Tafuta

Vatican News
Papa Francisko amewataka waamini kuimarisha utume wa Sala kwa ajili ya kuliombea Kanisa na viongozi wake. Papa Francisko amewataka waamini kuimarisha utume wa Sala kwa ajili ya kuliombea Kanisa na viongozi wake.  (ANSA)

Papa Francisko: Waamini imarisheni utume wa Sala kwa ajili ya Kanisa!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sala ni nguvu ya Kikristo na kwamba, waamini wanapaswa kudumisha utume wa sala kwa ajili ya kuliombea Kanisa pamoja na viongozi wake wote. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanasali zaidi pale ambapo Kanisa linakabiliwa na mawimbi mazito katika maisha na utume wake, ili kumwalika Kristo awatie nguvu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu Jumapili ya VII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, akiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus wa Bari, Jimbo kuu la Bari-Bitonto, ametumia fursa hii kuwashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwaombea na kuwasindikiza Maaskofu Katoliki kutoka Ukanda wa Mediterania ambao kuanzia tarehe 19-23 Februari 2020 wamekuwa wakikutana mjini Bari ili kutafakari kwa kina mchango wa Mediterrania katika muktadha wa kudumisha amani. Baba Mtakatifu anasema, sala ni nguvu ya Kikristo na kwamba, waamini wanapaswa kudumisha utume wa sala kwa ajili ya kuliombea Kanisa pamoja na viongozi wake wote.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanasali zaidi pale ambapo Kanisa linakabiliwa na mawimbi mazito katika maisha na utume wake, ili kumwita na kumkaribisha Kristo Yesu, kuweza kuokoa Jahazi kabla mambo hayajaenda mrama! Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini waliokuwepo mbele ya Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus wa Bari kwamba, Bikira Maria daima analiombea na kulisindikiza Kanisa kwa ulinzi na tunza yake ya kimama. Kwa pamoja wamesali sala ya Salam Maria na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume!

Papa: Utume wa Sala

 

24 February 2020, 08:39