Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika Liturujia ya toba na upatanisho kwa wakleri wa Jimbo kuu la Roma amegusia machungu ya maisha, utume na wito wa mapadre! Baba Mtakatifu Francisko katika Liturujia ya toba na upatanisho kwa wakleri wa Jimbo kuu la Roma amegusia machungu ya maisha, utume na wito wa mapadre!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Tafakari kuhusu machungu ya maisha ya Mapadre!

Baba Mtakatifu ametaja mambo makuu yanayopelekea wakleri kuwa na machungu katika maisha, wito na utume wao: jambo la kwanza ni matatizo ya imani, pili ni matatizo na Askofu mahalia; tatu ni matatizo kati ya wakleri wenyewe kutokana na upweke hasi, kushindwa kuheshimu na kuthamini neema iliyoko ndani mwao; pamoja na kushindwa kuwaheshimu na kuwathamini wengine!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari iliyosomwa kwa niaba yake na Kardinali Angelo De Donatis, Makamu wa Askofu Jimbo kuu la Roma, Alhamisi tarehe 27 Februari 2020, wakati wa Liturujia ya Upatanisho kwa ajili ya wakleri wa Jimbo kuu la Roma kama mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2020, ametafakari kuhusu: machungu yanayojitokeza katika maisha ya wakleri. Tafakari hii ni matunda ya utamaduni wa kusikiliza kwa dhati maoni yaliyotolewa na baadhi ya Majandokasisi na Wakleri kutoka majimbo mbali mbali ya Italia. Pili, anasema Baba Mtakatifu kwamba, sehemu kubwa ya wakleri anaowafahamu wameridhika na wanaendelea kufurahia maisha, wito na utume wao wa Kipadre. Machungu na magumu yanayozungumziwa hapa ni sehemu ya maisha na utume wa Wakleri. Huu ni mwangwi wa maoni ya Majandokasisi na Wakleri na wala si maoni ya Baba Mtakatifu Francisko mwenyewe kama sehemu ya ubinadamu wa wakleri!

Baba Mtakatifu ametaja mambo makuu yanayopelekea wakleri kuwa na machungu katika maisha, wito na utume wao: jambo la kwanza ni matatizo ya imani, pili ni matatizo na Askofu mahalia; tatu ni matatizo kati ya wakleri wenyewe kutokana na upweke hasi, kushindwa kuheshimu na kuthamini neema iliyoko ndani mwao; pamoja na kushindwa kuwaheshimu na kuwathamini wakleri wengine. Baba Mtakatifu anawaalika wakleri kuyaangalia machungu na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha, wito na utume wao wa Kipadre, kwa kutambua kwamba, kwanza kabisa wao ni wadhambi waliosamehewa dhambi zao na kutumwa, changamoto na mwaliko kwa wakleri kutumia fursa hii kujizatiti zaidi katika Ibada ya kumwabudu Mwenyezi Mungu, ili kuonja tena nguvu ya huruma na upendo wa Mungu!

Baba Mtakatifu anasema, Wakleri wengi wanaokumbana na machungu katika maisha, wito na utume wao wa Kipadre ni kutokana na matatizo na changamoto za kiimani, kwa kushindwa kujiaminisha kwa Kristo Yesu kama ilivyokuwa kwa wale wafuasi wa Emau, waliokata tamaa na kukosa matumaini kutokana na mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Ili kukaniliana na changamoto hii, kuna haja ya kujenga utamaduni wa kusali daima, ili kupata nafasi ya kugundua matumaini na mambo yanayotarajiwa. Uhusiano na mafungamano tenge na Mwenyezi Mungu ni kati ya matatizo makubwa yanayowakumba Wakleri katika ulimwengu mamboleo, ikilinganishwa na siku ile walipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kufifia kwa moyo wa sala kunasababisha machungu katika maisha na utume wa mapadre na matokeo ya haya machungu haya wanaambukizwa hata waamini wanaowaongoza.

Wakleri wanapaswa kujizatiti kikamilifu katika maisha ya Sala na Ibada kwa Mwenyezi Mungu. Haya ndiyo mapambano ya maisha ya kiroho kwa kujiachia na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu badala ya Mapadre kutaka kujimwambafai kwa kudhani kwamba, wanaweza kujitegemea na kujitosheleza wenyewe pasi na neema ya Mwenyezi Mungu. Heri za Mlimani, ziwe ni nguzo katika maisha, wito na utume wa Wakleri. Mapadre wajenge utamaduni wa kusikiliza na kutathmini historia ya maisha yao katika mwanga wa Neno la Mungu, kama ilivyojitokeza baadaye kwa wafuasi wa Emau walipokutana na Kristo Yesu Mfufuka akawafunulia siri ya furaha ya Maandiko Matakatifu. Machungu haya yanapaswa kusikilizwa na kushughulikiwa kikamilifu. Wakleri wasipende kujiamini kupita kiasi, wakasahau kwamba, wameweka Agano na Mwenyezi Mungu. Wajifunze kuwa wapole na wanyenyekevu; kwa kutokubali kumezwa na malimwengu, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Kwa njia hii machungu ya maisha, wito na utume wa Kipadre yatageukwa kuwa ni chemchemi furaha, imani na matumaini thabiti!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, sababu nyingine kubwa ni matatizo na Maaskofu mahalia, wanaotwishwa matatizo, shida na changamoto za mapadre na kusahau kwamba, wao wenyewe ndio chanzo cha matatizo haya kwa kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu. Ni watu wanaoshindwa kutambua karama, udhaifu na mapungufu yao, kama ilivyojionesha kwa Adamu kwa kumtupia Eva lawama zote za kuanguka kwake katika dhambi ya asili. Ikumbukwe kwamba, hata Askofu mahalia anayo haki ya kukosea kama ilivyo kwa watu wote. Shida kubwa ni baadhi ya Mapadre kushindwa kupokea mawazo na maoni ya watu wengine, tofauti na mawazo au maoni yao. Matokeo yake mambo ya msingi kama imani na ubatizo mmoja na Mwenyezi Mungu Baba wa wote, yanaanza kutoweka taratibu na huo ni mwanzo wa kuporomoka kwa mahusiano na mafungamano kati ya Askofu mahalia na mapadre wake.

