Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 15 Machi 2020 amefanya hija kwa kutembelea Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu na Kanisa la "San Marcello" ili kuomba huruma ya Mungu dhidi ya virusi vya Corona. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 15 Machi 2020 amefanya hija kwa kutembelea Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu na Kanisa la "San Marcello" ili kuomba huruma ya Mungu dhidi ya virusi vya Corona.  (ANSA)

Papa Francisko afanya hija ili kusali na kuomba huruma ya Mungu dhidi ya Virusi vya Corona

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwaombea wagonjwa ili wapone, anawatia moyo waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Amewaombea faraja, amani na utulivu wa ndani, wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa mlipuko wa Virusi vya Corona, COVID-19 ambalo kwa sasa limetangazwa kuwa ni janga la Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, amesema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 15 Machi 2020 majira ya Saa 10: 00 za jioni alikwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Mkuu, ili kuomba ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi, “Salus popoli Romani” katika kipindi hiki kigumu cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19, sehemu mbali mbali za dunia. Baadaye, Baba Mtakatifu akitembea kwa miguu kwenye barabara ya “Del Corso” kama kielelezo cha hija ya kiroho, amekwenda na kusali kwenye Kanisa kuu la “San Marcello” lililoko kwenye barabara ya “Del Corso”. Ndani ya Kanisa hili kunahifadhiwa Msalaba wa Miujiza uliotumika kwa maandamano makubwa ya toba na wongofu wa ndani kunako mwaka 1522 ili kuomba huruma ya Mungu kutokana na maambukizi makubwa yaliyokuwa yamesababishwa na mlipuko wa ugonjwa wa Tauni mjini Roma.

Baba Mtakatifu katika sala zake, amemwomba Mwenyezi Mungu awaangalie watu wake kwa macho ya huruma, ili hatimaye, aweze kusitisha ugonjwa huu unaoendelea kupukutisha maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anaendelea kuwaombea wagonjwa ili wapone, anawatia moyo waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Amewaombea faraja, amani na utulivu wa ndani, wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa mlipuko wa Virusi vya Corona, COVID-19 ambalo kwa sasa limetangazwa kuwa ni janga la Kimataifa. Baba Mtakatifu amewaombea wafanyakazi katika sekta ya afya, vikosi vya ulinzi na usalama na wale wote ambao katika kipindi hiki kigumu cha karantini, wanaendelea kutoa huduma muhimu, ili kuiwezesha jamii kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Baba Mtakatifu Francisko ana ibada ya pekee sana kwa Bikira Maria, Afya ya Warumi, “Salus populi Romani”. Baba Mtakatifu kabla na baada ya hija zake au anapokabiliwa mbele yake na matukio makuu ya Kikanisa, hupenda kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi.

Si mara ya kwanza, viongozi wa Kanisa kukimbilia huruma ya Mungu kwa ajili ya kuwaombea watu wanapokabiliwa na milipuko ya magonjwa. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo, Mtakatifu Yohane Paulo II, alitumia Msalaba wa Miujiza katika kuhitimisha Siku ya Toba, Wongofu wa ndani na Msamaha. Huu ni Msalaba uliosalimika baada ya Kanisa kuu la “San Marcello” kukumbwa na janga la moto tarehe 23 Mei 1519, Msalaba huu ukabaki bila kuguswa na moto hata kidogo. Tukio hili liliwagusa waamini wengi wa nyakati zile. Baada ya miaka mitatu, kunako mwaka 1522 mji wa Roma ulikumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa Tauni. Msalaba huu, ukatembezwa kwenye vitongoji mbali mbali vya Roma kwa muda wa siku kumi na sita, yaani kuanzia tarehe 4 hadi 20 Agosti 1522. Mlipuko wa ugonjwa wa Tauni, ukakoma na watu wakapata amani. Hizi zilikuwa ni jitihada zilizofanywa na Kardinali Raimondo Vic. Silaha za mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 ni: taratibu, kanuni na sheria za kisayansi; imani, matumaini na mapendo!

Si haba, kuona waamini na watu mbali mbali wanahimizwa kufunga, kusali na kufanya toba, kama njia ya kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake katika kipindi hiki kigumu cha shida na mahangaiko makubwa: kiroho na kimwili kutokana na kusambaa kwa kasi kubwa Virusi vya Corona, COVID-19.

Papa: Via Del Corso

 

16 March 2020, 11:19