Papa Francisko: Kuwapenda na kuwaombea adui ni kiini cha Injili ya Kristo! Papa Francisko: Kuwapenda na kuwaombea adui ni kiini cha Injili ya Kristo! 

Papa Francisko: Kuwapenda na kuwaombea adui ni kiini cha Injili

Wapendeni na kuwaombea adui zenu ni mwaliko kwa waamini kujitahidi kuyamwilisha maneno haya machungu katika uhalisia wa maisha yao, kwa kuwapenda na kuwaombea adui zao. Kwa mwamini anayempenda Mungu kwa hakika hana adui moyoni mwake. Hii ni ibada ya kuondokana na utamaduni wa chuki na hali ya kutaka kulipizana kisasi. Muhimu: Kupenda na kuombea!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya kukutana na kuzungumza na Maaskofu Katoliki kutoka Ukanda wa Bahari ya Mediterrania, Jumapili tarehe 23 Februari 2020 alikwenda kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika uwanja wa Vittorio Emanuele ulioko kwenye Jimbo kuu la Bari-Bitonto. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia sheria mpya ya upendo, kwa kutambua kwamba, waamini wanapendwa na Mungu na wao pia wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya upendo hata kwa maadui zao. Wajizatiti katika mapambano dhidi ya utamaduni wa chuki, tabia ya kulipizana kisasi na litania ya malalamiko kwa kujikita katika msamaha wa kweli. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja kwa waamini kuomba neema na ujasiri wa kuweza kutekeleza mafundisho haya kwani kwa nguvu zao wenyewe hawawezi kufua dafu!

Baba Mtakatifu anasema, sheria ya jicho kwa jicho; na jino kwa kijino ilikuwa na madhara makubwa katika jamii. Kristo Yesu katika mafundisho yake anatoa mwelekeo mpya unaopaswa kufuatwa kwa kutoshindana na mtu movu wala kulipiza kisasi kwa kuwa umetendewa maovu. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo kwa watoto wake wote bila ubaguzi. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Mwenyezi Mungu anawataka watoto wake wote wawe watakatifu kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mtakatifu. Kwa maneno mengine, Mwenyezi Mungu anawaalika watoto wake kuishi vyema na kutafuta kila ambacho Kristo Yesu katika maisha na utume wake alivyofanya!

Hata akiwa pale juu Msalabani hakuwanyooshea watesi wake kidole kuwahukumu bali aliwafungulia mikono yake, akawasamehe na kuwaachia waigongomelee Msalabani. Hii ndiyo njia, dira na mwongozo kwa Wakristo. Mwenyezi Mungu amewapenda upeo, na wao wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo; wamesamehewa dhambi zao, wawe pia wepesi wa kusamehe! Wameonja upendo, wawe wa kwanza kuwaonjesha wengine huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wakristo wawe na ujasiri hata wa kuwapenda na kuwaombea adui na wale wote wanao wadhulumu na kuwatesa! Haya ni maneno aliyoyachagua Kristo Yesu mwenyewe kwa makusudi mazima! Huu ndio utofauti mkubwa unaopaswa kuoneshwa na Wakristo kwa kuwaombea na kuwapenda adui zao kwa kutambua kwamba, upendo wa Mungu hauna mipaka: Hiki ni kiini cha Injili na wala hakuna “cha salia Mtume”.

Hiki ni kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa. Wapendeni na kuwaombea adui zenu ni mwaliko kwa waamini kujitahidi kuyamwilisha maneno haya machungu katika uhalisia wa maisha yao, kwa kuwapenda na kuwaombea adui zao. Kwa mwamini anayempenda Mungu kwa hakika hana adui moyoni mwake. Hii ni ibada ya kuondokana na utamaduni wa chuki na hali ya kutaka kulipizana kisasi. Utamaduni huu unaweza kufyekelewa mbali kwa kwenda kinyume na litania ya malalamiko kwa kupenda na kusali. Haya ni mapinduzi makubwa ambayo yameletwa na Kristo Yesu katika historia ya maisha ya binadamu kwa kuwapenda na kuwaombea adui. Huu ndio mwelekeo sahihi wa maisha. Baba Mtakatifu anasema, kwa mtu anayependa, anatambua pia umuhimu wa kusamehe.

Hii inatokana na ukweli kwamba, hekima ya dunia hii ni upuuzi mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anaona mbali zaidi na anafahamu jinsi ya kushinda katika mapambano haya kwa sababu amemkomboa mwanadamu si kwa ncha ya upanga bali kwa njia ya Msalaba. Huku ndiko kupenda, kusamehe na kuishi kama mtu mwenye ushindi. Imani inaenezwa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na wala si kwa ncha ya upanga! Bustanini Getsemani, Mitume walitumia upanga, lakini wakawa wa kwanza “kuchanja mbuga na kutokomea kusikojulikana”. Maisha na utume wa Kristo Yesu ni mfano bora wa kuigwa: kwa kupenda kwa dhati kabisa katika hali ya unyenyekevu na kupenda upeo!

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa mahubiri yake anasema, mapinduzi haya yaliyoletwa na Kristo Yesu katika historia ya maisha ya mwanadamu ya kuwapenda na kuwaombea adui yanaonekana kana kwamba, ni jambo lisilowezekana kabisa! Ni kweli kwa nguvu za mtu binafsi si rahisi sana, kumbe, wanapaswa kuomba neema ya kujifunza kupenda na kusamehe. Waombe neema ya kuwaona jirani zao kuwa ni watu wanaopaswa kupendwa na kusamehewa na wala si vikwazo na vizingiti vya maisha. Changamoto kubwa ni kuomba neema ya kupenda na kuishi kadiri ya Injili ili kuwa ni Wakrisro kweli kweli! Waamini wathubutu kujenga utamaduni wa kupenda kwa dhati, hii ni changamoto kutoka kwa Kristo, changamoto ya upendo! Kwa njia hii, waamini watakuwa kweli Wakristo na dunia itajengwa zaidi kwenye msingi ya utu wema!

Papa: Mahubiri: Upendo na Sala
23 February 2020, 14:48