Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 18 Machi 2020 ametafakari kuhusu: Heri za Mlimani: Huruma na Msamaha ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 18 Machi 2020 ametafakari kuhusu: Heri za Mlimani: Huruma na Msamaha ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana. 

Baba Mtakatifu Francisko: Huruma ya Mungu ni kiini cha Ukristo!

Huruma ya Mungu ni tema ambayo ni kielelezo cha maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huruma na msamaha ni tunu msingi ambazo Baba Mtakatifu anapenda kuona zikimwilishwa katika maisha ya waamini. Huruma ya Mungu ni kielelezo cha udhaifu wa binadamu na kwamba, daima binadamu wanapaswa kuhurumiana na kusameheana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waamini wanaalikwa kuliishi kikamilifu Fumbo la Ukombozi kwa kutafuta faraja kutoka kwa Roho Mtakatifu bila ya kuchanganya mambo. Hotuba ya Mlimani au Heri za Mlimani zilizotangazwa na Yesu ni: dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo. Ni muhtasari wa Mafundisho yake makuu kwa wanafunzi wake. Anawataka kwa namna ya pekee wawe na huzuni na umaskini wa roho; wawe na njaa na kiu ya haki; wawe na rehema, wenye moyo safi na wapatanishi. Heri nane ni faraja ya Roho Mtakatifu kwa wale ambao wamekombolewa na kuweka mioyo yao wazi kwa ajili ya kupokea neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, wako huru. Heri za Mlimani ni chemchemi ya furaha ya upendo aminifu wa Mungu unayobubujikia maisha ya waamini! Hii ni furaha endelevu ambayo hakuna mtu wala mazingira yanayoweza kuwapokonya watoto wapendwa wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Heri za Mlimani, aliyoitoa Jumatano, tarehe 18 Machi 2020 anasema, “Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema” Mt. 5:7. Kwa hakika waamini hawa watakuwa ni mashuhuda na vyombo vya upendo na huruma ya Mungu. Huruma na msamaha ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu na maisha ya Mwenyezi Mungu. Katika Injili ya Luka, 6:37, Yesu anasema “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Naye Mtakatifu Yakobo, Mtume katika Waraka wake anasema, “Maana hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma. Huruma hujitukuza juu ya hukumu.

Waamini katika Sala ya Baba Yetu, wanamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwasamehe makosa yao kama wanavyowasamehe wengine. Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kutoa na kupokea msamaha ni sawa na chanda na pete, mambo ambayo yanategemeana na kukamilishana katika maisha ya mwanadamu. Lakini, jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, kuna watu wengi ambao wanashindwa kabisa kusamehe na kusahau, lakini inawezekana kabisa kusamehe na hata kupokea msamaha kutoka kwa wengine. Jambo la msingi ni kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kuweza kupata rehema na msamaha wa dhambi kutoka kwake.

Watu wote bila ubaguzi ni wadeni mbele ya Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na mkarimu kwa wote wanaomwendea kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani. Watu wajifunze kusamehe na kusahau, kwa kutambua kwamba, hapa ulimwenguni hakuna mtu ambaye ni mkamilifu, kwani kila mtu anahitaji huruma ya Mungu. Udhaifu wa binadamu ni msingi wa kusamehe kwa kutumia kipimo kile kile wanachowapia wengine. Kwa kutoa na kupokea msamaha ni tendo linalojikita katika unyenyekevu. Ndiyo maana Mwenyezi Mungu anachukua hatua ya kwanza ya kusamehe. Kwa kupokea msamaha wake, waamini wanakirimiwa uwezo wa kusamehe pia, kiasi kwamba, udhaifu wao unakuwa ni njia inayowafungulia Ufalme wa Mungu, mintarafu kiwango cha Mungu ambaye ni mwingi wa huruma.

Waamini wanapojitahidi kunafsisha upendo wa Mungu katika maisha yao, hata wao wanageuka kuwa ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa kupenda zaidi. Huruma ya Mungu ni kiini cha maisha ya Kikristo. Kumbe, maisha ya Kikristo iwe ni hija inayowapeleka waamini kwenye kisima cha huruma ya Mungu. Huruma ya Mungu ni chanzo na kilele cha hija ya maisha ya Kikristo. Matunda ya upendo ni furaha, amani na huruma. Huruma ya Mungu ni tema ambayo ni kielelezo cha maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huruma na msamaha ni tunu msingi ambazo Baba Mtakatifu anapenda kuona zikimwilishwa katika maisha ya waamini. Huruma ya Mungu ni kielelezo cha udhaifu wa binadamu na hakuna anayeweza kuishi bila ya huruma na msamaha; daima binadamu wanapaswa kuhurumiana na kusameheana!

Papa: Huruma ya Mungu

 

18 March 2020, 16:28