Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yanapaswa kudhibitiwa na: kanuni maadili na utu wema, elimu makini na sheria! Papa Francisko asema, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yanapaswa kudhibitiwa na: kanuni maadili na utu wema, elimu makini na sheria! 

Papa: Maendeleo ya Teknolojia: Akili Bandia: Muhimu: maadili, elimu na sheria madhubuti!

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wajumbe wa Mkutano mkuu wa 26 wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha amegusia kuhusu maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa kidigitali. Lakini ameonya kwamba, kuna haja ya kujizatiti kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema; elimu makini ili kuunda dhamiri nyofu pamoja na sheria ili kuratibu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa kidigitali, yamesaidia maboresho makubwa katika matumizi ya “akili bandia” katika sekta mbali mbali za maisha ya mwanadamu iwe kwa mtu binafsi au jamii katika ujumla wake. Mapinduzi haya makubwa ya teknolijia yanawawezesha watu kujifahamu sanjari na kuufahamu ulimwengu unaowazunguka, kiasi hata cha kuathiri maamuzi, uwezo wa kufiki na kutenda katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Leo hii utashi wa mwanadamu unaathiriwa kwa namna ya pekee na matumizi ya “akili bandia” kutokana na mchango wake mkubwa!

Hii ni sehemu ya hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko, iliyosomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya maisha, Ijumaa tarehe 28 Februari 2020. Hotuba hii ni mchango wa maadhimisho ya Mkutano mkuu wa ishirini na sita unaojikita katika matumizi ya “artificial intelligence” yaani “akili bandia” kwa ajili ya huduma ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hususan katika sekta ya afya. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewataka wadau mbali mbali katika ulimwengu wa kidigitali kupembua kwa kina na mapana mchango wa “akili bandia” katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu na hususan katika baiolojia. Kuna haja ya kuendeleza majadiliano na wadau mbali mbali katika ulimwengu wa kidigitali; Umuhimu wa kulea ili kuwa na dhamiri iliyokomaa pamoja na kuratibu mwingiliano wa mchakato wa maendeleo unaozingatia na kuheshimu kanuni maadili na utu wema!

Baba Mtakatifu anasema, historia ya maendeleo ya mwanadamu imekwisha kupiga hatua kubwa tangu ugunduzi wa mashini pamoja na hifadhi ya habari kwa wakati huu. Haya ni matunda ya mwingiliano wa sayansi katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu kiasi cha kufikia hatua ya kutenganisha au kuunganisha mambo katika uhalisia wake au katika ulimwengu wa kufikirika. Ulimwengu wa kidigitali umemwezesha mwanadamu kupata mang’amuzi mapya kuhusu: nafasi, muda na kuhusu mwili wa madamu. Katika masuala ya kiuchumi na kijamii, watumiaji wa teknolojia hii wamegeuzwa kuwa ni walaji wa kupindukia, kiasi kwamba, mafao ya watu wengi yamo mikononi mwa watu wachache. Ulimwengu wa kidigitali unaendelea kuratibu mahusiano ya watu kwa ajili ya masuala ya kibiashara au kisiasa bila hata ya watumiaji wenyewe kujitambua.

Baba Mtakatifu anakaza kusema kwamba, kuja haja ya kuwa na utambuzi mpana zaidi ili watu waweze kutumia vyema uhuru wao, badala ya amana na utajiri huu kuhodhiwa na watu wachache ndani ya jamii. Matumizi ya “akili bandia” katika masuala ya Kibaiolojia yamepelekea mabadiliko makubwa katika uelewa na uratibu wa maisha ya viumbe hai na kwa namna ya pekee maisha ya binadamu. Kuna tofauti kubwa ya uzoefu wa maisha kwa njia ya hisia na hali halisi. Kanuni maadili na utu wema ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika maisha ya binadamu. Ili kuweza kukabiliana na changamoto hii kuna haja ya kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi kati Nyanja mbali mbali za maisha ya binadamu, ili kuweza kutoa majibu muafaka. Uwepo wa wadau na wakuu mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa katika mkutano huu ni mwaliko wa kujenga utamaduni wa kusikilizana, ili kuunganisha mang’amuzi na tafakari makini.

Waamini kwa njia ya Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kiimani wanaweza kusaidiwa kutambua njia bora zaidi ya kufuata na kwa kujikita katika uinjilishaji, wakaendelea kutemba kwa pamoja. Kwa njia hii, wataweza kukuza na kudumisha majadiliano na kuendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza, kwa kuzingatia pia maendeleo ya maisha yake ya kiroho pamoja na kuishirikisha familia ya binadamu katika ujumla wake! Watu wafundishwe kuwa na matumizi bora na sahihi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwa sababu yanaacha athari zake katika dhamiri na tunu msingi za maisha ya binadamu, daima mafao ya wengi yakipewa msukumo wa pekee. Kamwe mwanadamu asigeuzwe kuwa ni kichokoo cha maendeleo ya sayansi. Kuna haja ya kuunda Taasisi za Kimataifa zitakazokazia pamoja na mambo mengine kanuni maadili na utu wema kwa walimu na watumiaji wa sayansi na maendeleo ya teknolojia katika ulimwengu wa kidigitali.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, uwajibikaji huu unajumuisha mchakato mzima wa maendeleo ya teknolojia katika tafiti, mipango, uzalishaji, ugavi na matumizi yake; kwa kuzingatia kanuni maadili katika maendeleo, ili kuweza kuweka uwiano bora kati ya binadamu na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaweza kutoa mchango mkubwa katika azma hii kwa kuzingatia: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; haki na mshikamano unaoratibiwa na kanuni auni. Yote haya ni kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu bila ubaguzi wala mtu kutengwa!

Kanuni maadili na utu wema liwe ni daraja linalowakutanisha wadau katika maendeleo ya teknolojia kwa njia ya majadiliano; kwa kuzingatia uelewa wa ulimwengu na haki msingi za binadamu; haki na wajibu, ili kukabiliana na changamoto changamani kwa siku za usoni. Kanuni maadili na utu wema ni jambo la kupewa msukumo wa pekee kabisa katika mchakato wa maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kumbe, maadili, elimu na sheria ni mambo muhimu sana ya kuzingatiwa katika maendeleo ya teknolojia. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewataka wadau mbali mbali wa maendeleo ya sayansi na teknolojia kuendelea kufanya mang’amuzi na majadiliano na wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Papa: Akili Bandia
28 February 2020, 16:06