Umoja na mshikamano na Askofu mahalia ni jambo la msingi linalopaswa pia kusimikwa katika utu na heshima. Askofu mahalia kabla ya kufanya maamuzi makubwa katika maisha na utume wa Mapadre, ajitahidi kuchunguza hali halisi pamoja na kutafuta ushauri wa kina kwa kuzingatia busara, usawa kwa kusikiliza maoni ya wote wanaohusika na hatimaye kufanya mang’amuzi. Askofu ajenge utamaduni wa kuwasikiliza Mapadre wake, watawa na waamini walei. Lengo ni kupata maoni tofauti na wala si kuwa na mawazo sawa! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, katika miaka ya hivi karibuni, wakleri wametumbukia katika kashfa mbali mbali za kifedha na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Hali hii imeleta ukakasi katika mahusiano na mafungamano kati ya wakleri wenyewe! Katika hali na mazingira kama haya, kuna baadhi ya wakleri wanajiona kuwa ni “wakeleketwa, wana mapinduzi na watakatifu wa Mungu” kiasi hata cha kushindwa kuchangama na “wakleri wadhambi” wanaochafua maisha na utume wa Kanisa.

Ikumbukwe kwamba, Kanisa linaundwa na watakatifu pamoja na wadhambi wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu. Bila kukubali uhalisia huu, Mapadre wengi watakosa amani na matokeo yake wataendelea kila siku kuzama katika machungu na mahangaiko ya ndani. Dhambi jamii zimegumisha sana maisha, wito na utume wa Kipadre. Malezi na majiundo endelevu yasaidie kujenga na kudumisha umoja na udugu miongoni mwa wakleri, ili kujenga Jumuiya za Mapadre zinazosimikwa katika umoja, udugu na upendo, kwa kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kama ndugu wamoja katika Daraja Takatifu. Mapadre wajitahidi kushinda upweke hasi, kwa kujiundia mazingira ya upweke chanya utakaowawezesha kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu, kwa njia ya sala. Mapadre wajitahidi kutafuta muda binafsi ili kukaa peke yao mbele ya Mwenyezi Mungu ili kuzungumza naye kwa kina na mapana! Upweke hasi mara nyingi unawapelekea Mapadre kutafuta faraja nje ya maisha, wito na utume wao!

Hali ya wakleri kuanza kujitenga na kutumbukia katika upweke hasi inajionesha kwa kwa wakleri kushindwa kuheshimu neema na baraka zinazobubujika kutoka katika maisha, wito na utume wa Kipadre na matokeo yake ni kupoteza dira na mwelekeo wa Kipadre. Kushindwa kuheshimu na kuthamini historia ya maisha ya watu na mazingira yao kwa kutaka kuyafanya yote mapya ni hatari. Wakleri wajenge utamaduni wa kuendeleza mazuri yaliyotendwa na watangulizi wao! Waboreshe mapungufu yaliyojitokeza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wakleri wajenge utamaduni wa kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kama ndugu katika Daraja Takatifu. Wasaidiane wakati wa raha na shida! Vinginevyo ni baadhi ya wakleri kujifungia katika ubinafsi wao na “kuanzisha kambi ya upinzani”.

Wakleri wajifunze kujenga dhamiri nyofu kwa kutambua udhaifu wao, tayari kukiri na kuomba msamaha; wawe tayari pia kukuza na kuendeleza karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Watambue kwamba, Shetani, Ibilisi yupo na anataka kuwapekenyua na kuwasambaratisha! Mashindano yasiyokuwa na tija wala mashiko ni chachu ya upweke hasi. Kuna Jumuiya pasi na umoja, upendo, mshikamano na ushirikiano, “watu wanapishana kama Meli Baharini”. Wakleri waone fahari ya kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha badala ya kutaka kutambuliwa na kupigiwa magoti! Mapadre wanapaswa kutambua kwamba, waamini walei wanawafahamu vizuri zaidi kuliko hata wao wenyewe wanavyojifahamu. Kuna watu wanaowaheshimu na kuwathamini sana, kwa kusali na kuwasindikiza katika hija ya maisha, wito na utume wao. Wanatambua machungu, shida na changamoto za maisha na daima wako tayari kuwaombea wakleri wao.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika wakleri kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwasaidia kutambua mambo msingi yanayowaletea machungu katika maisha, ili waweze kujipatanisha ili wapatanishe wengine; kwa kuwa na amani, ili kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani kwa jirani zao; watu wa matumaini wanaosambaza matumaini kwa wale waliokata tamaa. Watu wa Mungu wanatarajia kuwaona wakleri wakiwa kweli ni waalimu wa maisha ya kiroho, wenye uwezo wa kuwaonesha watu visima vya maji baridi katika jangwa la maisha yao ya kiroho!

Papa: Machungu ya Mapadre

 

 

27 February 2020, 16:20