Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, kujiunga pamoja naye ili kumlilia Mwenyezi Mungu aweze kuwanusuru watu wake na janga la ugonjwa wa Corona. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, kujiunga pamoja naye ili kumlilia Mwenyezi Mungu aweze kuwanusuru watu wake na janga la ugonjwa wa Corona. 

Papa Francisko: Ungana na Papa: #PrayForTheWorld. 25 Machi 2020

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kujiunga pamoja naye Siku ya Jumatano tarehe 25 Machi 2020 kwa ajili ya Kusali Sala ya Baba Yetu, ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwanusuru watu wake na janga la ugonjwa wa Corona. Ijumaa tarehe 27 Machi 2020, ataongoza Ibada ya Kuabudu Sakramenti Kuu na hatimaye, atatoa baraka: Urbi et Orbi

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, kujiunga naye Jumatano tarehe 25 Machi 2020, majira ya saa 6:00 za mchana kwa saa za Ulaya, sawa na Saa 8: 00 Adhuhuri kwa saa za Afrika Mashariki, kwa ajili ya kuomba ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hii ni Siku maalum ambamo Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu. Ijumaa tarehe 27 Machi 2020, Saa 12:00 za Jioni kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 2: 00 Usiku kwa Saa za Afrika mashariki, Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuongoza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, itakayokuwa na tafakari ya Neno la Mungu, Sala na Maombi na hatimaye, atatoa baraka kwa Sakramenti kuu ya Ekaristi Takatifu kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake yaani “Urbi et Orbi”. Katika kipindi hiki, Baba Mtakatifu atatoa Rehema kamili kwa waamini waliojiandaa barabara na kutimiza masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa namna ya pekee kabisa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaoendelea kufunga na kusali kwa ajili ya kuomba huruma ya Mungu dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 bila kujali, dini, imani na mapokeo yao. Sala hii ya pamoja kwa watu wa Mungu inapatikana kwa kufuata #PrayForTheWorld. Mwenyezi Mungu awaangalie waja wake kwa jicho la huruma na kuwasaidia katika kipindi hiki kigumu, kumwilisha huruma na upendo, kama kielelezo cha uwepo wa karibu kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na ugonjwa huu hatari. Njia za mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii, iwasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwafikia wale wote wanaoteseka kutokana na ugonjwa huu. Baba Mtakatifu anasema, hiki ni kipindi cha kuonesha umoja, upendo na mshikamano kwa kujikita katika huruma na wema. Umoja na mshikamano huu uonekane kwa wale wote walioathirika. Mama Kanisa anapenda kuwa karibu zaidi na madaktari, wafanyakazi katika sekta ya afya, wauguzi pamoja na watu wa kujitolea. Umoja huu uwaguse hata viongozi wenye mamlaka mbali mbali, wanaoweka sera na mikakati kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

Umoja huu uwe ni kielelezo cha mshikamano na vikosi vya ulinzi na usalama, vinavyosimamia ulinzi na usalama wa watu na mali zao pamoja na kutekeleza sera na mikakati ya kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Tangu kuibuka kwa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 mwishoni mwa Mwezi Desemba 2019, tayari ugonjwa huu umekwisha kusambaa katika nchi 162 na zaidi ya watu 290, 000 wameambukizwa na zaidi ya watu 12, 000 wamekwisha kufariki dunia. Ni kutokana na muktadha huu, Shirika la Afya Duniani, WHO tarehe 11 Machi 2020 likatangaza kwamba, ugonjwa huu ni janga la kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake ameendelea kuwa karibu na waathirika wote wa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa sala, tafakari na uwepo wake wa karibu. Sala: Tunakimbilia ulinzi wako mzazi Mtakatifu wa Mungu usitunyime tukiomba katika shida zetu tuopoe siku zote kila tuingiapo hatarini, Ee Bikira Mtukufu na mwenye baraka. Amina.

Papa: Sala Maalum
25 March 2020, 08:06