Tafuta

Vatican News
Maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2020 ni Siku ya Mshikamano wa Sala nchini Italia, Papa Francisko naye anashiriki kikamilifu. Maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2020 ni Siku ya Mshikamano wa Sala nchini Italia, Papa Francisko naye anashiriki kikamilifu.  (Vatican Media)

Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wa Bikira Maria: Siku ya Sala!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Alhamisi, tarehe 19 Machi 2020 anajiunga na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI , saa 3: 00 Usiku kwa saa za Ulaya kukimbilia ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu katika kipindi hiki kigumu cha mlipuko wa ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu anawaalika waamini wote kusali Rozari Takatifu, Matendo ya Mwanga. Mt. Yosefu, Utuombee!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 19 Machi, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu. Yosefu anaitwa mtumishi mwaminifu wa Mungu, kwani uaminifu wake huo ndio ambao unamshirikisha kwa namna iliyositirika katika historia nzima ya wokovu. Matendo yake ya kiimani hayadhiiriki kwa wazi sana katika Maandiko Matakatifu lakini ni ya kupewa mkazo wa pekee, mathalani kwa kuwa mtii katika hali ya ukimya wakati wa kuitikia sauti ya Mungu. “Huyu ndiye wakili mwaminifu na mwenye busara”. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linamwadhimisha Mtakatifu Yosefu katika maisha ya kila siku, katika juhudi, bidii na maarifa kazini; kwa kusimama kidete kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kuendelea kumtumainia Mungu wakati wa raha na shida!

Mtakatifu Yosefu alikuwa na upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu na akaonekana kuwa ni mtu mwaminifu na mwenye busara. Baba Mtakatifu anasema, Alhamisi, tarehe 19 Machi 2020 saa 3:00 Usiku kwa Saa za Ulaya, anajiunga na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kukimbilia ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu katika kipindi hiki kigumu cha mlipuko wa ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu anawaalika waamini wote kusali Rozari Takatifu, Matendo ya Mwanga, ili kwa maombezi ya Bikira Maria na kwa njia ya Kristo, watu wa Mungu waweze kupata hifadhi na usalama dhidi ya ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa maombezi ya Familia Takatifu ya Yosefu, Maria na Yosefu! Siku hii, iwe ni kielelezo cha umoja na mshikamano katika mambo matakatifu!

Mtakatifu Yosefu

 

18 March 2020, 15:36