Papa Francisko: Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo kwa Mwaka 2020 inaandaliwa na wafungwa kutoka Padua, nchini Italia! Papa Francisko: Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo kwa Mwaka 2020 inaandaliwa na wafungwa kutoka Padua, nchini Italia! 

Ijumaa kuu 2020: Njia ya Msalaba: Tafakari ni kuhusu Magereza!

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso, mahangaiko na matumaini ya wafungwa sehemu mbali mbali za dunia, ameamua kwa dhati kwamba, tafakari ya Ijumaa Kuu, Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo kwa Mwaka 2020, iandaliwe na wafungwa wanaotumikia adhabu yao kutoka katika magereza mawili yaliyoko mjini Padua, Kaskazini mwa Italia. WAFUNGWA!

Na Padre Richard Mjigwa, - Vatican.

Magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma ni uwanja maarufu sana uliokuwa unatumika kwa ajili ya kuwashindanishia binadamu na wanyama, kielelezo cha ukatili na mateso katika maisha ya mwanadamu. Mama Kanisa katika Ibada ya Ijumaa kuu kila mwaka anayatumia Magofu ya Colosseo kwa ajili ya kutafakari Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Yesu anawaambia wafuasi wake kwamba, mtu anayetaka kumwona, yaani kumwamini kwa dhati kabisa hana budi kumwangalia ndani kabisa ya Fumbo la Msalaba, ambalo linafunua utukufu na ukuu wake kama Mwana wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuyainua macho yao juu ya Msalaba wa Kristo ili kumtafakari na hatimaye, kumfahamu. Kwa bahati mbaya, Msalaba umekuwa ukitumiwa na baadhi ya watu kama “mapambo tu”, lakini kwa waamini, Msalaba ni ufunuo wa Fumbo la Mateso na Kifo cha Mwana wa Mungu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wa Mungu, chemchemi ya maisha mapya na wokovu kwa binadamu wa nyakati zote!

Kwa njia ya Madonda yake Matakatifu, watu wote wamepata kuponywa! Katika hali na mazingira kama haya, wajitahidi kuona na kuguswa na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, pale juu Msalabani, Kristo Yesu, ametundika mateso na mahangaiko ya binadamu wote. Akiwa ametundikwa Msalabani, watu wengi walimdhihaki, wakamtukana na kumdhalilisha; wakamchoma mkuki ubavuni, na hatimaye, akafa kifo cha aibu. Kristo Yesu katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi. Katika shida na mahangaiko ya binadamu, Kristo Yesu, aliweza kuhuzunika, akatoa machozi, akawa faraja na chombo cha baraka kwa wale waliokuwa wanamzunguka. Katika shida na magumu ya maisha, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, wawe wepesi kumkimbilia na kumwangalia Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani, ili kujiaminisha na kujikabidhi katika ulinzi na tunza yake. Yesu ni jibu makini katika mateso na mahangaiko ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso, mahangaiko na matumaini ya wafungwa sehemu mbali mbali za dunia, ameamua kwa dhati kwamba, tafakari ya Ijumaa Kuu, Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo kwa Mwaka 2020, iandaliwe na wafungwa wanaotumikia adhabu yao kutoka katika magereza mawili yaliyoko mjini Padua, Kaskazini mwa Italia. Baba Mtakatifu ameyasema haya katika barua aliyomwandikia Bwana Paolo Possamai, Mkurugenzi mkuu wa Gazeti la “Mattino di Padova”. Baba Mtakatifu anasema, lengo la Kanisa ni kutoa sauti kwa watu wasiokuwa na sauti, ili hata wao waweze kusikika. Tafakari hii itaratibiwa na Padre Marco Pozza na itawashirikisha kwanza kabisa wafungwa wenyewe; askari magereza, watu wa kujitolea, familia za wafungwa, mahakimu, wanasaikolojia wanaotoa ushauri kwa wafungwa, Kanisa, pamoja na raia wasiokuwa na hatia ambao wakati mwingine “wanabambikiziwa kesi” na matokeo yake ni kuishia magerezani.

Gereza ni mahali ambapo mtu anaonja udhaifu wake wa kibinadamu kwa kunyimwa uhuru. Lakini ni fursa ya kuweza kutubu na kumwongokea Mungu, ili baada ya Ijumaa kuu, aweze kufufuka tena. Baba Mtakatifu anasema, wokovu wa binadamu ni kazi ya umoja na mshikamano inayotekelezwa na Jumuiya ya waamini, kielelezo cha mshikamano wa upendo unaomwilishwa katika haki na huruma. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, tafakari ya Ijumaa kuu kuzunguka Magofu ya Colosseo kuandikwa na wafungwa. Gereza ni mtandao wa maisha unaowaunganisha: wafungwa, askari magereza, familia zao, watu wa kujitolea na wahudumu katika sekta mbali mbali za maisha. Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii kuzishukuru Parokia za Magereza kwa jitihada zao katika mchakato mzima wa uinjilishaji unaopania kuwapatia wafungwa fursa ya kutubu na kuongoka, tayari kuanza maisha mapya yanayofumbatwa katika imani, matumaini na mapendo.

Barua hii ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mkurugenzi mkuu wa Gazeti la “Mattino di Padova” ni kielelezo cha mshikamano wa huruma na upendo kwa wananchi wa Mkoa wa Veneto ulioko Kaskazini Mashariki wa Nchi ya Italia, kivutio kikuu cha watalii, ambao kwa sasa umegubikwa na mlipuko wa ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. 

Nia ya Msalaba 2020
11 March 2020, 13:00