Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasitisha kabisa vita inayoendelea nchini Siria na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasitisha kabisa vita inayoendelea nchini Siria na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.  (AFP or licensors)

Viongozi wa Kanisa wanalilia amani kwa ajili ya watu wa Siria!

Viongozi wa Kanisa kwa pamoja wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasaidia kusitisha vita huko Mashariki ya Kati, ili hatimaye, amani iweze kutawala tena. Jumuiya ya Kimataifa, iwasikilize maskini na watu wasiokuwa na uwezo wa kujilinda wenyewe, kwa kuweka mbali mafao binafsi, ili hatimaye, kuweza kusimama kidete kulinda na kutetea maisha ya watu wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, akiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus wa Bari, Jimbo kuu la Bari-Bitonto, Jumapili, tarehe 23 Februari 2020 amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, tangu tarehe 19-23 Februari 2020 Maaskofu Katoliki kutoka katika nchi zinazouzunguka Ukanda wa Mediterrania wamekuwa mjini Bari kwa ajili ya kusali ili kuombea amani hasa kwa wananchi wanaoishi huko Mashariki ya Kati hasa Siria wanaoteseka kutokana na vita, nyanyaso na madhulumu ya kidini. Viongozi wa Kanisa kwa pamoja wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasaidia kusitisha vita huko Mashariki ya Kati, ili hatimaye, amani iweze kutawala tena. Jumuiya ya Kimataifa, iwasikilize maskini na watu wasiokuwa na uwezo wa kujilinda wenyewe, kwa kuweka mbali mafao binafsi, ili hatimaye, kuweza kusimama kidete kulinda na kutetea maisha ya watu wengi na hasa watoto wasiokuwa na hatia wanaoendelea kuathirika kutokana na vita!

Baba Mtakatifu anawaombea wadau wote katika mgogoro wa Siria ili waweze kuongoka na kuondokana na utamaduni wa chuki na tabia ya kutaka kulipiza kisasi, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja. Baba Mtakatifu anamwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia watu wote kumwilisha matendo ya huruma na upendo katika uhalisia wa maisha ya kila siku, ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano mapya ya kijamii, yanayofumbatwa katika hali ya uelewano, ukarimu, uvumilivu ili kuonja furaha ya Injili inayoweza kusambaa katika medani mbali mbali za maisha. Bikira Maria, Nyota ya Bahari, Mama wa Mungu, ambaye alikuwa mwaminifu kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu na kwa Neno lake, awasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutembea katika njia hii.

Baba Mtakatifu amewashukuru Maaskofu Katoliki wote walioshiriki katika mkutano wa Ukanda wa Mediterrania uwanja wa amani bila kuwasahau wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, tukio hili linapata ufanisi mkubwa. Wote hawa wamechangia kwa namna ya pekee katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana katika Ukanda wa Mediterrania, muhimu sana katika ujenzi wa amani duniani!

Papa: Siria

 

 

 

23 February 2020, 12:51