Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini kujenga umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa kwa njia ya sala na Fumbo la Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini kujenga umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa kwa njia ya sala na Fumbo la Ekaristi Takatifu. 

Papa Francisko: Ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo: Sala na Ekaristi!

Umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, unarutubishwa kwa njia ya sala na Fumbo la Ekaristi Takatifu hata kama kutokana na sababu mbali mbali inashindikana kupata Komunio Takatifu, lakini Komunio ya kiroho inawezekana. Baba Mtakatifu anapenda kuuelekeza ujumbe huu kwa watu wanaojisikia pweke katika kipindi hiki cha mlipuko wa Virusi vya Corona, COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye Maktaba yake binafsi, Jumapili tarehe 15 Machi 2020, ametumia fursa hii kuwatakia waamini pamoja na watu wote waliokuwa wanafuatilia tafakari hii kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii kwa sababu wakati huu Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican umefungwa kama sehemu ya utekelezaji wa Itifaki ya mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Katika muktadha huu, unaowafanya watu wengi kuishi katika hali na mazingira ya upweke, Baba Mtakatifu anawaalika na kuwahamasisha kugundua ndani mwao tunu ya umoja na mshikamano inayowaunganisha watoto wote wa Kanisa.

Kwa kuungana na Kristo Yesu, kamwe hawatajisikia kuwa wapweke, bali wote kwa pamoja ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa na Yesu mwenyewe ndiye kichwa cha Fumbo la Mwili huu. Huu ni umoja unaorutubishwa kwa njia ya sala na Fumbo la Ekaristi Takatifu hata kama kutokana na sababu mbali mbali inashindikana kupata Komunio Takatifu, lakini Komunio ya kiroho inawezekana. Baba Mtakatifu anapenda kuuelekeza ujumbe huu kwa watu wanaojisikia pweke katika kipindi hiki cha mlipuko wa Virusi vya Corona, COVID-19.

Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu ameonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala kwa wagonjwa na wale wote wanaowahudumia. Anawakumbuka na kuwaombea watu wanaoendelea kujisadaka kwa kujitolea kuwahudumia watu ambao hawawezi kutoka majumbani mwao, bila kuwasahau wale wanaowahudumia maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa jitihada mbali mbali zinazotekelezwa na kila mmoja wao, katika kipindi hiki kigumu cha historia ya maisha ya watu wengi duniani. Wote hawa, amewapatia baraka zake za kitume na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya wagonjwa.

Papa: Fumbo la Kanisa: Sala na Ekaristi

 

15 March 2020, 10:19