaji, Mtakatifu Paulo VI alitafuta ushauri kwa viongozi mbali mbali wa Kanisa na hatimaye akaibuka na ushuhuda wa Kanisa kwa kusema kwamba, uchungu na fadhaa ya mwanadamu anayeteseka hasa makini ni furaha, matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia!

Kanisa na Injili ya Uhai dhidi ya Utamaduni wa Kifo

 

24 March 2020, 11:10