Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima: Alama kuu ni mavumbi na majivu! Kifo na Maisha mapya katika Kristo Yesu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima: Alama kuu ni mavumbi na majivu! Kifo na Maisha mapya katika Kristo Yesu! 

Papa Francisko: Jumatano ya Majivu: Mavumbi na maisha mapya katika Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu amefafanua kuhusu majivu, umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, maana ya maisha na hatimaye kifo. Kipindi cha Kwaresima ni wakati muafaka wa kuondokana na unafiki, ili hatimaye, kuweza kusali vyema, kufunga, kutafakari na kutenda matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Lengo ni kupatanishwa na Mungu na jirani ili kuadhimisha vyema Fumbo la Pasaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maandamano kutoka katika Kanisa kuu la Mtakatifu Anselmi na hatimaye, maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina pamoja na waamini kupakwa majivu, Jumatano ya Majivu ni mapokeo ya kale yaliyopania kuimarisha imani na kudumisha umoja wa Kanisa, hasa katika kipindi cha Kwaresima, mwanzo wa safari katika Jangwa la maisha ya kiroho! Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano ya Majivu, tarehe 26 Februari 2020 ameongoza maandamano na hatimaye, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina, Jimbo kuu la Roma! Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amefafanua kuhusu majivu, umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, maana ya maisha na hatimaye kifo. Kipindi cha Kwaresima ni wakati muafaka wa kuondokana na unafiki, ili hatimaye, kuweza kusali vyema, kufunga, kutafakari na kutenda matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Ili kufikia lengo la kupata neema na utakatifu wa maisha, waamini wanahamasishwa kupatanishwa na Mungu kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka linalopyaisha maisha ya waamini katika Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Baba Mtakatifu anasema, Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima. Majivu yanawakumbusha waamini kwamba, wametolewa katika mavumbi, lakini wanapendwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, wana thamani kubwa sana mbele ya Mungu kwa sababu wao ni matumaini ya Mungu, amana na furaha yake Majivu yanawakumbusha waamini kwamba, safari ya maisha yao inaanza katika mavumbi, changamoto na mwaliko wa kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaunda. Kwa bahati mbaya mwanadamu anapokabiliwa na shida, magumu na changamoto za maisha mbele yake anaona mavumbi peke yake.

Mwenyezi Mungu anaendelea kuwatia shime kwamba, hata katika hali hii bado wanayo thamani kubwa mbele ya macho yake. Hii inatokana na ukweli kwamba, mwanadamu amezaliwa kwa ajili ya kupendwa na kwamba, wao ni watoto wa Mungu. Papa Francisko anasema, Kipindi cha Kwaresima si wakati wa “kuwashindilia watu kanuni maadili na utu wema”, bali ni fursa ya kutambua kwamba, wao ni mavumbi na wanapendwa na Mwenyezi Mungu. Ni kipindi cha neema, ili kuguswa na upendo wa Mungu, kwa kusonga mbele, ili kujizatiti zaidi katika upyaisho wa maisha. Huu ni mwaliko kwa waamini kutoka katika mavumbi na kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya, katika matumaini bila ya kujikatia wala kukatishwa tamaa kutokana na ubaya unaojidhihirisha ulimwenguni, woga na wasi wasi. Lakini hata katika hali kama hii, bado Mwenyezi Mungu anayo nafasi ya kubadili mavumbi ya mwanadamu kuwa ni sehemu ya utukufu wake.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa kina umuhimu wa maisha yao na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu kutokna na uchu wa mali, fedha, utajiri wa haraka haraka na madaraka. Kwani kwa kufanya hivi wakumbuke daima kwamba wao ni mavumbi. Waamini wajitahidi kuratibu vyema maisha yao; wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo kwa Mungu na jirani zao. Binadamu anayo thamani kubwa kwani wanapaswa kutekeleza ndoto ya Mungu yaani upendo. Majivu waliyopakwa waamini vichwani mwao, yasaidie kuwasha moto wa upendo, kama tiketi ya kuendea mbinguni. Mali za dunia hii, “haziwezi kufua dafu” kwa ajili ya kwenda mbinguni, bali upendo walioshuhudia kwenye familia zao, mahali pa kazi, ndani ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake ndio utakaowaokoa kwa sababu unadumu milele yote! Majivu yawakumbushe waamini maisha ni safari kutoka mavumbini na kwamba, watarudi tena mavumbini. Leo hii watu wengi wanarudishwa mavumbini kutokana na majanga, vita, vitendo vya utoaji mimba pamoja na wazee kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Watu wanarejeshwa mavumbini kutokana na mahusiano tenge ndani ya familia, kinzani na mipasuko mbali mbali; kwa kukosa kuomba na kutoa msamaha wa kweli, tayari kuanza maisha mapya. Lakini kwa bahati mbaya, watu wengi ni wepesi kudai haki zao na wala hawana upendo wa dhati; mambo yanayohatarisha zawadi ya maisha. Hata ndani ya Kanisa bado kuna vumbi kubwa la watu kumezwa na malimwengu. Waamini wanaendelea kuchafua upendo wa Mungu kwa majivu ya unafiki. Baba Mtakatifu anakaza kusema, haitoshi kutenda matendo ya huruma, kusali na kufunga, ikiwa kama bado kuna watu wanaotaliwa na unafiki pamoja na ubinafsi. Kwa hakika maneno yanapaswa kudhihirishwa kwa vitendo! Mawazo ya ndani yadhiirishwe kwa njia ya maisha ya nje, ili kweli mavumbi yasichafue na wala majivu yasizime moto wa upendo wa Mungu.

Ni katika muktadha wa mazingira haya, Mtume Paulo anasema: “twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: mpatanishwe na Mungu” kwa sababu utakatifu ni neema ya Mungu. Ni kwa njia hii, Mwenyezi Mungu anaweza kuwasaidia waja wake kuondoa mavumbi kutoka katika sakafu ya nyoyo zao. Kristo Yesu anazifahamu fika nyoyo za waja wake na anao uwezo pia wa kuzingaza na kuziponya. Kwaresima ni kipindi cha kuganga na kuponya undani wa maisha ya kiroho. Maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Fumbo la Pasaka iwe ni fursa ya kutoka mavumbini na kuelekea katika maisha mapya, kwa kuonja: huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Kristo! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujipatanisha na Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, inayopyaisha maisha na kutakasa undani wa maisha yao. Upatanisho na Mungu utawasaidia kuishi kama watoto wapendwa wa Mungu; wadhambi waliosamehewa; wagonjwa walioponywa, na waliopotea njia, kupata kiongozi. Waamini wajiachilie mbele ya Mwenyezi Mungu ili awapende nao waweze kupenda. Wawe na ari ya moyo wa kusimama kuelekea katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Kwa njia hii watakuwa na furaha ya kugundua kwamba, Mwenyezi Mungu ana uwezo wa kuwafufua tena kutoka katika majivu yao!

Papa: Mahubiri J5 ya Majivu
27 February 2020, 15:55